Ingawa Marekani daima inapiga ngoma ya vita na kutishia kuishambulia Iran kwa kutuma manowari na zana nyingine nzito za kijeshi katika maji yaliyo karibu na Iran, lakini ukweli wa mambo unaashiria hali tofauti kabisa.

Marekani inaitisha Tehran kwa kutuma kiasi kikubwa cha zana za kijeshi na askari  katika Asia Magharibi, haswa katika maeneo yanayozunguka Iran. Hata hivyo, kuna ushahidi wa wazi wa unaoonyesha uchakavu na uchovu wa kijeshi wa Marekani.

Manowari ya USS Gerald R. Ford (CVN-78), ya Jeshi la Wanamaji la Marekani na ambayo inagharimu dola bilioni 13, inachukuliwa kuwa nembo ya nguvu na utunishaji misuli wa nchi hiyo. Pamoja na hayo kuwa majini kwa muda mrefu kwa manowari hiyo bila mapumziko kumeanika peupe udhaifu wa manowari hiyo katika mfumo wa ulinzi wa Marekani. Gerald Ford, manowari ya bei ghali zaidi ya kivita na inayoendeshwa kwa nishati ya nyuklia, imetumwa Asia Magharibi baada ya kuwa kwenye misheni kwa muda mrefu usio wa kawaida. Ni wazi kuwa utumaji wa meli hiyo karibu na maji ya Iran unaipa changamoto kubwa katika kukabiliana na Tehran. Hasa ikitiliwa maanani kuwa, uchakavu wa juu umedhoofisha sana utayari wake wa kutekeleza operesheni za kijeshi.

Ijapokuwa Manowari ya Gerald Ford ilitumwa kwenye Bahari ya Mediterania kwa lengo la kukabiliana na Iran huku ikitia nanga karibu na bandari ya Haifa ya utawala wa Kizayuni, lakini kwa kutilia manani kuwa kwake safarini kwa takriban siku 300, ambayo itakuwa safari ndefu zaidi ya manowari hiyo baada ya Vita vya Vietnam, dalili za uchakavu wa chombo hiki na uchovu wa wanajeshi wake zinaonekana wazi. Meli hii imekuwa ikifanya kazi mfululizo tangu Juni 24, 2025 (takriban siku 238) na inatarajiwa kufikia siku 300 za misheni ifikapo Mei 2026. Kutumwa huku kwa muda mrefu kumeichosha Gerald Ford na hivyo kutoa changamoto kubwa kwa uwezo wake wa kukabiliana na Iran.

Gazeti la Kizayuni la Ma’ariv limesema katika muktadha huo kwamba wafanyakazi na askari waliomo kwenye manowari hiyo wanapinga kuongezwa muda wa majukumu yao. Likinukuu taarifa za vyombo vya habari vya nchi za Magharibi, gazeti hili limeeleza kuwa idadi kubwa ya wafanyakazi na askari wa manowari hii iliyotumwa eneo la Asia Magharibi kwa amri ya Trump, wameonyesha kukerwa kwao na kurefushwa kwa misheni yao na kutishia kwamba hawatahudumu tena katika Jeshi la Wanamaji baada ya kurejea nyumbani. Katika mahojiano na vyombo vya habari vya Marekani, baadhi yao wanalalamikia kuvurugwa kwa mipango yao ya maisha kutokana na kuongezwa muda wa majukumu yao na kusisitiza kuwa agizo la Rais wa Marekani la kuongeza muda wa kuhudumu manowari ya Gerald Ford kabla ya kwenda mapumzikoni linawatwika mzigo mkubwa pamoja na familia zao, na kuwa hali hii imepelekea idadi kubwa yao kuamua kuondoka jeshini mara tu watakaporejea nchini kwao.

Manowari ya Marekani ya Gerald Ford

Ingawa muda wa misheni za manowari za Marekani kwa kawaida ni kama miezi 6 hivi, wanajeshi kwenye meli hii wamekuwa baharini kwa zaidi ya miezi 8 huku wakiwa mbali na familia zao. Mmoja wa mabaharia alisikika akisema: ‘Wafanyakazi wamekasirika sana, baadhi yao wametangaza hadharani kwamba watajiuzulu mara tu watakaporudi nchini kwao.’

USS Gerald Ford imefanya kazi katika Bahari ya Kaskazini, Bahari ya Mediterania na Bahari ya Karibi tangu mwanzo wa misheni zake. Sasa, kwa kuituma katika eneo la Palestina inayokaliwa kwa mabavu, Washington inadai kwamba inashiriki katika kampeni ya mashinikizo ya juu kabisa dhidi ya Tehran. Hii ni katika hali ambayo kuwa baharini kwa muda mrefu bila kupumzika kwa manowari hii yenye teknolojia ya hali ya juu na gharama kubwa, kumesababisha uchakavu mkubwa na matatizo ya matengenezo pamoja na uchovu wa wafanyakazi wake.

Nukta muhimu hapa ni kwamba Jeshi la Wanamaji la Marekani hutumia Manowari ya Ford kama zana ya kudhihirisha nguvu, bila kujali mapungufu yake ya kiufundi na kibinadamu. Hili linatokana na ukweli wa Marekani kutokuwa na manowari za kutosha za kutekeleza operesheni za dharura wakati wa kuibuka migogoro ya kikanda na kimataifa.

Manowari ya Gerald Ford sio tu mfano wa uchakavu wa meli za kivita za Marekani, bali pia ni ishara kwamba nchi hii  huingia vitani bila mahitaji ya kutosha ya kiviwanda na kijeshi, kwa ajili ya kuidhaminia ushindi. Matatizo ya kimfumo na vizingiti vya kimsingi katika sekta ya kijeshi na manowari za Marekani hayawezi kutatuliwa katika muda mfupi. Kutokana na maendeleo yaliyopatikana katika mifumo ya makombora ya kuzamisha meli za kivita na upanuzi wa mifumo hii kati ya washindani wa Marekani, hatari ya kuzamishwa manowari ya Ford na meli nyinginezo za kivita za Marekani katika vita vya siku zijazo imeongezeka pakubwa. Suala hilo limeongeza wasiwasi mkubwa kwa viongozi wa Marekani na hasa katika wizara ya vita ya nchi hiyo Pentagon kwamba, Marekani ikipoteza hata manowari moja tu katika vita vijavyo, huenda isiwe na uwezo wa kuifidia inavyopasa.

Nukta nyingine muhimu ni kuwa, Rais Donald Trump wa Marekani alidhani kwamba, angeitisha Iran na kuifanya isalimu amri mbele ya matakwa yake yasiyo ya kimantiki wala kisheria, kwa kutuma vikosi vingi vya kijeshi, ikiwemo manowari ya Gerald Ford, katika maji yaliyo karibu na Iran. Hii ni katika hali ambayo kwa kusimama imara na kutahadharisha kuwa uchokozi wowote wa Marekani dhidi yake utakabiliwa na jibu kali na kusababisha vita vya kieneo, Iran sasa imepelekea utawala wa Trump kuchanganyikiwa na kutojua la kufanya kuhusiana na jambo hilo. Katika uwanja huo, Steve Witkoff, mwakilishi wa Trump katika mazungumzo na Iran, aliashiria katika mahojiano na shirika la habari la Fox News, kushangazwa Trump kuhusiana na kutotiswa Iran na vitisho vyake na kusisitiza kuwa, ameshangazwa kwamba licha ya mashinikizo haya yote makubwa ya manowari na wanamaji wa wa Marekani, lakini Iran bado haijasalimu amri mbele ya matakwa ya Marekani ili kufikia makubaliano. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *