
Muda wa kusoma: Dakika 6
Onyo: Simulizi hii ina maelezo ambayo baadhi ya wasomaji wanaweza kuziona kuwa za kukera.
Novemba iliyopita, mvulana Mpalestina mwenye umri wa miaka 14 anayeitwa Jad Jadallah alipigwa risasi karibu na wanajeshi wa Israeli katika kambi ya wakimbizi katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.
Jad alipokuwa ameanguka kwenye uchochoro, wanajeshi walimzungushia uzio na kuzuia magari mawili ya wagonjwa ya Wapalestina kumfikia.
Kulingana na video na walio shuhudia, jumla ya wanajeshi 14 walisimama karibu na Jad kwa muda usiopungua dakika 45 huku akivuja damu kutokana na jeraha moja au zaidi la risasi.
Wanajeshi wote wa Israeli hupokea mafunzo ya matibabu kwa waliojeruhiwa, na kitengo chochote cha mapigano cha Israeli kinapaswa kuwa na daktari maalum aliyepata mafunzo, lakini hakuna hata mmoja wa wanajeshi aliyeonekana kumpa Jad msaada wa kimatibabu kuokoa maisha yake. Wakati fulani walionekana kupuuza hatua ya mara kwa mara kutoka kwa Jad ya kutaka wamsikilize.
Jeshi la Ulinzi la Israeli (IDF) liliambia BBC kwamba wanajeshi wametoa “matibabu ya awali”, lakini msemaji alikataa kutoa maelezo yoyote kuhusu aina au muda ambao matibabu yalitolewa.
Jeshi la IDF pia limemshutumu Jad kwa kurusha jiwe, ambalo, chini ya sheria zao za ushiriki, linaweza kuwaruhusu wanajeshi kutumia nguvu kiasi cha hata kuua.
Lakini picha za tukio hilo zinaonyesha wanajeshi wa IDF wakiangusha kitu karibu na Jad baada ya kupigwa risasi, kisha wakapiga picha – kitendo ambacho familia ya Jad na kundi linaloongoza la haki za binadamu wanasema kinaonekana kuwa jaribio la kumsingizia.
Hatimaye wanajeshi walimpakia Jad nyuma ya gari la kijeshi la Israeli, lakini wakati fulani, kabla au baada ya hapo, alifariki dunia. Bado haijulikani ni wapi mwili wake ulipo au ni mara ngapi alipigwa risasi, kwa sababu jeshi la Israeli limekataa kurudisha mwili wake kwa familia na kukataa kujibu maswali yoyote kuhusu majeraha aliyopata.
Alipigwa risasi kwa karibu

Jad alizaliwa na kukulia katika eneo la al-Far’a, kambi ya wakimbizi katika Ukingo wa Magharibi ambayo ni makazi ya Wapalestina wapatao 10,000.
Pamoja na kambi zingine zinazofanana katika maeneo yanayokaliwa, inakabiliwa na mashambulizi ya mara kwa mara ya kijeshi ya Israeli, ambayo Israeli inasema ni muhimu ili kukabiliana na makundi yenye silaha katika eneo hilo.
Hakika, kifo cha Jad hakikuwa cha kawaida. Kulingana na Umoja wa Mataifa, watoto 55 waliuawa na wanajeshi wa Israeli katika Ukingo wa Magharibi mwaka jana na 227 wameuawa tangu shambulio la Hamas la tarehe 7 Oktoba 2023 dhidi ya Israeli.
Lakini mambo mawili yanajitokeza kuhusu kesi hii. La kwanza ni kwamba Jad alikaa bila kupata matibabu kwa muda mrefu, akiwa na wanajeshi wengi waliomzunguka hadi wakati anafariki. La pili ni kuibuka kwa video nyingi za tukio hilo, ambazo BBC imethibitisha.
Wakati halisi wa ufyatuaji risasi ulichukuliwa vizuri na kamera ya CCTV kambini. Picha zinaonyesha wavulana watatu wamesimama kwenye kona ya uchochoro. Kwanza wanaangalia upande wa kulia ambapo, kulingana na walioshuhudia, magari ya kijeshi ya Israeli yalikuwa yameelekea nje ya kambi muda mfupi uliopita.
Mmoja wa marafiki wawili waliokuwa na Jad wakati huo aliiambia BBC kwamba wavulana hao walikuwa wametoka nje baada ya ujumbe uliotumwa kwenye kundi la waliopo kambini, kusema kwamba vikosi vya Israeli vinaondoka, na wavulana walikuwa wakichungulia pembeni ili kutazama wanavyoondoka.
Jad na marafiki zake hawakujua, kundi la wanajeshi wanne wa Israeli lilikuwa limewasubiri nyuma na walikuwa wamesimama mita chache tu kutoka hapo, upande wao wa kushoto, wakiwa wamejificha nyuma ya ukuta. Marafiki wa Jad waliwaona wanajeshi hao kwanza na wakakimbia kwenye kichochoro. Jad ama hakuwaona au aliwaona kwa kuchelewa sana.
Picha za CCTV zinaonyesha mwanajeshi kiongozi akiingia kwenye fremu iliyo chini ya mita tatu kutoka kwa Jad, kisha anaonekana kuinua bunduki yake na kufyatua risasi. Jad anaonekana akiwa anasonga songa kuashiria kuwa huu ndio wakati anapigwa risasi. Katika kambi, mashimo ya risasi yanaweza kuonekana yakichomoza ukutani sehemu hii alipokuwa Jad.
Jad, ambaye huenda tayari amejeruhiwa, kisha anakimbia kwenye uchochoro na mwanajeshi wa Israeli anaonekana kugeuka, akimfuata Jad kwa bunduki yake. Picha za CCTV zinaonyesha vumbi likitibuka kwenye uchochoro uliokuwa mbele, ikiashiria kwamba mwanajeshi wa IDF aliendelea kumpiga risasi Jad kutoka nyuma alipokuwa akikimbia.

Katika picha hiyo, unamwona Jad akianguka baada ya mita chache tu, na kutoka kwenye fremu ambapo anapoanguka. Muda mfupi baadaye, picha ya mtu aliyesimama, iliyorekodiwa kwa siri na mkazi wa kambini, inaanza kutoka upande mwingine hadi kwenye CCTV. Picha hii inarekodi baadhi ya nyakati za mwisho za maisha ya Jad.
Inaonyesha kijana huyo akionekana kufanya majaribio ya mara kwa mara ili wanajeshi wamshughulikie, kwa kupunga mikono na kuwarushia kofia yake. Hata hivyo, wanajeshi wanaonekana kupuuza juhudi zake na kuirudisha kofia nyuma.
Alipoarifiwa kuhusu tukio la mwanawe kufyatuliwa risasi, mama yake Jad alijaribu kumfikia kwa miguu lakini alizuiwa na wanajeshi wa Israeli, yeye na mashuhuda wengine walisema. Mkazi mwingine alipiga simu ya dharura na gari la wagonjwa likatumwa mara moja, na kufika eneo la tukio dakika nane baadaye, kulingana na kumbukumbu za simu zilizotolewa kwa BBC na shirika la Palestinian Red Crescent.
Mhudumu mkuu wa afya, Hassan Fouqha, alisema timu yake ilisimamishwa na wanajeshi wa Israeli wakiwa wamemnyooshea bunduki na kuzuiwa kumfikia Jad, ambaye alikuwa umbali wa yadi mia moja hivi, mbele yao.

Fouqha na wafanyakazi wake wa ambulensi walilazimika kuendelea kumtazama Jad akiwa amelala akivuja damu kutokana na majeraha aliyoyapata. Mhudumu wa afya alisema walimtazama kwa takriban dakika 35, bila uwezo wa kufanya chochote. Fouqha aliita ambulensi ya pili kutoka upande tofauti, lakini pia ilisimamishwa na wanajeshi.
“Tulijaribu kusonga mbele mara kadhaa, kuwapa ishara waturuhusu tumfikie mtoto, lakini tulizuiwa kabisa,” Fouqha alisema. “Tungeweza kumfikia na kutoa msaada wa kimatibabu lakini tulizuiwa. Kusudi la hili, hatujui, lakini hili ndilo lililotokea.”
Jeshi la IDF liliiambia BBC kwamba limetoa “matibabu ya awali” kwa Jad baada ya kuthibitisha kwamba hakuwa na kilipuzi kilichofichwa mwilini. Picha za tukio hilo, pamoja na picha tofauti za CCTV za Jad akiondoka nyumbani kabla, zinaonyesha kwamba alikuwa amevaa fulana na jeans pekee.
Alipoulizwa kuelezea majeraha aliyopata Jad na matibabu aliyopewa, IDF ilikataa kujibu.
Anatuhumiwa kurusha mawe
Jeshi la IDF limesema kwamba Jad aliwarushia mawe na kwamba alikuwa “gaidi” ambaye “alijaribu kushambulia jeshi”.
Lakini familia ya Jad imewashutumu wanajeshi hao kwa kujaribu kumsingizia mwanawao, baada ya picha kusambaa zikimwonyesha mmoja wa wanajeshi akiingia eneo la tukio kutoka kwenye ufyatuaji wa risasi, akiangusha kitu kizito karibu na Jad, kisha akipiga picha kitu kilichokuwa karibu naye.
“Waliangusha jiwe karibu naye ili waweze kumsingizia, na kufanya ionekane kama aliwarushia mawe,” mama yake Jad, Safa, alisema. “Unaweza kuona hilo kwenye video,” alisema. “Yeyote atakayetazama video hiyo ataona.”
Makundi ya haki za binadamu yanasema kwamba wanajeshi wa Israeli katika Ukingo wa Magharibi wanafanya operesheni zao kwa sera ya “kufyatua risasi” na mara nyingi huwapiga risasi watu ambao sio tishio kwa maisha yao, wakiwemo watoto wanaowarusha mawe upande wao.
Shai Parnes, kutoka kundi la haki za binadamu la Israeli B’Tselem, aliambia BBC kwamba picha za Jad zilionekana kumwonyesha mwanajeshi akiweka jiwe karibu naye ili kuhalalisha ufyatuaji risasi.
“Ni vigumu kubaini kwa uhakika tunachokiona – kama ni jiwe na ikiwa wanajaribu kulitumia kumsingizia,” Parnes alisema. “Lakini nadhani yeyote anayetazama bila upendeleo labda atafikia hitimisho hilo.”
Kitendo kama hicho kingekuwa “kibaya sana”, Parnes aliongeza. “Lakini tumegundua visa vingine ambapo vikosi vya Israeli, kwa njia moja au nyingine, vilijaribu baada ya kitendo kama hicho kumtuhumu Mpalestina. Haitakuwa mara ya kwanza kuona hilo kwenye kamera.”
Alipoulizwa haswa kuhusu madai kwamba mwanajeshi huyo alikuwa ameweka jiwe karibu na Jad, IDF ilipuuza swali hilo.

Mazingira mengi halisi ya kifo cha Jad, ikiwa ni pamoja na mara ngapi alipigwa risasi na lini na wapi alifariki, bado hayajafahamika, kwa sababu IDF imekataa kurudisha mwili na kujibu maswali ya kina kuhusu tukio hilo.
Si jambo la kawaida kwa Israeli kukataa kurudisha miili ya watu waliouawa na IDF – mamlaka ya Israeli inaripotiwa kwa sasa kuizuia miili ya Wapalestina 776 au raia wengine wanaoshutumiwa au kushukiwa kufanya mashambulizi.
Walipoulizwa na BBC, IDF walikataa kusema ni kwa nini walikuwa wakiuzuia mwili wa Jad. Mama yake Jad, Safa, alisema kikosi hicho kilikuwa kinajaribu kuficha kitu, au kinafanya tu aina fulani ya ukatili wa makusudi.
“Labda ni kutaka kutukera, kutuchosha, na kujaribu uvumilivu wetu,” alisema. “Lakini tuna subira, na tuna matumaini, na tutaendelea kusubiri. Leo, kesho, au baada ya miaka mia moja, tutampata tena. Majaaliwa ya Mungu akipenda, watamrejesha.”