ALIYEKUWA mkurugenzi wa Fedha wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Cornel Barnabas, ameteuliwa kuwa ofisa mtendaji mkuu wa Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB).

Tangu Juni, mwaka jana, nafasi hiyo ilikuwa ikikaimiwa na Ibrahim Mwayela baada ya rais wa TFF, Wallace Karia kumsimamisha aliyekuwa akihudumu katika nafasi hiyo, Almas Kasongo, kufuatia mgogoro ulioibuka baada ya kushindwa kuchezwa kwa mechi ya watani wa jadi Tanzania, Yanga na Simba, Machi 08, 2025.

Cornel ametangazwa leo wakati Karia akiweka hadharani majina ya wakurugenzi mbalimbali wa idara za shirikisho hilo baada ya kumalizika kwa mkutano Mkuu wa TFF mjini Kahama mkoani Shinyanga.

“Lakini pia tumeweza kuteua na kuthibitisha mtendaji mkuu wa Bodi ya Ligi, atakuwa ni Cornel Barnabas, ambaye alikuwa mkurugenzi wa Fedha wa TFF. Mkurugenzi aliyekuwepo mkataba wake unaishia leo (jana) tarehe 28.

“Hizi teuzi zote ninazotangaza zitakuwa zinaanza kazi kesho, kwa maana ya tarehe moja mwezi wa tatu,” amesema Karia.

Katika uteuzi huo, Salum Madadi atakuwa mkurugenzi wa Miundombinu, Baraka Kizuguto ni mkurugenzi wa Mashindano, Hassan Njama atasimama kama mkurugenzi wa Fedha, Flora Harris ameteuliwa kuwa mkurugenzi wa Udhibiti na Frank Zamboko ni mkurugenzi wa Manunuzi.

Aliyekuwa Mtendaji wa Bodi ya Ligi kabla ya kusimamishwa mwaka jana, Almas Kasongo amerudi baada ya kuteuliwa kuwa mkurugenzi wa timu za Taifa. Habari za ndani kutoka TFF, zimeifichulia Mwananchi Digital kuwa Ibrahim Mwayela aliyekuwa akikaimu nafasi ya Mtendaji Mkuu wa TPLB, anarudi katika nafasi yake ya Mhasibu wa Bodi ya Ligi.

Katika Mkutano huo wa leo, Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Dar es Salaam (DRFA), Lameck Nyambaya amechaguliwa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF katika uchaguzi mdogo wa kujaza nafasi hiyo kwa kanda namba moja ambayo ilikuwa wazi kufuatia kujiuzulu kwa Hosseah Lugano, Novemba 27 mwaka jana. Mkutano huo pia umepitisha bajeti ya Sh56 bilioni ya shirikisho hilo kwa msimu wa 2026/2027.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *