Dar es Salaam. Ameumaliza mwendo. Ndivyo inavyoweza kuelezwa hitimisho la safari ya mwisho ya Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo katika maziko yake yaliyokusanya maelfu ya waombolezaji, wakiwemo viongozi wa kitaifa na wa kidini pamoja na wananchi wa kada mbalimbali.
Shughuli hizo zilianza kwa misa takatifu iliyoongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Juda Thaddeus Ruwa’ichi, ambapo salamu mbalimbali zilitolewa.
Katika salamu hizo, Kardinali Pengo ametambuliwa kama kiongozi wa kiroho aliyepita mipaka ya madhehebu na kuwa sauti ya maadili, uadilifu na uzalendo nchini.
Katika ibada hiyo, Watanzania wametakiwa kufuata na kuenzi maadili na uzalendo alivyovihubiri na kuviishi Kardinali Pengo, huku kila mmoja akihimizwa kuitumikia nchi kwa nguvu zake zote.
Aidha, wametakiwa kuacha tofauti za vyama vya siasa, dini na ukabila, kama sehemu ya kuuenzi urithi wake wa kiroho na kitaifa.
Wito huo ulitolewa leo, Februari 28, 2026, na viongozi mbalimbali wa kitaifa na kidini wakati wa ibada na shughuli za kumuaga kiongozi huyo wa kiroho zilizofanyika katika Kituo cha Hija Pugu.
Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika (SECAM) Kardinali Fridolin Ambongo wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo akiongoza maziko ya Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo ambaye amezikwa leo Jumamosi Februari 28, 2026 katika Kituo cha Hija kilichopo Pugu, jijini Dar es Salaam.
Viongozi hao walimtaja Kardinali Pengo kuwa alisimama imara katika kuhubiri na kuishi maadili hadi mwisho wa maisha yake.
Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi, ametoa salamu kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan na ujumbe wake mwenyewe akiwataka Watanzania, wakiwemo wasio wanachama wa vyama vya siasa, kuonyesha mapenzi kwa nchi yao kwa kuitumikia kwa uadilifu na uaminifu.
“Kila mtu ana nafasi katika utumishi wa nchi yetu, tusitegeane. Kazi ya kutumikia nchi si rahisi, ina vitisho na vishawishi, ndiyo maana tunawaomba viongozi wa dini waendelee kutuombea,” amesema.
Nchimbi, amesema kila Mtanzania ana nafasi ya kuitumikia nchi bila kujali tofauti za vyama, akisisitiza kuwa siasa za mivutano na kejeli hazina tija kwa Taifa.
“Hata nilipokuwa Katibu Mkuu wa chama nilikuwa nikisikia mwana CCM ameongea maneno ya hovyo dhidi ya upinzani nilikuwa nakemea mara moja ni ujinga tu, kwa sababu vyama vimeundwa kwa mujibu wa Katiba ya nchi, mtu anavyojiunga na chama kingine, maana yake naye anataka kutumikia nchi yake kwa njia nyingine, lakini utumishi ni utumishi,” amesema.
Akizungumzia uhusiano wake na Kardinali Pengo, Nchimbi amesema alifahamiana naye tangu mwaka 1996 na kuwa karibu naye hadi alipofariki dunia.
Alisimulia kuwa mara ya mwisho kabla ya Kardinali Pengo kusafiri nje ya nchi kwa matibabu, alimjulisha safari yake na akaenda kumuaga uwanja wa ndege.
“Kwenye tarehe 12-13 hivi hungeweza kufikiri ni mtu mwenye maumivu makali. Alisimama akatembea na mimi hatua kama 20, bado alikuwa na dhamira ya kuendelea kuishi,” alisema.
Nchimbi ameeleza kuwa wakati huo Rais alipokuwa katika ziara ya kikazi nchini Ethiopia, alimkabidhi mamlaka ya kuongoza nchi, ndipo alipata fursa kushughulikia usafiri wake.
Amesema hali ya Kardinali Pengo ilipobadilika na yeye alipofahamishwa kuhusu changamoto ya usafiri wa kumrejesha nyumbani, awali alidhani ni suala la kubadili tiketi, lakini baadaye akaelezwa kuwa hali yake ilihitaji kukodi ndege maalumu ya wagonjwa (air ambulance) ili kumuwahisha kwa muda aliotaka.
Jeneza lenye mwili wa Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo ambaye amezikwa leo Jumamosi Februari 28, 2026 katika Kituo cha Hija kilichopo Pugu, jijini Dar es Salaam likishushwa kaburini.
“Washauri wakasema lazima Rais afanye maamuzi. Nikamwandikia ujumbe mrefu. Mwisho Rais akasema, ‘Makamu mbona unazunguka sana, sema shida ni nini?’ Alipofahamu inahitajika air ambulance akasema, ‘Nimeridhia, fanyeni mchakato ufanyike haraka sana,’” amesema Nchimbi.
Alisema uamuzi huo uliwezesha usafiri maalumu wa kumrejesha Kardinali Pengo nchini, akisisitiza kuwa heshima na mshikamano kwa viongozi waliolitumikia Taifa ni wajibu wa kila Mtanzania.
Jaji Warioba
Akitoa salamu zake, Waziri Mkuu Mstaafu Jaji Joseph Warioba amesema msiba huo ni mzito kwa Taifa kwa kuwa marehemu Pengo hakuwa tu kiongozi wa Kanisa Katoliki, bali kiongozi wa Watanzania wote.
“Si rahisi kuzungumza katika msiba huu. Kardinali Pengo hakuwa tu kiongozi wa Katoliki, alikuwa kiongozi wetu sote. Mimi si Mkatoliki, lakini nilimheshimu kama kiongozi wangu wa kiroho,” amesema Warioba.
Amekumbushia hotuba ya Kardinali Pengo wakati wa kuaga mwili wa Rais wa kwanza wa Tanzania, Julius Nyerere, akisema ilikuwa hotuba ya kizalendo iliyowalenga Watanzania wote bila kujali dini zao.
Kwa mujibu wa Warioba, katika kipindi ambacho Taifa limekuwa likikabiliwa na changamoto ya kuporomoka kwa maadili, Kardinali Pengo aliendelea kuwa sauti ya kuwakumbusha Watanzania umuhimu wa maadili, usawa, umoja na uzalendo.
Dada wa Pengo
Kwa upande wake, mdogo wa marehemu, Helena Joseph Pengo, amelishukuru Kanisa Katoliki kwa malezi na malezi ya kiroho aliyoyapata ndugu yake tangu akiwa kijana, akisema tangu utotoni alionyesha ndoto ya kulitumikia Kanisa hadi kufikia kuwa askofu na baadaye kardinali.
Amesema kaka yake alianza kulelewa na kanisa tangu akiwa na umri wa miaka 27 lakini akiwa mtoto aliwaeleza wazazi wake ameota ndoto atakuwa askofu na shahidi, lakini hawakumuamini.
Askofu Ruwa’ichi
Katika mahubiri yake,Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Jude Thaddeus Ruwa’ichi, amewataka waumini na Watanzania wote kuendeleza moyo wa kujituma na kujitoa aliouonyesha Kardinali Pengo.
Amesema marehemu atakumbukwa kwa moyo wake wa kichungaji na kwamba ataendelea kuwa mwombezi wa Watanzania wote bila ubaguzi wa dini, chama au kabila.
Katika hatua nyingine Ruwa’ichi amesema, “Hili nitakalolisema sasa ni gumu, mwaka jana Oktoba lilipotokea lile sokomoko niliongea na Kardinali (Pengo) akaonyesha masikitiko makubwa kwa yale yaliyojiri na tukakubaliana tuliombee Taifa letu.
“Sasa kwa kuwa ametangulia naamini atakuwa mwombezi wetu Watanzania wote, nirudie kwa msisitizo atakuwa mwombezi si tu wa Wakatoliki, bali wa Watanzania wote bila ubaguzi wa dini, chama, kabila au chochote kile kinachoweza kututenganisha,” amesema Ruwa’ichi.
Walichosema waombolezaji
Felix Mrema kutoka Mlandizi, amesema ameguswa na kifo cha Kardinali Pengo kwa kuwa enzi za uhai wake alikuwa kila wakati anahuburi amani na kuonekana kuwa kiunganisho kikubwa kwa Watanzania.
Naye Angel Hendry, mkazi wa Ukonga amesema yaliyozingumzwa na watu mbalimbali kuhusu maisha enzi za uhai wa kardinali huyo, anatamani kila mtu angeweza kuishi hivyo, ili nchi iweze kuwa sehemu salama ya kuishi.
Brian Antipas mkazi wa Tabata Kinyerezi, amesema ukisikiliza historia ya kardinali huyo iliyotolewa na dada yake wakati ana ndoto za kumtumikia Mungu katika maisha yake, ni wazi inatoa funzo kwa wazazi na walezi kuwasikiliza watoto wanapowaambia wanataka kuwa nani.
“Kama wazazi wa Kadinali Pengo wasingemsikiliza mtoto wao na ndoto zake, huenda hayo mazuri aliyolifanyia kanisa na nchi kwa ujumla leo tusingekuja kuyasikia hapa. Wazazi na walezi kuna la kuifunza kupitia historia yake tuliyoisikia ya safari ya kuwa askofu,” amesema Antipas.
Maziko yalivyokuwa
Shughuli za kuaga mwili wa Kadinali Pengo zilianza saa 1:00 asubuhi kwa waumini na wananchi mbalimbali kuuaga mwili uliokuwa umewekwa mbele ya kanisa lililopo ndani ya Kituo cha hija Pugu.
Ilipotimu saa 3:27 shughuli hiyo ilisimamishwa na kuanza kwa misa iliyoongozwa na Askofu Ruwa’ichi.
Baada ya kumalizila kwa misa hiyo ya takribani saa mbili, baada ya waombolezaji na wawakilishi wa taasisi mbalimbali wakapewa nafasi za kutoa salamu zao za mwisho.
Pia viongozi mbalimbali wa dini kutoka ndani na nje ya nchi, walipewa nafasi ya kufanya hivyo kwa nyakati tofauti.
Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba akiweka udongo kwenye kaburi lenye mwili wa Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo ambaye amezikwa leo Jumamosi Februari 28, 2026 katika Kituo cha Hija kilichopo Pugu, jijini Dar es Salaam.
Ilipotimu saa 8:46 mchana safari ya kwenda kuupumzisha mwili wa kiongozi huo kwenye eneo maalumu ndani ya kanisa dogo la Hija Pugu ilianza ambapo baadhi ya mapadri walibeba jeneza lililokuwa na mwili wake huku wachache waliotajwa wakiusindikiza kwa maandamano.
Miongoni mwa wachache waliotajwa ni Dk Nchimbi na Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba.
Pia ndugu wachache akiwemo dada wa Kadinali Pengo na baadhi ya maaskofu na mkuu wa watawa walitajwa kutokana na udogo wa eneo husika.
Mwili wa Kadinali Pengo ulianza kushushwa kaburini saa 9:09 huku watu wengine wakiwa wanashuhudia kupitia runinga kubwa zilizokuwa zimefungwa kwenye viwanja vya kituo hicho.
Mpango, Majaliwa, Warioba waibua shangwe
Katika hatua nyingine ilifika wakati, watu wakapumzisha majonzi na kushangilia msibani.
Hii ni baada ya kutambulishwa kwa viongozi mbalimbali wastaafu wa Serikali huku shangwe ikianzia kwa Makamu wa Rais Mstaafu, Dk Philip Mpango.
Katibu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (Tec) Padri Charles Kitima alikuwa akiwatambulisha viongozi hao, wakiwemo mawaziri wakuu wastaafu, Kassim Majaliwa, Joseph Warioba na Mizengo Pinda.
Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba akisalimiana na viongozi wastaafu akiwamo Makamu wa Rais mstaafu, Dk Philip Mpango, mawaziri wakuu wastaafu, Kassim Majaliwa, Mizengo Pinda na Jaji Joseph Warioba.
Baadhi ya waombolezaji walisema kushangiliwa huko ni ishara kwamba viongozi hao walitekeleza majukumu yao vizuri walivyokuwa madarakani.
“Ukiona umetoka nje ya Serikali, ukifika kwenye halaiki kama hiyo ya msiba ambapo watu wana majonzi unashangiliwa, ujue kuna alama uliyoiacha kwa wananchi. Hili ni funzo tosha kwa waliopo madarakani kutumia nafasi hizo vizuri ili kesho na wao wasemwe vizuri midomoni mwa watu.
Alexandra Kilima amezungumzia kauli ya Dk Nchimbi kuwa hapendi kuona watu wakigombana, akisema ni yenye kuleta matumani na ameshauri isiishie kwenye mdomoni bali Serikali ilitekeleze hilo kwa vitendo.