MWILI wa Askofu Mkuu mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo (81) unaagwa leo katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu, Dar es Salaam. Kardinali Pengo aliaga dunia usiku wa Februari 19, wakati akipatiwa matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dar es Salaam.

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Jude Thaddaeus Ruwa’ichi amesema leo mwili wa Kardinali Pengo utachukuliwa Hospitali ya Jeshi Lugalo, Dar es Salaam na utapelekwa katika kanisa hilo. Ruwa’ichi aliwaeleza waandishi wa habari kanisani hapo kwamba leo waumini watasali na kutoa heshima za mwisho kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa saba mchana.

Amesema baada ya hapo kutakuwa na misa takatifu na baadaye waumini wataendelea kutoa heshima za mwisho hadi saa 10 jioni. “Misa nyingine itafanyika jioni na mwili utalala kanisani hapo na waumini wanaruhusiwa kukesha kwa sala kanisani hapo,” alisema Askofu Mkuu Ruwa’ichi.

Amesema kesho saa 12 asubuhi mwili utachukuliwa kanisani hapo na kupelekwa katika Kituo cha Hija Pugu na kutakuwa na misa ya mazishi kuanzia saa nne asubuhi na mwili utazikwa kanisani kwenye kaburi aliloliandaa Kardinali Pengo. Askofu Mkuu Ruwa’ichi amesema Kardinali Pengo alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa moyo. Amesema kiongozi huyo aliwekewa kifaa cha kusaidia mapigo ya moyo kuuwezesha ufanye kazi kwa utaratibu unaotakiwa. “

Alikuwa pia na changamoto ya uti wa mgongo. Alifanyiwa matibabu katika nchi mbalimbali zikiwemo Ujerumani na India na baadaye akaenda Marekani katika Hospitali ya Cornell ambako alifanyiwa upasuaji mkubwa uliodumu kwa saa 13,” alisema Ruwa’ichi. Amesema upasuaji huo ulimsaidia Kardinali Pengo kwa kuwa awali alikuwa ameanza kupinda mgongo lakini baada ya matibabu alirejea katika hali ya kutembea wima.

Ruwa’ichi amesema kifo cha Kardinali Pengo ni pigo kwa kanisa na waumini kwa ujumla, hasa kutokana na mchango wake mkubwa katika kuliongoza Jimbo Kuu la Dar es Salaam kwa miaka mingi. Amesema Kardinali Pengo alihamishiwa Dar es Salaam mwaka 1990 akiwa Askofu Mkuu Mwandamizi na mwaka 1992 alichukua rasmi mamlaka ya kuliongoza jimbo hilo hadi alipostaafu mwaka 2019.

Askofu wa Jimbo Katoliki la Same, Rogath Kimaryo amesema mambo mengi ya kiaskofu anayoyafanya katika jimbo hilo amejifunza kwa Kardinali Pengo hivyo anajiona amempoteza baba. SOMA: CCM: Pengo atakumbukwa kwa faraja, tumaini

Askofu Kimaryo amesema Kardinali Pengo alikuwa zaidi ya nusu ya maaskofu waliopata Daraja hilo katika miaka ya 1990 hadi 2000 waliwekwa wakfu na kiongozi huyo na akadai alikuwa na ushawishi hadi kwenye siasa kwa kuwa neno lake lilikuwa na nguvu kwa kuwa alikuwa na hekima. “Hata viongozi wengi wa serikali walikuwa wanaenda kwake, wanaenda kwake wanaomba ushauri kwake, alikuwa ni mshauri wa watu wengi. Na ukiona utulivu wa nchi ni pamoja na yeye,” alisema Askofu Kimaryo.

Amesema Kardinali Pengo alikuwa msingi na nguzo ya imani Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla na alikuwa akiwaeleza asingependa Mungu amchukue kabla parokia za Dar es Salaam hazijafika 100. “Amerahisisha zikawa parokia nyingi, nyingi sana, watu wa Dar es Salaam wana mwitikio wa imani, mimi ambaye nilifanya kazi kwenye jimbo hilo la Dar es Salaam kwa kweli naona ameacha alama kubwa mno, alama ya imani, alama ya Wakatoliki kujiamini,” alisema.

Ameongeza : “Alikuwa anaongea habari za kifo aache parokia 100 lakini nadhani sasa hivi zipo zaidi ya 170, kwa hivyo ni ndoto alikuwa nayo lakini ni ndoto ambayo imefanya watu wahamasike”.

Askofu wa Jimbo Katoliki la Mtwara, Titus Mdoe amesema  Kardinali Pengo ana misimamo ya maadili kwenye imani na uadilifu. “Ninapozungumzia msimamo ni kwamba, jambo la imani unalolisadiki, jambo la uadilifu unalotaka kuliishi basi ulisadiki, uwe nalo ndani ya moyo wako na ulisimamie na ulifanyie kazi na ujitoe kwa ajili ya hilo alipenda kuwa mkweli katika maisha, haya mambo ya kubabaisha babaisha hakuyapenda kwa kweli,” alisema Askofu Mdoe.

Amesema Kardinali Pengo hakuwahi kuogopa changamoto na hakuwa mtu wa kubabaisha. “Yeye alichukulia kuwa hayo ndio maisha na kwa kweli ni jambo muhimu, simamia jambo ambalo unaliamini, simamia jambo ambalo kutoka kwenye moyo wako kuwa ni jambo ambalo ndio ukweli,” alisema Askofu Mdoe.

Amesema Kardinali Pengo alikuwa ni mtu wa diplomasia, alipenda maelewano na watu lakini kwa misimamo na hakumuogopa mtu. “Si kwamba wewe tunaelewana basi nikuogope kwa sababu labda ya cheo au kwa sababu ya nini, alitaka kusimamia ukweli juu ya jambo fulani, iwe imani yetu, iwe uadilifu wa tunavyotakiwa kuishi, alipenda kuwa wazi na kutekeleza kwa mifano,” alisema.

Ameongeza : “Alikuwa ni mtu wa kupenda umoja, alipenda sana kuona watu wanashikamana kuanzia huko tulivyokuwa shuleni, kwa sababu umoja unaleta upendo, unaleta mshikamano alipenda watu washikamane, watu wapendane lakini ni mtu ambaye alipenda haki za watu, alichukia kuona mtu hatendewi kile anachostahili”.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *