ZAO la embe ni fursa kubwa sana katika kujipatia uchumi endelevu lakini bado wakulima au jamii kwa ujumla haijatambua na kuona kuwa kilimo hiki ni fursa kama ilivyo kwa kilimo cha mazao mengine ya biashara yanayolimwa kwenye maeneo mbalimbali nchini kama vile ufuta, korosho na mengine.
Tanzania nzima maeneo yote tunayopita iwe barabarani au kwenye makazi ya watu ni lazima tunakutana na miti ya maembe ila bado jamii yetu haijaona kuwa kama ni fursa kubwa kiuchumi na yanaweza kuwa kama mazao hayo mengine ya biashara.
Maembe ni sehemu ya kilimo cha mboga mboga na matunda kama ilivyokuwa parachichi, mapapai, ndizi, nyanya, machungwa na mengine ambayo uchumi wake ni endelevu kwa sababu ni kilimo cha muda wote endapo wakulima watawekeza nguvu kubwa kwenye kilimo hicho.
Licha ya sehemu ya jamii kushindwa kutupia nguvu au jicho kwenye fursa hiyo lakini wapo wazalishaji wakubwa ambao wameona fursa ya kilimo hapa nchini na wanazalisha na kupeleka sokoni na wamekuwa wakijiingizia kipato. SOMA: Upotevu wa nafaka wapungua hadi asilima 20
Pamoja na changamoto hiyo lakini sasa zao hilo la embe limeshapatiwa majawabu na wizara husika kwa kuhakikisha inaendelea kuwekeza kwenye kilimo hicho hususani suala la dawa za kukabiliana na inzi wa maembe. Pia, kuhakikisha zao hilo linakuwa sehemu ya mazao mbalimbali ya biashara yanayozalishwa nchini kama vile parachichi, korosho, ufuta, mbaazi na mengine.

Kitu cha kushauri kuhusu zao hilo la embe ni kwamba serikali kwa kushirikiana na taasisi binafsi ziendelee kuhakikisha wanaweka nguvu zaidi kwenye zao hicho ili kuendelea kuibua fursa ya kilimo hicho katika jamii. Lakini jamii yenyewe pia inawajibu wa kuona ni wakati sasa wa kutumia kila fursa inayojitokeza mbele yao wachangamkie hususani kwenye kilimo kama hicho cha maembe, parachichi na mengine kwa sababu wakishalima na wakavuna mazao hayo na yakaingia sokoni mkulima anaondokana na suala la umasikini.
Katika suala la kukuza uchumi hasa unaotokana na kilimo ni kwamba mkulima anapaswa kuondokana na utamaduni wa kuzalisha zao moja pekee na badala yake ajikite kuzalisha mazao tofauti tofauti ili kupata uchumi endelevu kama vile parachichi, nyanya, mahindi, viazi mviringo na mengine.
Hali hiyo inasaidia mkulima kuwa ndani ya mwaka mzima atajikuta anafanya kazi ya kuzalisha mazao na kuyaingiza sokoni akishauza anapata fedha za kujikimu na familia, kwa hiyo unakuta suala la umasikini kwake inakuwa ni historia kwa sababu anazalisha mazao yanayomletea uchumi endelevu.
Kiuhalisia mazao ya mboga mboga na matunda licha ya kuwa ni lishe kwenye mwili wa binadamu lakini yanaleta na kumfanya mkulima kuwa na uchumi endelevu na wa kudumu katika maisha yake ya kila siku. Tukija kuangalia umuhimu wa kilimo hicho cha embe au mboga mboga na matunda kwa ujumla ni kwamba kinamsaidia mkulima kuwa uchumi mbadala wa mazao ya biashara yanayozalishwa kwa msimu katika baadhi ya maeneo ikiwemo korosho, ufuta, mbaazi, choroko na mengine.
Kilimo cha matunda hakina msimu bali ni endelevu kwa sababu mbali na kutegemea mvua lakini kuna kilimo cha umwagiliaji na serikali kupitia wizara husika imewekeza miradi mingi ya umwagiliaji katika maeneo mengi nchini. Lengo ni kumuwezesha mwananchi au mkulima kufanya kilimo endelevu kupitia umwagiliaji ili azalishe zaidi ndani ya mwaka mzima.