Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limewawekea vikwazo makamanda wanne wa kundi la waasi la Rapid Support Forces (RSF) linalopigana na jeshi la Sudan, wanaoshukiwa kufanya ukatili dhidi ya raia ambao wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanasema ulikuwa na “ishara za mauaji ya kimbari.”

Makamanda hao wanne wa Rapid Support Forces, ambayo imekuwa vitani na jeshi la Sudan tangu 2023, wamewekwa kwenye orodha nyeusi kutokana na vitendo vyao huko el-Fasher, haswa mnamo Oktoba 26, siku ambayo wapiganaji wa RSF walitwaa makao makuu ya Darfur Kaskazini.

Ripoti zinaonyesha kwamba RSF ilifanya mauaji ya halaiki na ukatili mwingine huko el-Fasher baada ya kuuzingira mji huo kwa miezi 18. Maafisa wa Umoja wa Mataifa wanasema maelfu kadhaa ya raia waliuawa katika hujuma hiyo ya RSF dhidi ya el-Fasher.

Waliowekewa marufuku ya safari ya Umoja wa Mataifa na kufungiwa akaunti zao za fedha ni pamoja na manaibu makamanda wawili wa RSF, Abdul Rahim Hamdan Dagalo na Luteni Jenerali Gedo Hamdan Ahmed.

Rahim Dagalo, ambaye ni ndugu wa kamanda wa RSF, Jenerali Mohammed Hamdan Dagalo, ametajwa kuwa alikuwa katika kambi ya el-Fasher siku ilipotwaliwa na wanamgambo hao, kwa mujibu wa kamati ya Baraza la Usalama inayofuatilia vikwazo dhidi ya Sudan.

Kamati hiyo imesema: “Picha zinazoaminika kuwa za Dagalo zinamuonyesha akiwapa amri ya moja kwa moja wapiganaji wake wasichukue mateka bali waue kila mtu”.

Kamati hiyo ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa imesema ukatili uliofanyika unajumuisha mauaji yaliyolenga wasio Waarabu na ripoti za ukatili mkubwa wa kingono, ikiwa ni pamoja na ubakaji wa genge mbele ya jamaa za waathiriwa, na utekaji nyara wa watu, ikiwa ni pamoja na kushikilia wafanyakazi wa matibabu kwa ajili ya kudai fidia.

Kamati ya Umoja wa Mataifa imesema Ahmed, ambaye pia anajulikana kama Abu Nashuk, alikuwa mmoja wa majenerali sita huko el-Fasher na alionekana kwenye video pamoja na Dagalo mnamo Oktoba 26, wakati RSF ilipofanya mauaji ya halaiki dhidi ya raia.

Umoja wa Mataifa pia umemuwekea vikwazo Brigedia Jenerali Al-Fateh Abdullah Idris wa RSF, anayejulikana kama Abu Lulu na “Mchinjaji wa el-Fasher,” ukimtaja kuwa “mhusika mkuu” wa ukatili huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *