Dar es Salaam. Msanii wa Hip Hop Bongo, Joh Makini (45), ambaye anayawakilisha vizuri makundi ya River Camp na Weusi, mwaka huu utatimiza miaka 20 tangu ametoka rasmi kimuziki.
Joh Makini, zamani Rapcha, alivuma kwa mara ya kwanza kupitia wimbo wake maarufu hadi sasa, Chochote Popote (2006) ambao ulitayarishwa na Dunga wa Madungu Digital.
Tangu wakati huo, ameendelea kufanya makubwa katika rap akitoa albamu, EP na kushinda tuzo, na sasa wengi wanamchukulia kama chapa inayouzika zaidi sokoni, kitu ambacho mwenyewe amekuwa akijivunia.
Chochote Popote ni wimbo wa mapenzi na harakati za utafutaji maisha ambao Joh Makini aliutumia kuzungumza na mwanamke aliyempenda akimueleza yupo tayari kwa lolote katika safari ya uhusiano wao.
Hata hivyo, katika verse ya kwanza tu, anakiri kuwa mambo ya fedha kwake bado hayajakaa vizuri, na ukizingatia bado ana mipango ya kubadilisha maisha ya nyumbani kwao na kuwapeleka wadogo zake shule.
Lakini hilo halimzuii kuwa na picha ya kubwa ya uhusiano wao kiasi kwamba cha kuufanisha na ule wa rapa kutokea Marekani, Jay Z na mkewe Beyonce Knowles ambao ulianza mwishoni mwa miaka ya 1990.
“Njoo mami nawe twende bega kwa bega, ingawa kwangu kipato bado mambo si shega. Ni kama ndio nipo manta nachoronga kwa diga, nipige jiwe tuwe safi kama Beyonce na Jigga [Jay Z],” anarap Joh Makini.
Joh Makini ambaye baadhi ya watu wamekuwa wakidai rap style yake inafanana na ile ya Jay Z, si tu alitumia wimbo huo kuyaimba mapenzi, bali pia kuonyesha anavyomkubali rapa huyo wa Roc-A-Fella.
Jay Z aliyetoka na albamu yake, Reasonable Doubt (1996), baada ya Chochote Popote (2006), jina lake lilikuja kusikika katika nyimbo nyingine za Joh Makini ikiwemo Stimu Zimelipiwa (2009) na Waya (2017).
Hata hivyo, Joh Makini hakuweza kutoa video ya wimbo huo badala yake alikuja kuujumuisha katika albamu yake ya kwanza, Zamu Yangu (2007) iliyokuwa na ngoma nyingine kali kama Sintochoka na Tomorrow.
Baada ya muda mfupi tu, mfululizo wa ngoma kali nyingine kutoka kwake ulichukua nafasi akitamba na nyimbo kama ‘Ufalme’, ‘Muda’, ‘Niaje Nivipi, ‘Stimu Zimelipiwa’, na ‘Kila Wakati’ akiwashirikisha na Bushoke na Nikki wa Pili.
Joh Makini aliendelea na moto huo hadi alipokutana na Pancho Latino, mtayarishaji muziki aliyeanza kazi studio kwa Dully Sykes, 4.12, zamani Dhahabu Records, kisha akaja kuhamia B’Hits (sasa Bxtra) kwa Hermy B.
Pacho ambaye sasa ni marehemu, hadi sasa Joh Makini anamtaja kama mtu mwenye uwezo mkubwa (genius) wa muziki kwa namna alivyomtengenezea midundo mikali ya ngoma zake.
Nyimbo za Joh Makini zilizotengenezwa na Pancho ni Karibu Tena (2010), Brand (2010) na Bye Bye (2011), pamoja na ule wa Nikki wa Pili, Higher (2010) ambao alishirikishwa.
Je, kwanini tumechagua kumzunguzia Pancho zaidi wakati Joh Makini amefanya kazi watayarishaji wengi katika miaka hii 20 ndani ya Bongofleva?, sababu ni mbili kama ifuatavyo.
Mosi; kufanya vizuri kwa wimbo wake, Karibu Tena (2010), kulimuwezesha kushinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) kama Msanii Bora wa Hip Hop 2011, akiwabwaga Fid Q, Ngwea, Chid Benzi na Godzilla.
Tuzo hiyo aliyokabidhiwa jukwaani na Besta na mumewe Marlaw, ndio ilikuwa ya kwanza kwa Joh Makini kushinda ikiwa ni miaka miwili baada ya kukosoa mfumo wa tuzo kupitia wimbo, Stimu Zimelipiwa (2009).
Pili; katika uzinduzi wa video ya wimbo, Bye Bye (2011) uliofanyika Maisha Club mnamo Oktoba mwaka huo, ndipo na kundi la Weusi lilizinduliwa rasmi, hatua iliyoleta sura nyingine ya muziki wa Joh Makini.
Ujio wa Weusi ulitokana na muunganiko wasanii wa River Camp na Nako 2 Nako, ambapo awali ushirikiano wa mara kwa mara wa wasanii wa makundi hayo ulitambulika kama Good Music Family (GMF).
Wasanii waliotoka River Camp ili kuunda Weusi ni Joh Makini, Nikki wa Pili na Bonta, huku Nako 2 Nako wakitoka G Nako na Lord Eyes ambaye awali kabisa alikuwa kundi la Hood Squard Hardcore Unit.
Weusi walivuma kwa mara ya kwanza na wimbo wao, Gere (2013) uliotayarishwa na Nahreel. Ni wimbo uliowaweza kushinda tuzo mbili za TMA 2014 kama Kundi Bora la Mwaka na Wimbo Bora wa Hip Hop.
Hadi sasa Weusi wametoa albamu moja, Air Weusi (2021), huku Joh Makini akiendelea kusalia kama msanii kinara ndani ya kundi. Mathalani ni yeye na G Nako tu ndio hawajawahi kukosekana katika wimbo wowote wa Weusi.
Mnamo 2017, Joh Makini alitangaza ujio wa albamu yake ya pili aliyoipa jina la ‘God Engineering’ lakini haikutoka badala yake alikuja kutoa Extended Playlist (EP), Wave (2023).
Pia amefanya kazi na wasanii wa kimataifa kama AKA (Don’t Bother – 2015), Chidinma (Perfect Comb – 2016), Davido (Kata Leta – 2017) n.k, na ana kolabo na Fallz, Y Cee na Cassper Nyovest, hizi bado hazijatoka.