Dar es Salaam. Mabasi 100 mapya yaliyoletwa na kampuni ya uendeshaji mabasi ya Mwendo wa haraka ‘mwendokasi’ (Udart) yatatumika kutoa huduma kwa mradi wa awamu ya tatu wa mabasi hayo inayohusisha Barabara ya Nyerere kutoka mjini kwenda Gongo la Mboto.
Hayo yamesemwa na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa mabasi Yaendayo Haraka (Dart), Said Tunda, alipokuwa akitoa taarifa kwenye ziara ya makatibu wakuu wenye jukumu la kusimamia urejeshaji na uboreshaji wa hali ya usafiri nchini walipotembelea miundombinu inapopita mabasi hayo jijini Dar es Salaam.
Mabasi hayo 100 yanayotumia gesi , yaliingizwa nchini na Udart mwezi mmoja uliyopita yakitanguliwa na moja lililoletwa kwa ajili ya majaribio.
Awali, yalikuwa yaingizwe katika njia ya Kimara kuongeza nguvu baada ya yaliyokuwepo kuharibika hadi kubaki 30 yaliyokuwa yakitoa huduma.
Akizungumza katika ziara hiyo leo Ijumaa Februari 27, 2026, Tunda amesema mabasi hayo yanaelekezwa Gongo la Mboto baada ya mwekezaji aliyepewa njia ya Kimara ambaye ni Trans Dar, kutarajia kuleta mabasi yake nchini ifikapo Julai mwaka huu.
“Kwa kuwa mwenye njia yake sasa anakuja, Udart waliokuwa wanatoa huduma katika kipindi cha mpito itabidi waondoke na mpango ni kwenda kuanza kutoa huduma Barabara ya Gongo la Mboto,” amesema.
Hata hivyo, alipoulizwa ni lini huduma hizo zitaanza kutolewa, Tunda amesema hawezi kuitaja kwa kuwa ukamilishwaji wa miundombinu wala kukabidhiwa barabara hiyo na wanaoijenga bado hakujafanyika.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Uendeshaji Mbasi ya Mwendo wa Haraka( Udart), Pius Ng’ingo amesema katika utoaji huduma kwa Gongo la Mboto wana magari ya kutosha, ukiacha hayo 100 mapya yapo 50 tayari yameshatengenezwa na mengine yanaendelea kutengenezwa.
Katika Barabara ya Gongo la Mboto jumla ya mabasi 200 yatahitajika kutoa huduma.
Awali akifanya majumuisho katika ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Makatibu hao, ambaye pia ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Dk Jim Yonazi, amesema wameridhishwa na namna Serikali ilivyofanya uwekezaji wa miundombinu ya mabasi hayo na kufanya hali ya usafiri kuwa bora wa haraka na wa raha kwa wananchi.
“Tayari hapa tumeambiwa kuna kampuni zimeshaleta mabasi ikiwamo Mofat walioleta mabasi 200, Udart 100 na mengine ya Trans Dar yako njiani kuja. Baada ya kuingizwa kwa mabasi hayo ni kuona yanafanya kazi ambapo Jiji la Dar es Salaam litakuwa moja ya miji yenye usafiri bora na wa kisasa,” amesema Dk Yonazi.
Hata hivyo Katibu huyo amesema uwepo wa usafiri huo sio tu unaleta usafiri mzuri lakini pia unazalisha ajira.
Kilio cha daladala kuathiri mwendokasi Mbagala
Katika hatua nyingine, Kilio cha athari ya kuendelea kuwepo kwa daladala katika barabara ya Mbagala na kuathiri utendaji kazi wa mabasi yanayotoa huduma huko kimetua kwa makatibu wakuu hao.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mofat wanaoendesha mradi huo kwa Mbagala, Mohammed Kassim Abdallah amewaambia makatibu hao ni kutokana na wingi wa daladala kati ya mabasi 200 waliyoleta ni 43 tu ndio yanayofanya kazi hadi sasa.
Alipoulizwa kama daladala zikiondolewa watakidhi kutoa huduma, Abdallah amesema kwa idadi ya mabasi waliyonayo wana uwezo wa kusafirisha hadi abiria milioni moja kwa siku.
Akitoa maelekezo kuhusu daladala, Dk Yonazi amesema kutawekwa utaratibu maalumu wa kuziondoa daladala hizo bila kuathiri wengine.
“Uendeshaji usafiri kwenye miji mikubwa kama Dar es Salaam huwa inawekwa utaratibu wake maalumu. Pia, Serikali kushirikiana na sekta binafsi ambao ni pamoja na hawa wamiliki wa daladala, kwa hiyo watapangiwa utaratibu mzuri tu namna ambayo watashiriki kuhakikisha usafiri wa Dar es Salaam unakuwa mzuri,” amesema Yonazi.
Ameongeza kuwa, wanafanya hivyo kwa kuwa Serikali inatambua namna daladala zilivyotengeza ajira, hivyo ni vema kupangiwa utaratibu mzuri ili nazo ziendelee kushiriki kutoa huduma.
Katibu mkuu huyo amesisitiza kuwa, Serikali haina mpango wa kumnyima mtu fursa lakini fursa hizo zitapangwa vizuri ili kuweka miji katika utaratibu wa kimataifa na kuvutia watu waweze kutembea vizuri, kusafiri na hatimaye kila mmoja kushiriki katika uchumi wa nchi.
Akilifafanua hilo, Mkurugenzi wa Dart, Said Tunda amesema katika utoaji huduma hizo za usafiri kila mmoja amewekeza hela, hivyo huwezi kusema kwa siku moja daladala zote ziondoke.
Tunda amefafanua kuwa, katika kulishughulikia hilo, kadri leseni za daladala zitakavyokuwa zinamaliza muda wake, zitaondoka taratibu.
“Ni kama umejenga kiwanda cha kuzalisha bidhaa fulani, huwezi kusema kwa siku moja utazalisha kwa asilimia 100. Vivyo hivyo kwa daladala huwezi kuziondoa, japo tayari kuna makubaliano ya ndani leseni za wenye daladala zikiisha wasiongezewe tena muda na mwisho wa siku zitaondoka taratibu hadi kuisha,” amesema.