Dar es Salaam. Mamia ya waombolezaji wamejitokeza katika shughuli ya mazishi ya aliyekuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam,Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.

Kinachoendelea Pugu mazishi ya Kardinali Pengo

Kardinali Pengo alifariki dunia Februari 19, 2026 katika Hospitali ya Moyo ya Jakaya Kikwete alipokuwa akipatiwa matibabu.

Mwili wake unatarajiwa kuzikwa leo Jumamosi Februari 28, 2026 katika Kituo cha Hija kilichopo Pugu Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam.

Ukiacha wananchi wa kawaida, waumini kanisa hilo, pia viongozi mbalimbali wa kiserikali wameshawasili katika kituo hicho akiwamo Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi, ambaye ndio anawakilisha Serikali katika shughuli hiyo.

Wengine waliofika ni Waziri Mkuu Dk Mwigulu Nchemba na mawaziri wastaafu , Mizengo Pinda, Jaji Joseph Warioba na Kassim Majaliwa.

Baadhi ya waombolezaji waliojitokeza katika Kituo cha Hija kilichopo Pugu Wilaya ya Ilala mazishi ya aliyekuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.

Shughuli ya waombolezaji waliofika hapo ya kuaga mwili wa kiongozi huyo ilianza saa 1:00 asubuhi na kukoma saa 9:27 huku baadhi ya viongozi waliofika baada ya hapo walipita kuaga mwili uliohifadhiwa kanisani hapo kabla nya kwenda kukaa.

Baadhi ya watu waliofika hapo walionekana wakipiga picha katika mabango mbalimbali yaliyobandikwa picha za Askofu huyo zikiwemo za utotoni, ujanani, akiwa na familia na hadi uaskofu.

Aidha ulinzi katika maeneo ya kuingia katika kituo hicho ulikuwa umeimarishwa huku wakionekana askari wa Jeshi la Polisi wanaotembea na wengine wakiwa kwenye magari na silaha wameshikilia silaha nzito.

Vilevile nje ya kituo hicho kulionekana kushamiri kwa biashara mbalimbali zikiwemo za vyakula, vinywaji  na picha za askofu huyo zenye kamba ya kuvaa shingoni pamoja na vifaa mbalimbali vinavyotumika kusalia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *