
Dar es Salaam. Muziki una siri kubwa sana. Muziki una nguvu kubwa sana. Muziki unaweza kuliwaza, unaweza kuongeza uchungu, unaweza kuhamasisha ushujaa, unaweza ukaleta uwoga, unaweza kuhamasisha uzalendo, pia ukahamasisha uasi. Muziki unatumika kuwaweka waumini karibu na Mungu wao, muziki unatumika kwa wengine kuwasiliana na mizimu yao, na mambo mengine mengi si rahisi kutaja sifa zote za muziki.
Katika maisha yangu ya muziki nimepitia katika matumizi ya aina nyingi za muziki, na mpaka leo ninaendelea kujifunza upana wa matumizi ya muziki.
Miaka kadhaa iliyopita, meli moja ilitua katika bandari ya Dar es Salaam. Ilikuwa ni meli ambayo ilikuwa ni chuo kikuu ambacho kilikuwa kikisafiri nchi mbalimbali duniani. Chuo hicho kiliitwa ‘Floating University’, yaani chuo kikuu kilichokuwa kikielea.
Nilitaarifiwa kuwa waalimu wawili wa chuo hicho wananitafuta. Baada ya kukutana nao, wakaniambia kuwa wao kila wanapotia nanga katika nchi yoyote, hujaribu kutafuta taarifa yoyote kuhusu ‘healing music’, yaani muziki unaotibu maradhi. Waliniulizia kuhusu muziki wa namna hii hapa kwetu.
Hiyo ilikuwa mara yangu ya kwanza kusikia kazi hiyo ya muziki, na nilikuwa nina uhakika kuwa sijawahi kuisikia muziki wa aina hiyo. Lakini nikawaahidi kuwa nitaulizia. Haikuchukua muda mrefu nikaambiwa pale Magomeni kuna mganga wa jadi anatumia muziki kutibu, nilishangaa mno.
Nilipelekwa kwa yule mganga na nikamueleza kuwa kuna watu walikuwa wakitaka kujua kuhusu muziki wa matibabu, akatukaribisha kesho yake. Saa sita mchana tukafika pale kwa mganga, tulipoingia ndani tukamkuta mganga ana wenzie wote wamejifunga kaniki, na kilichoendele ni kuwa mganga alianzisha wimbo, wenzie wakawa wanamjibu huku wakipiga manyanga.
Baada ya muda mfupi mganga alinyamaza na kuwa kama mtu aliyelewa wenzie wakaendelea na wimbo, hapo wale wagonjwa wakaanza kuingia mmoja mmoja na kueleza shida zao, mganga akawa anatoa matibabu huku akiwa katika hali ya kuwa na mzuka, wale wapiga manyanga wakawa wanaendelea kuimba na manyanga wakati wa matibabu.
Nilikuwa nimeshawahi kusikia aina hiyo ya muziki lakini ilikuwa mara ya kwanza kuuona kwa macho yangu. Wale waalimu waliniambia kuwa walipofika baadi ya nchi za Marekani ya Kusini, waliwakuta waganga wakifanya kama vile alivyokuwa akifanya mganga wa pale Magomeni, na waliniachia CD ya muziki wa wale waganga wa Kimarekani. Hakika siku ile nilijifunza matumizi mengine ya muziki.
Mwaka 1981, nilishiriki katika filamu moja iliyoitwa ‘Wimbo wa Muanzi’. Filamu hii ilitengenezwa na kampuni y umma iliyoitwa Tanzania Film Company (TFC) na kampuni ya Kiholanzi iliyoitwa One World Production.
Baada ya kukamilika kwa filamu, mimi na wenzangu tukapewa kazi ya kutengeneza muziki kwa ajili ya filamu hiyo. Katika kazi hiyo nilisaidiana na wanamuziki wenzangu watatu kutoka Iringa, marehemu Willy Maselenge, marehemu Hashim Kasanga na Ally Lashku.
Baadaye tulikuja kushirikiana na kundi la wanamuziki lilikuwa likiongozwa na Tchimanga Assossa, wakati huo akiwa kwenye harakati za kuunda bendi yake aliyokuja kuiita Orchestra Mambo Bado. Kazi kama hiyo nikaja kuifanya tena katika filamu iliyokuja kuitwa Kutakapokucha.
Mwandishi wa hadithi ya filamu hii ni Irene Sanga. Siku moja alinunua nakala ya CD ya nyimbo alizopiga baba yangu, na katika CD hiyo kulikuweko na wimbo wenye jina Kulava Kwicha ambayo ni tafsiri ya Kihehe ya Kutakapokucha. Irene akachukua maudhui ya wimbo ule na kutunga hadithi nzuri ambayo ilitengenezewa filamu. Na katika filamu hii nilichaguliwa kuigiza kama mwenyekiti wa kijiji mkorofi ambaye pia alikuwa anajua kupiga gitaa, nilichangia nyimbo kadhaa katika filamu hii.
Filamu nyingine ambayo niliitungia muziki ni filamu ya Gitaa langu, katika filamu hii nilikuwa mzee mmoja mlevi aliyependa kupiga gitaa kilabuni, nilifariki na kumuachia binti yangu urithi wa gitaa ambalo binti yangu hakulitaka kabisa kwani lilileta usumbufu mwingi katika familia wakati wa uhai wangu, mumewe alilipenda na kujifunza na baadae kuwa mwanamuziki maarufu kutokana na kuzipiga nyimbo zangu nilizokuwa naimba klabuni. Mkwe wangu alikuwa Banana Zorro.
Katika filamu ya Petu na Galu ambayo niliigiza kama dereva wa taxi niliyekuwa napenda ‘kuisaidia serikali’, pia nilichangia kwa kutunga muziki wa filamu hiyo, Petu na Galu ilikuwa moja ya filamu kumi zilizoingia kwenye kinyanganyiro cha Best Original Music katika tamasha la filamu la SZIFF 2019NIliapata bahati pia kutengeneza muziki kwa ajili ya filamu kuhusu historia ya reli ya Tazara (Train Stories), na muziki kwenye sehemu ya filamu ya Vuta ni kuvute.
Wiki hii nimekamilisha kutengeneza muziki kwa ajili ya filamu iliyotengenezwa na kampuni ya Kijerumani, filamu inayohusu vita ya Majimaji. Kazi nyingine ya muziki ambayo niliifanya mwaka 2017 ilikuwa ni kutengeneza muziki kwa ajili ya kipindi mchezo wa radio kilichoitwa Kumekucha, na kipindi hicho pia kiliambatana na filamu iliyoitwa Kumekucha Fatuma.
Ilikuwa ni filamu iliyohamasisha akina mama kushikilia uchumi uliotokana na nguvu zao katika kilimo. Muziki wa aina hizi za kazi hizi huwa tofauti na muziki wa dansi kwani unatakiwa kuwa muziki ambao unaleta hisia kwa mtazamaji wa filamu au msikilizaji wa kipindi cha redio.
Kazi hii ya kutunga muziki huu ni tofauti na kutunga muziki wa mapenzi, kwa mfano, ili kupata hisia nzuri kwa kutunga muziki wa vipindi vya redio vya Kumekucha, ililazimika niende Ifakara kwa wiki moja ambapo kwa siku tatu nikawa nashinda sokoni kwa nyakati mbalimbali.
Alfajiri wakati soko linafunguliwa, mchana wakati biashara imepamba moto na jioni wakati wa kufunga. Sauti za pale sokoni zilisaidia sana kutunga aina ya muziki nilioutaka.