Shirika la Amnesty International limetangaza kwamba tangu mwezi Disemba mwaka jana, serikali ya Israel imezidisha harakati zake katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu huko Palestina, ikiwa ni pamoja na Quds Mashariki (Yerusalemu Mashariki), kupitia mfululizo wa maamuzi ambayo imesema yanalenga kuimarisha unyakuzi wa ardhi hiyo.

Shirika hilo la kimataifa la kutetea haki za binadamu limeeleza kwamba hatua hizo za Israel zinajumuisha kutoa zabuni za ujenzi wa vitongo vipya vya walowezi, kuidhinisha kuanzishwa makazi ya ziada, kupanua yaliyopo, pamoja na hatua zinazohusiana na kusajili ardhi ya Palestina kama “ardhi za serikali” ya Israel.

Amnesty International imesema kuwa Disemba 10 mwaka jana, zabuni ilitolewa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba 3,401 katika eneo la “E1” mashariki mwa Quds (Yerusalemu), kwa lengo la kupanua vitongoji vya walowezi wa Kizayuni vya Ma’ale Adumim na kuviunganisha na Quds Mashariki.

Taarifa ya Amnesty International imesema kwamba kutekeleza mpango huo kutasababisha mgawanyiko wa kijiografia katika Ukingo wa Magharibi na kufurushwa jamii za Wapalestina wanaoishi katika eneo hilo.

Kwa upande wake, afisa wa Amnesty International, Erika Guevara-Rosas, amesema kwamba licha ya maazimio ya Umoja wa Mataifa, maoni ya ushauri ya Mahakama ya Kimataifa na kulaaniwa kimataifa, Israel inaendelea kupanua vitongoji vya walowezi (katika ardhi ya Palestina) waziwazi, ikikaidi sheria za kimataifa na kuimarisha utawala wa kibaguzi unaoharibu maisha ya Wapalestina.

Kwa mujibu wa shirika la Israel la “Peace Now”, vituo vipya 86 vya ya walowezi wa Kizayuni vilianzishwa mwaka 2025 pekee katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina, vingi vikiwa vya ufugaji au kilimo.

Shirika la haki za binadamu la Israel, B’Tselem, pia limeripoti kwamba zaidi ya jamii 21 za Wapalestina zimefurushwa kabisa au kwa sehemu katika mwaka huo huo kutokana na mashambulizi ya walowezi wa Kizayuni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *