Marekani. Msanii wa muziki wa Latin trap na reggae, Bad Bunny ameandika ukurasa mpya katika ulimwengu wa soka baada ya kuvaa jaketi lililovaliwa na gwiji wa soka Brazil, Pele wakati wa Kombe la Dunia la mwaka 1966.

Bad Bunny alivaa jaketi hilo kwenye tamasha lake la kwanza kufanyika katika ardhi ya mabingwa hao mara tano wa Kombe la Dunia, jijini São Paulo, Brazil.

Jaketi hilo la kihistoria linatajwa kuwa sehemu ya kumbukumbu adimu za soka duniani, likiwa ni miongoni mwa vitu vilivyovaliwa na Pelé katika enzi zake za uhai.

Pelé aliyefariki dunia mwaka 2022 akiwa na umri wa miaka 82, anasalia kuwa mchezaji pekee kushinda mataji matatu ya Kombe la Dunia (1958, 1962 na 1970), rekodi ambayo bado haijavunjwa hadi leo.

Mbali na kuvalia jaketi hilo, msanii huyo aliimba wimbo maarufu wa ‘Monaco’ wenye maneno ‘Kufunga bao baada ya Messi na Maradona’ huku yeye akisema ‘Kufunga bao baada ya Pele na Maradona’ kumpa heshima mwanasoka huyo.

Baada ya shoo hiyo, akaunti ya Instagram ya Pele ilimshukuru msanii huyo kwa kuthamini urithi wa soka la Brazil.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *