Jeshi la Israel jana lilipeleka idadi kubwa ya wanajeshi katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, hasa katika vituo vya ukaguzi vinavyoelekea katika mji wa Quds (Jerusalem), sanjari na kuimarisha vizuizi dhidi ya Wapalestina waliotaka kuingia katika Msikiti wa al-Aqsa kwa ajili ya Swala ya Ijumaa ya pili ya mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Hatua kali za Israel ziliwazuia Wapalestina wengi kuingia katika Msikiti huo, huku waumini wakisema “walirudishwa nyumbani licha ya kufika mapema”, wanajeshi wa Kizayuni wakida wameshindwa kutimiza masharti yaliyowekwa awali.

Watoto walio chini ya umri wa miaka 12, wanaume wenye zaidi ya miaka 55, na wanawake wenye umri wa miaka 50 au zaidi ndio walioruhusiwa tu na Wazayuni kuswali Masjidul Aqsa.

Kadhalika utawala wa Kizayuni wa Israel uliwawekea vizuizi vikali Wapalestina kuingia katika Msikiti wa al-Aqsa katika mji wa Quds unaokaliwa kwa mabavu, kwa ajili ya Swala ya Ijumaa ya kwanza ya mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Haya yanajiri huku jeshi la utawala wa Kizayuni likishadidisha mashambulizi yake katika maeneo mbalimbali ya Ukingo wa Magharibi huko Palestina katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.

Katika uvamizi wao dhidi ya mji wa al-Khalil, vikosi vya utawala vamizi wa Israel, vilishambulia mji wa Surif kaskazini mwa al-Khaliil, mji wa Awa magharibi mwa al-Khalil, na mji wa Deir Samet magharibi mwa Dura kusini mwa mji huo.

Aidha wanajeshi wa utawala huo pandikizi wamevamia mji wa “Qasra” kusini mwa Nablus, na mji wa Al-Obeidiyah, mashariki mwa Beit Laham.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *