
Raia wa Ghana wapatao 55, wameuawa wakipigana nchini Ukraine, huku wengine wakikamatwa na kufungwa kama wafungwa wa kivita.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Waziri wa Mambo ya nje Samuel Okudzeto Ablakwa, amethibitisha hili, wakati wa ziara yake jijini Kiev.
Ameongeza kuwa, raia wa Ghana wapatao 272 wanaaminiwa walishawishiwa kwenda kupigana nchini Ukraine tangu mwaka 2022.
Waziri huyo wa mambo ya nje amesema, ripoti hizi zinavunja moyo na kusikitisha, na Ghana haiwezi kunyamaza au kufumbia macho raia wa nchi yake wakijipata katika vita hivyo, ambavyo vinaendelea kwa mwaka wa nne sasa.
Hii ndio idadi kubwa ya vifo kuripotiwa rasmi kutoka nchi moja ya Afrika, ambao raia wake wameuawa katika vita kati ya Ukraine na Urusi.
Haijafahamika vema, ni nchi gani raia hao wa Ghana, walikuwa wanapigania lakini, Wizara ya Mambo ya nje ya Ukraine siku ya Jumatano ilisema, waafrika zaidi ya 1,700 kutoka nchi 36 za Afrika, wamesajiliwa kuipigania Urusi katika vita hivyo.
Mbali na Ghana, raia wa Kenya, Uganda, Cameroon na Afrika Kusini ni miongoni mwa nchi ambazo vijana wameripotiwa kushiriki kwenye vita hivyo.