Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un, ametishia “kumfuta kabisa” jirani yake wa kusini iwapo usalama wa nchi yake utatishiwa, akiitaja Korea Kusini kuwa ndiyo “kitu chenye uadui mkubwa zaidi” na kutupilia mbali uwezekano wowote wa kufanya mazungumzo na nchi hiyo.

Haya yamesemwa mwishoni mwa mkutano wa tisa wa Chama tawala cha Wafanyakazi, ambapo Kim alitumia lugha kali dhidi ya Seoul, akizitaja juhudi za hivi karibuni za amani za Korea Kusini kuwa “za udanganyifu”.

Kwa upande wake, Seoul amejibu kwa lugha ya utulivu, huku Rais wa Korea Kusini, Lee Jae Myung akisema jana Alkhamisi, kwamba juhudi za kujenga hali ya kuaminiana na kupata msingi wa pamoja na Korea Kaskazini “lazima ziendelee” ili kupatikana amani na utulivu katika Rasi ya Korea.

Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un pia amehusisha “maelewano” yoyote na Marekani na utambuzi wa Washington kwamba Pyongyang ni taifa lenye nguvu za nyuklia kama ilivyoainishwa katika katiba yake, na kuacha sera ya uadui.

Shirika la Habari la Korea Kusini limemnukuu Kim akisema kwamba upeo wa uhusiano baina ya pande hizo mbili yanategemea kabisa msimamo wa Washington.

Mkutano wa chama tawala, ambao unaainisha mwelekeo wa miaka mitano ijayo, umehitimishwa kwa gwaride kubwa la kijeshi katika Uwanja wa Kim Il-sung, ambapo Kim Jong-un amesisitiza kuimarishwa mifumo ya silaha za kisasa ili kuimarisha silaha za nyuklia za nchi hiyo. Mifumo hiyo inajumuisha makombora ya masafa marefu yanayorushwa kutoka bara moja hadi jingine yanayoweza kurushwa kutoka chini ya maji na silaha za nyuklia za kimkakati zilizoelekezwa hasa kwa jirani yake wa kusini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *