Dar es Salaam.Wakati nchi mbalimbali duniani zikizidisha mjadala na hatua za kudhibiti matumizi ya simu za mkononi na mitandao ya kijamii kwa watoto na vijana, ripoti mpya ya kimataifa imeiweka Tanzania katika nafasi ya tano duniani kwa kuwa na vijana wenye uimara mzuri wa afya ya akili.

Ripoti ya Dunia ya Afya ya Akili 2025 iliyotolewa na Taasisi ya Utafiti ya Sapien Labs jijini Washington DC, inaonesha kuwa licha ya ongezeko la changamoto za afya ya akili miongoni mwa vijana duniani, nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara zinafanya vizuri zaidi kuliko mataifa mengi yenye kipato cha juu.

Tanzania imeshika nafasi ya tano, nyuma ya Ghana, Nigeria, Kenya na Zimbabwe.

Utafiti huo ulihusisha zaidi ya watu milioni moja katika nchi 84 na kubaini kuwa, asilimia 41 ya vijana wa umri wa miaka 18 hadi 34 duniani wanakabiliwa na changamoto za afya ya akili, hali inayohusishwa kwa kiasi kikubwa na matumizi makubwa ya teknolojia za kidijitali kuanzia utotoni.

Katika kukabiliana na hali hiyo, baadhi ya nchi za Ulaya na Amerika zimepitisha au kupendekeza sheria za kupiga marufuku matumizi ya mitandao ya kijamii kwa watoto chini ya miaka 16, huku zingine zikiweka muda maalumu wa matumizi ya simu kwa makundi ya umri tofauti.

Ripoti hiyo inapendekeza hatua kama hizo, ikisisitiza umuhimu wa kuweka umri maalumu wa kuanza kutumia mitandao ya kijamii na kupiga marufuku simu shuleni wakati wa masomo.

Kwa mujibu wa ripoti, mafanikio ya Tanzania yanahusishwa na uimara wa kiroho, mfumo wa malezi ya kifamilia na kuchelewa kuanza matumizi ya simu kwa watoto.

Hata hivyo, wataalamu wanaonya kuwa bila sera madhubuti za kulinda kizazi kijacho dhidi ya matumizi holela ya teknolojia, mafanikio hayo yanaweza kupungua kadri upatikanaji wa intaneti unavyozidi kuongezeka nchini.

Akizungumza leo Ijumaa Februari, 27, 2026, Mtaalamu wa Afya ya Binadamu, Dk Ernest Winchislaus amesema ripoti hiyo inatoa ishara kwamba afya ya akili ya vijana inazidi kuwa changamoto kuu ya afya ya umma na uchumi kwa wakati huu.

“Ingawa ni jambo la kushtua kuona baadhi ya nchi za Afrika zikishika nafasi za juu, tunapaswa kuchambua matokeo haya kwa makini kutokana na changamoto za kidijitali na tofauti wa kitamaduni, kwa nchi zetu,” amesema Dk Winchislaus.

Pia, amesema kinachotia wasiwasi zaidi ni mwenendo wa kushuka kwa afya ya akili duniani kote, huku vijana wakiwa katika changamoto kubwa zaidi kuliko wazee.

“Hali hii inahitaji hatua za dharura kutoka sekta mbalimbali ili kuzuia athari za kuingia mapema kwenye teknolojia ya kidijitali, ulaji wa vyakula visivyo na afya, kudorora kwa muundo wa familia na changamoto zingine za kijamii,” amesema.

Mtaalamu huyo amesema ripoti hiyo inapaswa kuwa mwongozo kwa watunga sera kushughulikia mizizi ya changamoto hizi, badala ya kutibu dalili tu.

“Kupunguza matumizi mapema ya simu, kukuza lishe bora, kuimarisha familia na kusaidia ukuaji wa kiroho ni hatua muhimu zinazoweza kulinda ustawi wa kizazi kijacho na kudumisha ukuaji wa kijamii na kiuchumi duniani,” amesema.

Mtaalamu wa Saikolojia, Ramadhani Masenga amesema ripoti hiyo inaonesha kuwa utajiri si kigezo cha moja kwa moja cha afya bora ya akili.

Amesema vijana katika nchi zenye kipato kikubwa kama Uingereza, New Zealand na Japan wanapata alama za afya ya akili zilizo chini ikilinganishwa na vijana wa Sub-Sahara Afrika.

Masenga amesema takwimu za kimataifa zinaonesha kwamba afya ya akili ya vijana katika mataifa tajiri inaashiria kushuka kwa kiwango cha kawaida.

Ameeleza kuwa, mambo muhimu yanayoathiri afya ya akili ya vijana ni mahusiano ya kifamilia, dini, matumizi mapema ya simu za mkononi na ulaji wa vyakula vilivyoandaliwa viwandani.

“Ripoti ya Global Mind Health in 2025 inatupa taswira wazi kwamba afya ya akili ya vijana imekuwa changamoto ya kimataifa na haiwezi kupuuzwa,” amesema  Masenga.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *