
Arusha. Serikali za Tanzania na Zambia zimeahidi kuimarisha uhusiano na ushirikiano katika masuala ya ulinzi na usalama ikiwamo kudhibiti changamoto za kiusalama zinazovuka mipaka hususani ugaidi na uhalifu wa kupangwa ili kukabiliana navyo.
Zimesema usalama huo utasaidia kuweka vizuri mambo yao ya kijamii, kisiasa na kiuchumi na masula mengine mtambuka ikiwamo biashara ili wafanyabiashara wa pande hizo waweze kufanya biashara bila usumbufu.
Hayo yamesemwa leo Ijumaa Februari 27, 2026 na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Rhimo Nyansaho alipozungumza katika kikao cha nne cha Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Tanzanzia na Zambia kuhusu Ulinzi na Usalama.
Amesema vitisho vinavyotokana na ugaidi na uhalifu wa kupangwa unaovuka mipaka vinaendelea kubadilika, hali inayohitaji umakini endelevu, mikakati bunifu na ushirikiano wa karibu kati ya nchi hizo.
“Vitisho vya ugaidi na uhalifu wa kupangwa unaovuka mipaka vinaendelea kubadilika na kunahitajika mikakati mipya na ushirikiano wa karibu zaidi ili kukabiliana navyo,” amesema.
“Katika usalama unatusaidia kuweka vizuri mambo yetu ya kijamii, kisiasa na kiuchumi ndiyo maana tunakutana kila mwezi wa pili kuangalia mambo mtambuka ambayo yanahusu pande zote mbili, leo ni Watanzania na Wazambia kutokusumbuka wakiwa wanafanya biashara katika nchi hizo mbili na nchi zile zinazopita korido ya Zambia,” amesema.
“Kwa jumla tumekutana na kuangalia masuala mtambuka ambayo yanahusu ugaidi, uhamiaji haramu na mambo ya kiintelijensia ambayo yanasababisha kutoimarika kwa usalama katika mipaka yetu.
“Na mambo yanayosababisha biashara kati yetu zisiende kama inavyotakiwa na tumekubaliana mambo ya msingi ambayo tutayashughulikia kwa haraka ili kuimarisha ushirikiano ulioanzishwa,” amesema.
Amesema kuwa juhudi za pamoja za mataifa hayo mawili zimezaa mafanikio makubwa, ikiwa ni pamoja na operesheni zilizofanikiwa, kuboreshwa kwa ushirikishaji wa taarifa za kiintelijensia na mipango ya kujengeana uwezo chini ya mfumo wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Mwenyekiti Mwenza wa tume hiyo, ambaye ni Kaimu Waziri wa Ulinzi na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Zambia, Jacob Mwiimbu amesema mkutano huo umefanyika kwa wakati muafaka huku nchi hizo mbili zikiendelea kupambana na uhalifu wa kimataifa.
Amesema uhalifu huo, ikiwamo usafirishaji haramu wa binadamu na dawa za kulevya, magendo, uhamiaji haramu na uchimbaji haramu wa madini, unaweza kudhoofisha maendeleo ya kiuchumi.
Ameongeza kuwa hakuna nchi inayoweza kukabiliana na changamoto hizo za kuvuka mipaka, pekee ndiyo maana wao wanatumia jukwaa hilo kujadiliana na kubadilishana uzoefu.
Amesema dhamira ya Serikali ya Zambia ni kuendeleza ushirikiano na kufanikisha malengo ya tume hiyo na kuwa usalama unasaidia katika kuvutia wawekezaji wa ndani na nje.
“Tunashukuru uongozi, unatoa fursa ya kipekee ya kushughulikia masuala yenye masilahi ya pamoja ndani ya sekta za ulinzi na usalama za nchi zetu mbili,” amesema.