Chanzo cha picha, Foreign Ministry of Oman
Waziri wa
mambo ya nje wa Oman amesema maafisa wa Marekani na Iran wamepata “maendeleo makubwa” katika mazungumzo ya nyuklia huko Geneva,
lakini uwezekano wa kuwepo kwa makubaliano ambayo yanaweza kuzuia vita bado hauko
wazi.
Badr
Albusaidi, ambaye alikuwa mpatanishi, amesema pande hizo mbili zimepanga kuanza
tena mazungumzo “hivi karibuni,” na majadiliano ya ngazi ya kiufundi
yatafanyika wiki ijayo huko Vienna.
Waziri wa
Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi, ambaye aliongoza ujumbe wa nchi yake, amesema “maendeleo mazuri” yamepatikana, ingawa kuna makubaliano
kuhusu baadhi ya masuala, bado kuna tofauti kuhusu masuala mengine.
Amesema duru
inayofuata ya mazungumzo itafanyika katika kipindi cha chini ya wiki moja.
Matarajio ya
kuwepo kwa mazungumzo zaidi yanaweza kupunguza uwezekano wa Rais Donald Trump
kuishambulia Iran.
Trump
ameamuru kupelekwa wanajeshi wengi wa Marekani katika Mashariki ya Kati, ikiwa
ni idadi kubwa tangu uvamizi wa Marekani nchini Iraq mwaka 2003, huku Iran
ikiapa kujibu shambulio lolote.
Kwa miongo
kadhaa, Marekani na Israeli zimeishutumu Iran kwa kujaribu kutengeneza
silaha ya nyuklia kwa siri. Iran imekana mara kwa mara kwamba inaunda bomu hilo
na inasema mpango wake ni wa amani tu, ingawa nchi hiyo ndiyo taifa pekee
lisilo na silaha za nyuklia ambalo limeongeza urani katika kiwango cha karibu
cha silaha.
Kulingana na
vyombo vya habari vya serikali ya Iran, wapatanishi walisisitiza kwamba Iran
ina haki ya kuwa na nishati ya nyuklia ya amani na walikataa madai ya Marekani
ya kusimamisha kabisa urutubishaji wa urani na kuhamisha akiba yake ya kilo 400
(880lb) ya urani iliyorutubishwa kutoka nchini humo.
Ingawa
mapendekezo hayo hayajawekwa wazi lakini mojawapo ya chaguzi zilizoripotiwa ni
Iran kuruhusiwa kurutubisha urani kwa kiwango kidogo chini ya ufuatiliaji wa
kimataifa.
Na kwa upande wa Iran, Araghchi ameiambia
televisheni ya Iran kwamba wapatanishi wao wanataka kuondolewa kwa vikwazo
ambavyo vimedhoofisha uchumi wa Iran.
Mazungumzo
hayo yasiyo ya moja kwa moja yalifanyika katika vikao viwili. Kipindi kimoja
asubuhi, ambacho kilidumu kwa saa tatu, na kingine, kifupi jioni. Hakuna
kauli ya Marekani kuhusu matokeo ya mkutano huo.
Kama
ilivyokuwa katika raundi zilizopita, Marekani iliwakilishwa na mjumbe maalum
Steve Witkoff na mkwe wa Trump, Jared Kushner. Rafael Grossi, mkuu wa shirika
la kimataifa la ulinzi wa nyuklia, Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki
(IAEA), pia alijiunga na mazungumzo hayo.
Iran tayari
imekataa kujadili mipaka ya mpango wa makombora ya balestiki na
kukomesha uungaji mkono wake kwa washirika wake katika eneo hilo, ikiwa ni
pamoja na Hamas huko Gaza, Hezbollah huko Lebanon, wanamgambo nchini Iraq, na
Houthi huko Yemen.