Dar es Salaam. Bunge la Tanzania limetia saini makubaliano ya kuwa mwenyeji wa mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), unaotarajiwa kufanyika Oktoba, 2026 jijini Arusha.
Utiaji saini huo pia umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Bunge na Serikali wakiwamo Rais wa IPU ambaye pia ni Spika mstaafu Dk Tulia Ackson, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na wwabunge wa majimbo ya Mkoa wa Dar es Salaam.
Spika wa Bunge la Tanzania, Mussa Zungu na Katibu Mkuu wa IPU, Martin Chungong wakisaini makubaliano ya Bunge la Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano mkuu wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), utakaofanyika jijini Arusha kuanzia Oktoba mosi hadi 9, 2026.
Katika hafla ya kusaini makubaliano hayo leo, Ijumaa 27, 2026 iliyofanyika katika ofisi ndogo za Bunge zilizopo Mtaa wa Shaaban Robert, jijini Dar es Salaam, Spika wa Bunge la Tanzania Mussa Zungu amemhakikishia Katibu wa IPU, Martin Chungong kuwa maandalizi ya mkutano huo yamefikia hatua nzuri.
“Tanzania ipo tayari kwa asilimia 100 kuwa mwenyeji wa mkutano huo, wajumbe watafurahia hali nzuri ya hewa pamoja na amani na utulivu wa nchi yetu unaosimamiwa na uongozi bora wa Rais Samia,” amesema.
Katibu Mkuu wa IPU, Martin Chungong (kulia) akizungumza katika hafla ya kusaini makubaliano Bunge la Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano mkuu wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), utakaofanyika jijini Arusha kuanzia Oktoba mosi hadi 9, 2026.
Zungu amesema ni heshima kwa Taifa kupewa hadhi ya kuwa mwenyeji wa mkutano wa IPU, akiwataka Watanzania kujiandaa kwa fursa za kiuchumi zitakazotokana na mkutano huo utakaohudhuriwa na wajumbe zaidi ya 2000 kutoka duniani kote.
“Mkutano huo ni fursa adimu ya kiuchumi kwa wakazi wa Arusha na Watanzania wote, unatarajiwa kuhudhuriwa na watu zaidi ya 2000 kutola maeneo mbalimbali wakiwemo wabunge,” amesema.
Akitaja baadhi ya fursa za kiuchumi, Spika Zungu amesema wageni hao watahitaji malazi, chakula na huduma mbalimbali jijini Arusha na maeneo mbalimbali ya nchi watakayotembelea.
Katibu Mkuu wa IPU, Martin Chungong, ameeleza kuridhishwa na mazingira ya Tanzania, akisema ameona mandhari nzuri ya nchi ambayo washiriki wa mkutano huo wataifurahia.
Amesema kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huo wa kidunia inakwenda kuongoza diplomasia ya dunia kwa muda wa wiki nzima.
“Kwa kusaini makubaliano haya niwahakikishie kuwa kwa wiki nzima ya Oktoba 1 hadi 9 mabunge yote duniani yatakuwa Arusha, Mnakwenda kuongoza diplomasia ya kibunge ya dunia kwa wiki hiyo yote,” amesema.
Akiwakaribisha wajumbe hao, Katibu wa Bunge la Tanzania, Baraka Leonard, amesema katika kuonesha utayari wa Tanzania katika uendeshaji wa mkutano huo, tuliunda kamati maalumu ambayo chini ya Katibu wa Bunge, imekuwa ikisimamia maandalizi yote ya mkutano huo na mpaka sasa imeshafanya kazi nzuri kubwa.