Iran imelishutumu Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kufumbia macho mashambulizi mabaya yaliyofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Lebanon, ambayo yanakiuka makubaliano ya kusitisha mapigano ya 2024.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei, jana Ijumaa alilaani vikali mashambulizi hayo ya anga ya Israel dhidi ya Lebanon, ikiwemo hujuma ya hivi karibuni dhidi ya Bonde la Beqaa.

Ametoa wito kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutekeleza majukumu yake katika kudumisha amani na usalama wa kimataifa, na kuchukua “hatua za haraka” mkabala wa ukiukaji wa mamlaka ya kujitawala, uhuru na umoja wa ardhi ya Lebanon unaofanywa na Israel.

Baghaei ameeleza bayana kwamba, kimya cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kutochukua hatua dhidi ya uhalifu wa Israel ni “janga kubwa”.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema Marekani na Ufaransa, kama wadhamini wa makubaliano ya kusitisha mapigano, zinabeba dhima ya ukiukaji wa mapatano hayo.

Matamshi ya Baghaei yanakuja huku ndege za kivita za Israel zilifanya angalau mashambulizi 13 ya anga kwenye Bonde la Beqaa la Lebanon siku ya Alkhamisi, na kuua mtu mmoja na kuwajeruhi wengine 29.

Jumamosi iliyopita, Wizara ya Afya ya Umma ya Lebanon ilitangaza kuwa, watu 10 wameuawa na 24 kujeruhiwa, wakiwemo watoto watatu, katika mashambulizi ya anga ya Israel mashariki mwa Lebanon. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *