CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema Askofu Mkuu mstaafu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo alikuwa kiongozi wa kiroho mwenye hekima. Katibu Mkuu CCM, Dk AshaRose Migiro amesema hayo baada ya kusaini kitabu cha maombolezo katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu, Dar es Salaam.
Dk Migiro ametoa salamu za rambirambi kwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Jude Thaddeus Ruwa’ichi kutokana na kifo hicho na akasema amewasilisha salamu hizo kwa niaba ya Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Samia Suluhu Hassan.
Amesema Kardinali Pengo atakumbukwa kama mchungaji wa faraja na tumaini, mnyenyekevu na mwenye msimamo thabiti wa maadili. Kardinali Pengo aliaga dunia Februari 19, mwaka huu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) alipokuwa akipatiwa matibabu.
Dk Migiro amesema kiongozi huyo alijipambanua si tu kwa huduma ya kanisa, bali pia kwa mchango wake katika kuimarisha mshikamano wa kitaifa, maadili ya jamii, malezi ya vijana na uwajibikaji wa viongozi. “Kardinali Pengo ameacha alama inayodumu ya utumishi wa Mungu, utumishi wa taifa na utumishi wa jamii. Maisha na mafundisho yake yataendelea kuwa dira kwa vizazi vijavyo,” alisema Dk Migiro.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC), David Kafulila amesema Kardinali Pengo alikuwa kiongozi wa umoja asiyependa migawanyiko. Kafulila alisema hayo baada ya kusaini kitabu cha maombolezo cha kifo cha Kardinali Pengo katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu, Dar es Salaam.
Amesema kiongozi huyo alikuwa tayari kusimamia msimamo usiopendwa na wengi lakini unaounganisha na kulileta taifa pamoja. Kafulila amesema Kardinali Pengo alikuwa ni Mtanzania, kiongozi na Mkristo aliyetumia muda wake kutimiza kile Mwenyezi Mungu alichomkusudia ndani yake ambacho kilikuwa ni kujenga jamii yenye maelewano.

Amesema Kardinali Pengo aliamini ujenzi wa taifa lenye uimara zaidi kwa kutumia jukwaa alilonalo kama kiongozi wa dini, pia hakusita kuongea analoamini ni sahihi na wakati mwingine haijalishi kikawa au sivyo, lakini muhimu ni sahihi. “Kama taifa tunapaswa kumuezi Kardinali Pengo kama binadamu na kiongozi aliyekuwa anaamini katika umoja wa kitaifa, alikuwa kinyume na kitu chochote kilichokuwa kinaweza kusababisha taifa kugawanyika,” alisema Kafulila.
Amesema Kardinali Pengo alikuwa tayari kusimamia msimamo usiopendwa lakini tu anaamini kuwa ni msimamo unaleta taifa pamoja, kwani kuna wakati unaweza kusimamia msimamo unapendwa, lakini ni ambao unaokwenda kusambaratisha taifa. Pia, amesema kiongozi huyo alipanga fikra kwa mambo anayazungumza na maoni yake yalikuwa yanajengwa kwenye fikra na si upepo unavyosema.
“Tunapozungumza ujenzi wa taifa katika mazingira ya leo ambayo taifa au dunia inaongozwa na habari, maoni ya watu kwa kiasi kikubwa ukomo wake unakuwa ni mdogo kwani dunia yenyewe imejaa ulaji wa habari,” alisema. SOMA: Kardinali Pengo azuru kaburi la JPM
Ametoa wito kwa viongozi wa dini kufuata somo lililoachwa na Kardinali Pengo la kulifanya taifa kuwa moja ni kipaumbele na kusimamia msimamo huo bila kujali unamuitikio gani katika jamii ya mitandao ya kijamii iliyochanganyikana na mashambulizi yake ni makali kiasi gani.