Dar es Salaam. Haikumtisha. Tayari bibie alikuwa ameshajiweka pembeni. Na zaidi hakuwa Hidaya yule wa Jeff, bali Hidaya ni yule wa Mr Med. Jeff ni kijana kama Hidaya, Ndiyo, Jeff ni ‘stafu’ kama ilivyo kwa Hidaya, ni ndani ya ofisi ya kampuni ya Mr. Med, katikati ya Jiji la Dar.

Vitisho vya Jeff kwa Hidaya, hapa vikawa kama vikorokoro vile vya wacheza kamari mitaa ya Uhuru na Msimbazi. Tayari hapo Hidaya aliondoka moyoni kwa Jeff, sasa akaondoka mkononi kwa Jeff rasmi. Hasikii la muadhini wala mnadi swala, yeye wa Masaki Jeff wa Kilungule.

Gauni refu lenye michirizi yenye rangi nyekundu na nyeusi kuanzia katika kora, hadi kwenye nyonga zake. Liliufanya uzuri wa Hidaya uongezeka mara elfu moja zaidi ya kawaida. Mrefu ndiyo, ila siyo kama Zaiylissa, rangi ya Lulu, shepu ya Posh Queen ipunguze kidogo hivi.

Bahati mbaya hii ilikuwa ni siku ya mwisho ya Jeff, kuona uumbaji wa Mungu kupitia umbile la Hida. Akageuka, kwa mwendo ule wa staha, akarudishia mlango kisha akatokomea. Aliacha nyumba na harufu tamu ya marashi na ndita katika uso wa Jeff.

Jeff akiwa kasimama kisanamu kama ya askari. Alishuhudia binti mrembo zaidi katika maisha yake, ‘of kozi’ alipenda kumuita Hida. Akiingia ndani ya gari akitokomea zake. Wahenga husema ‘imetoka ikirudi pancha’, ndicho kilichopo kwake sasa.

Wimbo ‘flan’ wa Mondi na Zuchu, kwa mbali ulisikika chumbani kwa Jeff. Ukijirudia, bila shaka ni maalum kwa ajili ya Hida ambaye tayari hakuwa wake tena. Kama kawaida ya wanaume wakipigwa tukio mwanzo hujifanya hawajali, wanakufa na tai shingoni.

Gari alilopanda Hidaya (Hida ‘ini Jeff voisesi’), ndilo lililompasua kichwa Jeff. Akili zilimrejea upya na kujitambua kuona gari nje likiondoka na Hida wake. Ni gari la nani? La Boss! Mr Med hapajui kwa Jeff, hajui uhusiano wake na Hida. Imekuaje, kafikaje, ili…? 

Akabaki na maswali hayo, lakini kubwa lililomuumiza Jeff ni ‘wai’ Hida aende na Mr Med (boss)? Kwenye hili hakupata jibu kamili, na vijana wa Sinza, Goba, Mbezi Mbezini, Tabata na Kinondoni. Jawabu lao huishia katika tungi. Akaenda kutungika. 

Ujue nini? Jeff ni msela na ‘stafu’ mwenzetu katika taasisi flan hivi. Ni wale madogo ‘wanaopushi’ Harrier New Model mjini, Mazda CX5, Crown, Klugger nk. Ni wale waliopanga nyumba upande ile mtaa niliyoitaja hapo juu. Masela ambao mapenzi huanzia bar na huishia bar. 

Safari hii alipata pisi kali kutoka Tanga. Pisi ya mitaa ya Sahare, Chuda, Chumbageni, Usagara, Mikanjuni, Nguvumali, Kwa Njeka, Mabanda ya Papa, Masiwani na hata Raskazone. Mtoto wa Tanga haswa aliyefundwa, muda wote anukia kama jini sufiani.

Hidaya alinyooka kweli na nakshi za kikeni haswa. Alivutia kwa kila kitu, sura, umbo, rangi, utanashati, achana na sauti. Kuna ile ladha ya lafudhi ya Tanga, akiongea upepo wa Kusi ulibadili uelekeo, badala ya Kas ukaenda Magharibi. Aibu.

Kila msela alitamani kupata robo ya dem aliye na testi ya Hidaya. Ni Hidaya kweli achana na yule wa Pepe Kale. Tunaongelea wa Tanga siyo wa Arusha. Mtoto wa kike alijua thamani ya kike kwa usafi na adabu. Asubuhi hadi giza alikuwa tayari kwa lolote.

Ungemuona alfajiri  ungetangaza ndoa. Ukienda kwao asubuhi au mchana na usiku, pia ungemkuta msafi, hana kisirani wala mapepe. Mtoto mwenye sifa hizi alituama mikononi mwa gendaheka lenye tani saba za wendwazimu Jeff. Hili ndo kosa la Hidaya.

Alijikuta mikononi mwa kijana wa pombe, soka, kamari wanawake na mitoko ya usiku kwa kiwango cha juu. Alipenda soka sawa na alivyopenda pombe, totoz, kamari na mitoko. Kimsingi ni kijana wa ovyo. Hafai kwa kulumangila wala chetezo. 

Hidaya anataka ndoa alikite, Jeff anataka kudonoa apite. Hidaya kalelewa na maustaadhi wenye heshima Usagara nzima. Jeff yeye kalelewa na mtaa, kazaliwa na kulelewa na ‘singo’ maza’. Na kila kitu alichojifunza baada ya balehe, alikijulia mitaani.

Kilimchomsaidia ni elimu ndogo ya kuunga akapata ‘satifiketi’. Na ‘koneksheni’ za ‘Bi mkubwa kwa wachati na madanga yake, Jeff akapata kitengo kitamu kazini. Pesa ndefu, posho, wizi wa hapa na pale. Akawa mmoja wa vijana wasumbufu kila wikiendi. 

Hidaya pia hana elimu ya kutisha, ana ‘digrii’ yake ya Mlimani pale. Pasi kama za Ozil, Chama ama Pacome. Zikamuwezesha kupata kazi haraka baada ya kumaliza tu chuo. Hakukaa mtaani kwa muda mrefu kama wengine wanaosotea ajira kuliko muda aliokaa shuleni.

Hida alipomaliza kidato cha sita Jumuiya Tanga, akaunganisha chuo kikuu. Baada ya kumaliza chuo akaunganisha kwenye ajira moja kwa moja. Mtaa au watoto wa mtaa hawajui kabisa, alikuwa maamuma wa kutambua tabia za watoto wa mjini. Zuzu.

Kwa uzuzu wake ndo akajikuta mikononi mwa muhuni Jeff. Na hapa ndipo akaanza kulijua Jiji na wana wa Jiji. Kila alichofanyiwa au kuoneshwa na Jeff ilkuwa ni ‘sapraizi’ kwake. Ni wazi kwamba kwa miaka mitatu pale Mlimani, Hidaya aliishi Kiustaadh Ustaadh sana.

‘Angejimiksi’ kama madenti wengi wa pale wanavyojimiksi. Ilikuwa  rahisi kujua kama Jeff siyo mume mtarajiwa bali ni ‘eksi’ ajaye. Hali hii ilimchukua muda mrefu sana, kuamua kwa dhati ya moyo wake kuachana na Jeff. Na siku hii ndo ikawa mwisho wake kwa Jeff.

Jeff ni dogo aliyelelewa upande mmoja wa mama. Mama’ke ndo wale ‘masista duu’ wa miaka ya Nora na Dk Cheni. Beckham na Posh, Puff Daddy na J-Lo, Justin Timberlake na Britney Spears. Ni enzi zile za ‘aitivii’ na mchezo wa Tausi na Mambo Hayo, Bishanga na Aisha.

Kalelewa kihuni bila maadili. Bila hofu ya mjomba, shangazi wala bamdogo achana na mshua. Ni wale watoto ambao wamejikuta wakubwa bila kushuhudia mshua akienda bafuni na taulo kiunoni. Ni mwendo wa mama na shosti zake tu. Nadhani naeleweka.

Ni ngumu Jeff kuishi na Hidaya. Jeff hana adabu. Washikaji zake tumefanya bonge la ‘pati’. Baada ya Jeff kuachika, na Hida kuwa nyumba ndogo ya bosi. Ni bora awe mke mdogo kwa bosi wake kuliko awe dem wa mwehu Jeff. Jeff hajui vikao vya kiumeni na hana analoweza kusaidia jamii.

Jeff kijana wa ovyo kama vijana wengine wasio na adabu, hofu wala aibu. Kwa sasa ni kama Jeff kapoteza nuru na kujiamini. Akili zinamrudi na kuona alichemka. Ni kupatwa kwa Mwezi wa Mapenzi ndani ya Mwezi Mtukufu. Marafiki zake tunashukuru Hidaya kutoka mikononi mwake.

Huu mwezi Hidaya ana ndoa ya ‘Uji’ ya Ramadhani’. Bosi wake kaamua kumuhifadhi kwa huu mwezi, binti aepukane na zinaa. Na kwa tunaomjua Hidaya, hii ndo imetoka hawezi kuachika kabisa. Ni mpuuzi pekee wa kuiacha pisi kali kama Hidaya. Na bosi wetu siyo mpuuzi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *