Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imezitaka Pakistan na Afghanistan kuketi kwenye meza ya mazungumzo haraka iwezekanavyo ili kusimamisha mapigano na kupunguza mvutano, huku mapigano ya mpakani kati ya nchi hizo mbili yakizidi kupamba moto.

Katika taarifa iliyotolewa jana Ijumaa, wizara hiyo ilielezea wasiwasi wake mkubwa kuhusu ongezeko la mivutano kati ya nchi hizo mbili jirani na za Kiislamu na athari zake mbaya za kiusalama na kwa binadamu.

“Mgogoro kati ya Pakistan na Afghanistan umesababisha vifo vya watu na hasara za mali kwa nchi hizo mbili jirani na utazidisha ukosefu wa usalama katika kanda hiyo na kusababisha athari mbaya kwa binadamu na usalama wa eneo lote,” imeongeza taarifa hiyo.

Wizara hiyo imesisitiza kwamba Jamhuri ya Kiislamu kwa mara nyingine tena inatoa wito kwa pande zote mbili kuheshimu ardhi na mamlaka ya kujitawala ya kila upande na kujiepusha na hatua yoyote ambayo inaweza kuzidisha mvutano na migogoro.

Iran pia imeelezea utayarifu wake wa kusaidia kupunguza mvutano na kuwezesha mazungumzo kati ya Kabul na Islamabad ili kukomesha kabisa mzozo wa kijeshi na kufikia maelewano.

Pakistan na Afghanistan zimeshuhudia mapigano makali tangu Alhamisi usiku. Pakistan imefanya mashambulizi ya anga katika maeneo kadhaa ya mji mkuu wa Afghanistan, Kabul na pia Kandahar, huku Waziri wa Mambo ya Ndani wa Pakistan, Mohsin Naqvi akiyaelezea mashambulizi hayo kama “jibu mwafaka” kwa “uchokozi wa wazi wa Taliban.” 

Kwa mujibu wa taarifa zilizothibitishwa, hadi sasa wapiganaji wapatao 44 wa Taliban wameuawa katika operesheni hiyo ya mashambulizi.

Pakistan imetangaza kuwa, operesheni hiyo ni jibu kwa hatua zisizo na sababu zilizochukuliwa na Taliban ya Afghanistan katika eneo la mpakani, na kwamba mashambulizi ya anga yangali yanaendelea.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *