Dar es Salaam. Kwa miaka mingi staa wa Bongofleva, Barnaba amewashirikisha waimbaji mbalimbali wa ndani na nje katika nyimbo zake na kupata matokeo mazuri kutoka kwa mashabiki wake.

Hata hivyo, amejijengea utamaduni wa kushirikiana na waimbaji wa kike na tayari amefanya kazi na wakali kama Linah (Wrong Number), Ray C (Watanionaje), Lady Jaydee (I Miss You) n.k. 

Ni Barnaba aliyeachia albamu tatu, Gold (2018), Refresh Mind (2020), Love Sounds Different (2022) pamoja na Extended Playlist (EP) moja, Mapenzi Kitabu (2020).

Kwa leo tutaangazia jinsi Barnaba alivyoshirikiana na baadhi ya waimbaji wa kike katika nyimbo zake tukianza na Vanessa Mdee, Nandy, Phina, Yammi na Abigail Chams.

1. Vanessa Mdee & Barnaba

Kabla ya Vanessa Mdee kutangaza kuachana na muziki takribani miaka mitano iliyopita, tayari alikuwa ameshirikiana na Barnaba katika nyimbo mbili ambazo zote zilipata mapokezi mazuri.

Nyimbo hizo ni Siri (2015) na Chausiku (2018) wake Barnaba na ndiye amehusika katika uandishi wa nyimbo zote hizo ambazo video zake zimebeba utamaduni wa uswahilini.

Ni Vanessa aliyetoka kimuziki baada ya kusainiwa na Bxtra Records, zamani B’Hits Music Group, ambapo alitoa wimbo wake, Closer (2013) ulioshinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) kama Wimbo Bora wa RnB 2014.

Baadaye alitoa albamu moja, Money Mondays (2018), akifanya kazi na Universal Music Group (UMG), huku akianzisha Mdee Music, rekodi lebo iliyokuja kuwasaini wasanii wawili, Brian Simba na Mimi Mars. 

2. Nandy & Barnaba

Hapa walikutana wasanii waliowahi kupata malezi ya kimuziki chini ya Tanzania House of Talent (THT), na kazi waliyoshirikiana ilifanya vizuri katika albamu ya tatu yake Barnaba, Love Sounds Different (2022). 

Mastaa hao waliachia kolabo yao, Tamu (2022) ambayo video yake iliongozwa na Director Hanscana, na hadi kufikia sasa imetazamwa YouTube zaidi ya mara milioni 7.3.

Tamu ni wimbo unaozungumzia mapenzi au uhusiano wenye furaha ambapo kila mmoja anashangaa jinsi anavyompenda mwenzake bila kuona kasoro yoyote ndani yake.

Ikumbukwe msanii wa kiume ambaye Nandy kashirikiana naye mara nyingi zaidi ni mumewe Billnass ambaye wametoa nyimbo tano, Bugana (2019), Do Me (2020), Party (2021), Bye (2022) na Totorimi (2024).

3. Phina & Barnaba

Huyu ni mshindi wa Bongo Star Search (BSS) 2018, na mshindi wa tuzo nne za TMA, hivyo Barnaba alichagua mtu sahihi kabisa wa kufanya naye kazi kwa sababu kipaji cha Phina ni kikubwa na kimewakosha wengi.

Wimbo wa Barnaba ambao Phina kasikika ni Hata Sielewi (2023) uliojumuishwa katika albamu yake, Love Sounds Different (2022) ambayo ilishinda tuzo ya TMA kama Albamu Bora ya Mwaka.

Utakumbuka awali, Phina alishinda tuzo ya TMA kama Msanii Bora Chipukizi 2021, ikiwa ni miaka 10 tangu msanii wa kike kufanya hivyo ambaye ni Linah aliyeshinda msimu wa 2011.

Tangu wakati huo, Phina ameendelea kufanya vizuri kupitia nyimbo zake kama Upo Nyonyo (2022), TiTiTi (2024), Sisi Ni Wale (2023), na Manu (2023), zote video zikitazamwa YouTube zaidi ya mara milioni 10.

4. Yammi & Barnaba

Picha tu za utambulisho wa wimbo wao, ziligeuka gumzo kubwa katika mitandao ya kijamii kwa sababu Barnaba tayari alikuwa katika ndoa na Raya, binti wa Mama Kimbo aliyetokea katika video ya wimbo wake, I Belong to You (2023).

Wawili hao waliachia wimbo uitwao Nibusu (2024), ukitayarishwa studio kwake, High Table Sound, na baadaye ilitoka remix yake wakimshirikisha Mbosso, kitu kilichofanya wimbo huo kuwa maarufu zaidi.

Kipindi kolabo hii inatoka, bado Yammi alikuwa akisimamiwa kimuziki na lebo yake Nandy, The African Princess ambayo alikuja kuachana nayo mwaka uliopita kwa makubaliano ya pande zote mbili.

Mbali na Barnaba, wasanii wengi waliomshirikisha Yammi, ni pamoja na Rayvanny (Usingizi), Abdukiba (You), Dully Sykes (Raha ya Tunda), Vanillah (Ok?), Kusah (Umekonda), Lava Lava (Aste Aste) n.k.

5. Abigail Chams & Barnaba

Wakati jina la Abigail Chams likiendelea kukua kwa kasi katika soko la muziki kimataifa, ndipo Barnaba akaona ni wakati sahihi wa kushirikiana naye kwa lengo la kuzidi kuinua juu chapa zote mbili.

Basi ikatoka kolabo yao, Kitu (2025) ambayo imetayarishwa na High Table Sound huku video ikisimamiwa na Director Joma ambaye sasa anafanya kazi na wasanii wengi wenye majina makubwa katika Bongofleva.

Huu ndio wimbo wa mwisho rasmi kwa Barnaba kuachia baada ya kufanya vizuri na kolabo yake ya pili na Diamond Platnumz, Salama (2025) ambayo video yake imetazamwa YouTube mara milioni 33.

Ikumbukwe Abigail Chams ambaye amesainiwa na Sony Music Africa, ndiye ni mwanamuziki wa kwanza wa kike kutokea Afrika Mashariki kuwania tuzo kubwa za muziki duniani za BET ambazo huandaliwa Marekani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *