
Dar es Salaam. Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) eo, Jumamosi, Februari 28, 2026 limemtangaza, Cornel Barnabas kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa kudumu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara akichukua nafasi iiyokuwa ikikaimiwa na Ibrahim Mwayela.
Mwayela alikuwa akikaimu nafasi hiyo tangu Juni mwaka jana baada ya Rais wa TFF, Wallace Karia kumsimamisha Amas Kasongo aliyekuwa ndiye Mtendaji Mkuu wa Bodi hiyo baada ya kutokea mgogoro wa mechi ya Watani wa Jadi Tanzania, Yanga na Simba.
Karia ametangaza uteuzi wa Cornel wakati akiweka hadharani majina ya wakurugenzi mbalimbali wa idara za Shirikisho hio baada ya kumalizika kwa Mkutano Mkuu wa TFF, Kahama, Shinyanga.
“Lakini pia tumeweza kuteua na kuthibitisha Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi. Atakuwa ni Cornel Barnabas ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Fedha wa TFF. Mkurugenzi aliyekuwepo, mkataba wake unaishia eo tarehe 23.
“Hizi teuzi zote ninazotangaza hapa zitakuwa zinaanza kazi kesho kwa maana ya tarehe moja mwezi wa tatu,” amesema Karia.
Katika uteuzi huo, Salum Madadi atakuwa Mkurugenzi wa Miundombinu, Baraka Kizuguto atakuwa Mkurugenzi wa Mashindano, Hassan njama atakuwa Mkurugenzi wa Fedha, Flora Harris ameteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Udhibiti na Frank Zamboko atakuwa Mkurugenzi wa Manunuzi.
Aliyekuwa Mtendaji wa Bodi ya Ligi kaba ya kusimamishwa mwaka jana, Almas Kasongo, amerudi kivingine katika shirikisho hilo baada ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi wa timu za Taifa.
Habari za ndani kutoka TFF, zimeifichulia Mwananchi Digital kuwa Ibrahim Mwayela aliyekuwa akikaimu nafasi ya Mtendaji Mkuu wa TPLB, anarudi katika nafasi yake ya Mhasibu wa Bodi ya Ligi.
Katika Mkutano huo wa leo, Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Dar es Salaam (DRFA), Lameck Nyambaya amechaguliwa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF katika uchaguzi mdogo wa kujaza nafasi hiyo kwa kanda namba moja ambayo ilikuwa wazi kufuatia kujiuzulu kwa Hosseah Lugano, Novemba 27 mwaka jana.
Mkutano huo pia umepitisha bajeti ya Sh56 bilioni ya Shirikisho hio kwa mwaka 2026/2027.