Dar es Salaam. Saa chache baada ya Singida Back Stars kutangaza kumsimamisha kwa miezi mitatu leo, Ijumaa, Februari 27, 2026, kiungo Khalid Aucho kwa kumtuhumu kuwa mtovu wa nidhamu, mchezaji huyo ameibuka na kukana tuhuma hizo.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Aucho amesema kuwa tangu alipoanza kucheza soka la kulipwa hajawahi kuwa mtovu wa nidhamu tofauti na tuhuma dhidi yake.

“Nimekuwa nikijibeba kwa weledi katika maisha yangu yote ya kazi, nikiwakilisha kila klabu kwa heshima na nidhamu. Katika miaka yangu yote ya soka, sijawahi kuhusika katika tukio lolote la utovu wa nidhamu kwa sababu ninaelewa wajibu unaokuja na kuwa mchezaji wa kulipwa.

“Kwa mashabiki wangu wapendwa ambao mmekuwa nami bega kwa bega siku zote, hali hii itapita. Asanteni kwa kuendelea kuniunga mkono,” amesema Aucho.

Leo, Singida Black Stars kupitia taarifa yake iliyotolewa na Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Jonathan Kassano imetangaza kumsimamisha mchezaji huyo kwa sababu za utovu wa nidhamu japo haikuweka bayana kosa/makosa aliyofanya.

Mbali na Aucho, Singida Black Stars pia imetangaza kumsimamisha kwa miezi mitatu, kipa wake Amas Obasogie kwa kumtuhumu kujihusisha na upangaji wa matokeo.

“Uongozi kupitia Kamati ya Nidhamu umechukua hatua hizi kwa mujibu wa kanuni na taratibu za klabu,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Wachezaji hao wamesimamishwa saa kadhaa baada ya timu hiyo kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Namungo FC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa jana, Alhamisi katika Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa Lindi.

Matokeo hayo yameifanya Singida Black Stars kupanda hadi nafasi ya 10 kwenye msimamo wa Ligi ikifikisha pointi 16.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *