Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Sayyid Abbas Araghchi amesema duru ya karibuni zaidi ya mazungumzo yasiyo ya ana kwa ana na Marekani iliyofanyia jana mjini Geneva, Uswisi ilikuwa moja ya mazungumzo bora, mazito zaidi, na marefu zaidi kuwahi kufanyika hadi sasa, na kwamba Tehran na Washington zimepiga hatua za “karibu zaidi kufikia mwafaka” katika baadhi ya masuala.

“Leo ninaweza kusema kwamba imefanyika moja ya duru nzito zaidi na ndefu zaidi ya mazungumzo yetu. Yamefanyika kwa takribani masaa manne asubuhi na masaa mawili jioni,” alieleza Araghchi mbele ya waandishi wa habari jana Alkhamisi baada ya mazungumzo ya Geneva.

Alisema majadiliano hayo yalifanyika kwa njia isiyo ya moja kwa moja kupitia upatanishi wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman Badr bin Hamad Al Busaidi, na kwamba mkuu wa shirika la nyuklia la Umoja wa Mataifa Rafael Grossi naye pia aliwasilisha hoja za kiufundi kati ya pande hizo mbili.

“Uwepo wake ulikuwa muhimu kitaalamu. Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman naye pia alitoa mchango wa maana, kama ilivyokuwa katika duru zilizopita,” ameongezea kueleza Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran.

“Kwa ujumla, wakati wa masaa haya marefu na mazito mno, zilipigwa hatua nzuri, na tuliingia katika mapitio mazito ya vipengele vya makubaliano, katika nyuga zote mbili za nyuklia na vikwazo”, amebainisha Araghchi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amefafanua kuwa, katika baadhi ya masuala, wamekaribia sana kufikia maelewano, na akafafanua kwa kusema “Bila shaka, kungali kuna kutokubaliana, jambo ambalo ni la kawaida, lakini ikilinganishwa na huko nyuma, pande zote mbili zinaonyesha kulipa uzito mkubwa suala la kufikia suluhisho la mazungumzo”. 

Aidha, amesema, imeafikiwa kwamba kuanzia Jumatatu, timu za kiufundi huko Vienna katika Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki zitaanza mapitio ya kina ya kiufundi ili kupanga baadhi ya masuala ya kiufundi kulingana na mfumo maalumu utakaowekwa, ambao baadaye utaendana na matakwa ya kisiasa na mambo ya mzingatio ya pande zote mbili.

Araghchi ameongeza kwamba imeamuliwa duru inayofuata ya mazungumzo ifanyike katika siku chache zijazo, muelekeo zaidi ukiwa ni katika kipindi cha chini ya wiki moja…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *