Dar es Salaam. Katika ulimwengu huu wa teknolojia, yaliyokuwa yanaonekana hayawezekani sasa yanawezekana. Fikiria mpendwa wako aliyefariki dunia, ambaye zamani uliishia tu kuona picha zake kwenye albamu. Sasa una uwezo wa kuona video yake tena akiwa pembeni ya kaburi lake.
Hakika jambo hili sio la kushangaza tena, kwani kupitia mabadiliko hayo ya teknolojia baadhi ya vijana wameamua kuyageuza fursa, kama alivyofanya mtengeneza maudhui kwa njia ya Akili Mnemba Charles David maarufu kama ‘Story za Leo’,
Picha ya Charles mtengeneza maudhui kwa njia ya Akili Mnemba
Charles ambaye kupitia teknolojia amekuwa akitengeneza video za watu mbalimbali maarufu waliopoteza maisha, kwa sura na mfanano wao huku wakionekana wanatembea karibu ya makaburi yao.
Charles ameliambia Mwananchi ameamua kufanya maudhui ya namna hiyo kwa lengo la kuuonesha umma kuwa AI inaweza kuwa na faida kama itatumika vizuri.
“Hii yote ni kutokana na mapinduzi ya teknolojia, zamani tulikuwa tunatengeneza rekodi kwa kuhifadhi kwenye picha. Lakini sasa hivi tunaweka kidijitali, Akili Mnemba ‘AI’ imekuja kuturahisishia zaidi sisi wabunifu ‘AI creators’
“Nilikuwa natafuta kitu cha kipekee, kuonesha uwezo wangu kwa namna nilivyoisoma na kuimasta AI. Baada ya kupata idea nikasema nataka nifanye mtu asione tu AI inatumika vibaya, nikataka tutoe somo jingine kubwa kwamba ukiitumia vizuri inaleta matokeo mazuri,”alisema.
Alisema hapo ndipo akaona atengeneze kumbukumbu kwa watu ambao wametangulia mbele za haki.
“Watu ambao wameacha alama lakini hata wengine ambao wanashindwa kupata kumbukumbu zao. Kuna watu wanapicha za zamani sana za wapendwa wao, picha ambazo za miaka ya 80 kamera zilikuwa ‘black and white’. Lakini mimi ninaweza kuitengeneza ile picha na kuileta katika uhalisia wa picha za sasa.
“Vyuoni zamani hakukuwa na masomo hayo ya AI, kozi nyingi tunazisoma online na huko haikufunzi moja kwa moja. Lakini unatengeneza vitu kutokana na idea zilizopo kichani mwako, kwa sababu AI inauwezo wa kufanya chochote ambacho wewe unakitaka na kukiweka kwenye uhalisia,”alisema Charles.
Alisema wazo la kutengeneza video na picha za namna hiyo alikuwa nalo muda mrefu lakini teknolojia ilikuwa bado haijaruhusu.
“Kwa sasa kila siku inazidi kuboreshwa na hapa bado kuna lengo nalitaka bado halijafikia. Nimepata mapokezi makubwa sana kwa watu maarufu pia. Leo ni siku ya tatu mpaka nne nimetengeneza kazi zaidi 70.
Picha ya aliyekuwa mchekeshaji marehemu MC Pilipili, iliyotengenezwa na Charles kwa kutumia Akili Mnemba
“Sijalala napata muda mchache wa kulala, kwa hiyo mapokezi ni makubwa nimeona uhitaji ni mkubwa hadi nashindwa kuwafikia wote. Kuna wengine wapendwa wao walifariki miaka ya 80 lakini wanataka iwe kwenye uhalisia ni lazima nikae nitengeneze kitu ambacho watapenda,”alisema.
Aliongezea wengine wana picha kipande za wapendwa wao hivyo hulazimika kurudisha sura iwe katika uhalisia. Aidha akizungumzia namna ya ufanyaji kazi alisema zipo picha anatengeneza bure na nyingine hutoza pesa.
“Kuna baadhi nimelipwa lakini zipo nyingine nafanya bure tu kwa kuthamini mchango ambao watu hao wamefanya,”alisema.
Video ya Kanumba ilivyompa changamoto
Alisimulia kati ya video nyingi za watu maarufu alizotengeneza ya aliyekuwa mwigizaji Steven Kanumba ilimpa changamoto, kutokana na picha nyingi alizokuwa nazo enzi za uhai wake.
“Video ya Kanumba unajua alikuwa na picha nyingi. Nikitengeneza picha ya Kanumba watu wanasema hawamuelewi kwa sababu wanashindwa kuelewa sura yake.
“Kila mtu anapicha yake kichwani. Lakini kwangu mimi naona napata picha kamili shida kwa wale wanaotazama. AI haikupi picha kwa asilimia 100 inakupa kwa asilimia 80,”alisema na kuongeza hulazimika kufanya kazi ili apate picha kamili.
Picha ya aliyekuwa mtangazaji, marehemu Amina Chifupa . Picha hii imetengenezwa kwa Akili Mnemba
Mtengeneza maudhui huyo ambaye kazi zake zimewakosha watu maarufu kama Joseph Kusaga, B Dazen, Kitale, MC Gara B, Malkia Karen na wengineo alisema kutokana na ubunifu kaka wa aliyekuwa mtangazaji marehemu Dida alimtafuta.
“Wanafamilia wa Dida walinitafuta kabisa. Walifurahi sana kaka yake akaomba na yeye awepo. Wengine bado kazi zao naendelea kufanya kwa sababu wapo ambao wanauliza mbona fulani hujatengenezwa.
“Mpaka nafika hapa nilishatengeneza vitu vingi vikubwa. Nina filamu fupi ambazo naweka YouTube.Video ambayo imefanya vizuri sana TikTok ya Sam wa Ukweli imetazamwa mara milioni moja na laki tatu pamoja ya Masogange. Kwa Insta ya Gadna nimeona matokeo yake watu wamenitafuta kupitia ile video,”alisema Charles
Utakumbuka marehemu Gardner G Habash alikuwa mtangazaji maarufu wa kituo cha redio cha Clouds FM, alifariki dunia Aprili 20,2024. Huku kwa upande wa aliyekuwa msanii wa Bongo Fleva, Sam wa Ukweli alifariki dunia usiku wa kuamkia Juni 7, 2018. Naye Agnes Gerald ‘Masogange’ambaye alikuwa video queen alifariki dunia Mei 9, 2021.
Akiendelea kueleza alisema kazi ambazo tayari ametengeneza ni zaidi ya 100.
“Video moja haichukui zaidi ya dk 10-20 nakuwa tayari nimemaliza kwasababu nimeandaa kila kitu naweka tu taarifa za mhusika.”alisema
Kuhusu kukatishwa tamaa
“Kitu ambacho kinanivunja moyo ni ile Watanzania kukubaliana na uhalisia wa sasa ulivyo. Ninapokea komenti mbaya hasa za vitisho kwa wengine ambao wanaimani zao kwamba nakosea haipaswi kuwa hivyo, marehemu anahitaji kupumzika
“Wanasema kumbukumbu ya marehemu haitakiwi kuhifadhiwa. Zile zinavunja moyo nashindwa kuendelea na ubunifu. Kwa ndugu wa marehemu mpaka sasa sijapokea malalamiko yoyote zaidi wengi wanakubaliana,”alisema
Alisema kabla ya kuchapicha video yoyote ya marehemu kwenye mtandao wa kijamii huweka maelezo akifafanua lengo lake siyo kupotosha bali kuenzi na kuthamini makubwa waliyofanya.
“Vijana wenzangu ukipata fursa ya kujifunza AI basi tuchangamkie na tujifunze kwa nguvu zote. Kwasababu haipo tu kwa ajili ya kutengeneza bali katika kila kitu inaweza kukusaidia kuongeza urahisi wa kazi.
“Natumia AI mbili tofauti, Chart GPT hii ya kawaida ambayo kila mtu anatumia na video generetion ni Clean AI. Lakini hakuna AI ya bure ndiyo maana mimi natoza gharama kwenye kutengeneza huku lazima ulipie ili upate kitu kizuri,”alisema.