
Dar es Salaam. Baada ya kupata kigugumizi wakati wa kujinadi kwa lugha ya Kiingereza, mbunge wa Ukonga (ACT Wazalendo), Bakari Shingo, amesema si lugha hiyo iliyomkwamisha kujieleza, bali kuna mengine yaliyosababisha kile kilichoshuhudiwa.
Shingo alipata kigugumizi hicho Februari 5, 2026, alipokuwa akijinadi bungeni jijini Dodoma kuomba nafasi ya Uwakilishi wa Tanzania katika Umoja wa Mabunge ya Nchi za Maziwa Makuu, ambaye kutoka upinzani alikuwa mgombea pekee.
“I’m Bakari Shingo from Ukonga… excuse me… ah… ah… excuse… ooh… dah…” alisikika Shingo na baadaye kuketi katika kiti chake, kisha kuinuka na kuomba kwa lugha ya Kiswahili, huku wabunge wakiangua kicheko na wengine kugonga meza.
Hata hivyo, katika nafasi hiyo, Shingo alishinda kwa kupata kura 242 kati ya 301 zilizopigwa.
Shingo amezungumza hayo wakati wa mahojiano maalumu yaliyofanyika katika ofisi za Mwananchi Tabata Relini, jijini Dar es Salaam.
Akisimulia ilivyokuwa, Shingo amesema wakati wa mchakato wa kuomba nafasi hiyo, alijaza fomu siku tatu kabla, na alidhani bunge hilo linawakilishwa na nchi sita.
Amesema yuko mtu mmoja aliyemwambia kuwa nchi zimeongezeka na kufikia 12, hivyo alizitafuta na kujua mabadiliko yake ili kujipanga na swali lolote atakaloulizwa.
“Nikawa nasoma zile sera, nikawa nimeandaa sera na nimejua nchi ziko ngapi, ziko 12, sera zake zikoje, na wakati nimekaa pale bungeni niliwasha kishikwambi changu, nikawa nadonoa maeneo ambayo nahisi ingewezekana kuulizwa,” amesema.
Mbunge huyo amesema alikuwa akifanya hivyo huku akiandaa baadhi ya taarifa ambazo zingekuwa majibu ya maswali mbalimbali ambayo alihisi angeulizwa.
Wakati huo, amesema akili na mawazo yake yote aliyapeleka kwenye kusoma alichokiandaa, na hata Spika alipomwita mara ya kwanza hadi ya tatu hakuwa amesikia, kwa kuwa alidhani muda wake bado, kumbe ulishafika.
“Nilivyonyanyuka, mkono wa kushoto inaonekana uligusa kitufe fulani, ile kazi ikapotea. Nilivyonyanyuka kusalimia, naitafuta ile kazi, wakati naangalia nizungumze nini, kazi ikawa haipo, ikaniondoa kwenye reli,” amesema.
Ameeleza alijaribu mara kadhaa kuirudisha kazi ili aendelee kujinadi katika nafasi anayoiomba, lakini ilishindikana, ndiyo maana yakatokea yaliyomtokea.
‘Kiingereza kisitubabaishe’
Shingo amesema, pamoja na yale yaliyomtokea, lugha ya Kiingereza isitazamwe kuwa ndiyo msingi wa ukombozi wa maendeleo, akirejea kuwa Tanganyika ilipata uhuru ikiwa na idadi ndogo ya wasomi, na wananchi walikula na kutibiwa bure katika hospitali.
Amefananisha na kipindi cha sasa chenye wasomi wengi katika kila eneo na nafasi mbalimbali, lakini kunashuhudiwa matumizi makubwa ya kifahari kuliko ubora wa huduma za kijamii.
Msisitizo wa Shingo ni kile alichosema, ni muhimu kuwekeza kwenye fani badala ya lugha, kama ilivyo China, aliyosema imeendelea lakini hawajui vema Kiingereza.
“China wanafanya vizuri duniani, wanajua Kiingereza au ni Waingereza?” amehoji.
Katika ufafanuzi wake kuhusu hilo, amesema ameingia kwenye semina ya Bunge la Maziwa Makuu na amepewa vitabu viwili– kimoja kina lugha ya Kiswahili na kingine Kiingereza, na kuna programu aliyopewa kumwezesha kutafsiri.
“Nimepewa programu ya kutafsiri lugha, unalipia kiasi kidogo cha fedha chini ya Sh20,000 kwa mwezi, kila unachotaka kwa lugha yoyote inakuletea. Shida iko wapi?” amesema.
Hata hivyo, mwanasiasa huyo amesema hawezi kujivunia kujua au kutokujua Kiingereza, kwa kuwa yeye si Muingereza na hana utaalamu zaidi wa lugha hiyo.
“Mtu asijione anajua Kiingereza akajiona wa maana zaidi, tena sasa hivi bungeni wametupa vishikwambi, lugha yoyote duniani ipo,” amesema.
Alipoulizwa kwa nini hakuanza kutumia Kiswahili wakati wa kujinadi, amesema hakufanya hivyo kwa sababu alijua hotuba na maswali ambayo angeulizwa yangekuwa ya Kiingereza.
“Nilikuwa sijayaleta kwenye Kiswahili, na nilijua nitaulizwa kwa lugha hiyo, kwa hiyo nilitaka kuyazungumza hayo kwa lugha hiyo,” amesema.
Katika maelezo yake, amesema uwezo wake wa Kiingereza ni pale anapokuwa na vitendea kazi, hawezi kukwama kwenye shughuli yoyote.
“Nikiwa na vitendea kazi, nakijua sana, najua namna ya kukitumia. Yaani, siwezi kukwama kwenye shughuli yoyote kwa sababu eti ulimi wangu mzito au mwepesi,” amesema.
Lakini amesema, kwa dunia ya sasa, kama Kiingereza kingekuwa cha maana, Tanzania ingeshakuwa tajiri kama China.
Mtazamo wake kuhusu uchaguzi 2025
Alipoulizwa kuhusu madai ya uchaguzi huo kutokuwa huru na haki, Shingo amesema hawezi kusema kuwa hakukuwa na uchaguzi huru na haki, kwani katika jimbo lake alishinda katika mazingira ya haki.
“Katika jimbo langu mimi, sina mamlaka, sina dola. Wasiwasi wangu ulikuwa kutangazwa, na huwa tunajua wapinzani tunapigwa. Wananchi waliniuliza tunalindaje kura, nikawaambia tusubiri wakati ufike,” amesema.
Ameeleza wasiwasi wake ulikuwa wakati wa majumuisho na vurugu zilizotokea, pengine ataelezwa inashindikana kujumuisha.
“Kata mbili hatukufanikiwa kufanya majumuisho, lakini watu walikuwa na kura, na wasiwasi wangu ukawa isije kukosa majumuisho yale ukawa ndiyo mwanya wa mimi kupigwa, ikabidi tukaweke kambi kwenye kituo cha kujumuisha,” amesema.
Amesema kila hatua ya majumuisho alikuwepo akishuhudia na kuhakikisha anatangazwa, hasa ukizingatia kuna mazingira ya kupigwa nyakati za mwisho.
Ameeleza kilichotokea mpinzani wake, Jerry Silaa, alikamatwa akawekwa mahabusu kwa siku zaidi ya mbili, naye akatangazwa kuwa mbunge wa Ukonga.
Katika msisitizo wake, Shingo amesema hana mashaka na haki iliyofanywa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) katika jimbo la Ukonga.
“Maeneo mengine, watu wote wanaolalamika wana akili, na ukitaka kuamini kuwa kuna shida, si unaona kuna tume ya Rais? Inakusanya maoni ya nini si ya uchaguzi, yaliyotokea na kilichosababisha? Maana yake kuna shida,” amesema.
Amesema ni imani yake kuwa bila nguvu ya dola, Chama cha Mapinduzi (CCM) hakiwezi kupata ushindi kwenye uchaguzi wowote nchini.
“Ndio maana kwenye kampeni zangu nilikuwa nawaambia polisi waniachie mtu wangu. Kote nilikokuwa nikifanya mikutano, nilichokuwa naomba ni polisi waniachie mtu wangu, na nashukuru, polisi waliniachia mimi na mtu wangu (Silaa),” amesema.
Ili uchaguzi uwe huru na haki, amesema ni muhimu kuwepo jukwaa la kuwasikiliza wananchi waeleze maeneo gani wanahitaji yaboreshwe.
Miongoni mwa mambo yanayopaswa kushughulikiwa kuhusu uchaguzi, amesema ni watendaji wa INEC wasitokane na kuteuliwa, badala yake waombe kazi, na kusiwe na mamlaka yenye uwezo wa kumtoa madarakani ili awe huru.
Tume ya uchunguzi Oktoba 29
Katika maelezo yake, Shingo amesema anaunga mkono utendaji wa tume iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuchunguza vurugu za Oktoba 29, 2025.
Amesema anachokiunga mkono ni hatua ya mamlaka kutambua kuna shida na kuamua kuunda tume hiyo.
Alipoulizwa kuhusu chama chake ambacho kiliipinga tume hiyo, amesema anaendelea kuuheshimu msimamo wa chama kwa kuwa vikao ndivyo vinavyoamua, lakini yeye binafsi kilichofanywa na Rais Samia ni sawa.
“Kwa tafsiri yangu mimi, alichokifanya Rais ni kitu kizuri kwa sababu ametambua kuna shida na anaona hatupaswi kurudi,” amesema.