DAR ES SALAAM: MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amewataka wakazi wa mkoa huo kuendeleza umoja na upendo miongoni mwao, akisisitiza kuwa mwezi mtukufu wa Ramadhani ni fursa adhimu ya kuimarisha mshikamano wa kijamii na kusaidiana.

Chalamila alitoa kauli hiyo Februari 27, 2026 wakati wa hafla maalum ya Iftar iliyoandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa ajili ya wakazi wa Dar es Salaam. Hafla hiyo ilifanyika jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini na serikali pamoja na wananchi kutoka maeneo tofauti ya mkoa huo.

Alisema serikali ya mkoa itaendelea kushirikiana kwa karibu na viongozi wa dini katika kudumisha amani na utulivu, akieleza kuwa mshikamano wa kijamii ni msingi muhimu wa maendeleo endelevu ya taifa.

Mgeni rasmi katika tukio hilo alikuwa Mufti Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zubeir bin Ally, ambaye aliwaongoza waumini katika dua maalum ya kuiombea nchi amani, mshikamano na maendeleo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mufti Mkuu aliishukuru Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa kuandaa Iftar hiyo, akieleza kuwa matukio ya aina hiyo huimarisha uhusiano kati ya Serikali na jamii. Pia aliwataka Watanzania kuendelea kuiombea nchi na kuzingatia maadili mema katika kipindi hiki cha Ramadhani.

Hafla hiyo ilihitimishwa kwa futari ya pamoja iliyoambatana na mawaidha mafupi ya kidini, huku washiriki wakionesha furaha na mshikamano mkubwa, jambo lililoashiria dhamira ya pamoja ya kudumisha amani na umoja katika jamii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *