Mohamed El-Baradei, aliyewahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA), ameionya Marekani kuhusu madhara makubwa na ya kutisha yatakayojitokeza iwapo itaingia katika vita vingine dhidi ya Iran, huku akipinga hoja za Washington zinazodai kuhalalisha uchokozi huo mpya.

El-Baradei aliandika kwenye mtandao wa X siku ya Jumatano akisema: “Marekani inaongeza kasi ya ngoma za vita dhidi ya Iran.”

Aliongeza kuwa: “Vita vyote, ikiwemo vile vinavyochaguliwa kwa hiari, vina gharama za kutisha. Ndiyo maana kuna vikwazo na mipaka iliyowekwa na kanuni za kimataifa.”

Aliyekuwa mkuu shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia masuala ya nyuklia amesema pia kuwa katika kadhia ya nyuklia ya Iran, Marekani imetoa hoja za kinadharia zinazojengwa juu ya uwezekano wa nia za baadaye.

Rais wa Marekani Donald Trump amezidisha kwa kiasi kikubwa matamshi yake ya vitisho dhidi ya Iran, sambamba na kuamuru kuongezwa kwa mkusanyiko mkubwa wa majeshi ya nchi hiyo katika eneo la Asia Magharibi, ikiwemo maeneo yanayozunguka Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Mwezi uliopita pia, El-Baradei, mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, alikosoa vikali vitisho vinavyozidi kuongezeka vya Marekani kuhusu hatua za kijeshi dhidi ya Iran. Alisema: “Vitisho vya upande mmoja vya kuishambulia Iran, bila kuwepo hatari ya wazi na ya sasa, na kinyume na sheria za kimataifa; vinanikumbusha hali ile ile ya kutisha kabla ya vita haramu na visivyo vya kimaadili dhidi ya Iraq, vilivyojengwa juu ya uongo na kisha kusababisha madhara ya kutisha.”

Alikuwa akiashiria madai ya wakati huo ya nchi za Magharibi kwamba Iraq ilikuwa inamiliki silaha za maangamizi ya umati ili kuhalalisha uvamizi uliokuwa ukiongozwa na Marekani dhidi ya nchi hiyo ya Kiarabu.

Uvamizi huo ulisababisha vifo vya maelfu ya watu, huku madai hayo yakithibitika baadaye kuwa hayakuwa ya kweli.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *