
KIUNGO mshambuliaji wa Singida Black Stars, Offen Chikola amesema msimu huu upande wake ni wa kujifunza vitu vingi, huku akiwa amecheza kwa dakika 50 pekee dhidi ya Fountain Gate tangu ajiunge na timu hiyo kwa mkopo kipindi cha dirisha dogo Januari 2026 akitokea Yanga.
Chikola aliyejiunga na Yanga msimu huu kwa mkataba wa miaka mitatu akisajiliwa kutoka Tabora United (sasa TRA United), amesema ushindani wa alipotoka ni tofauti jambo la msingi ni kukua kiuwezo, akiamini siku za usoni atakuwa mchezaji mkubwa ndani na nje.
“Hakuna mafanikio rahisi, Yanga ilinisajili baada ya kufanya vizuri Tabora baada ya kumaliza msimu uliopita nikiwa na mabao saba na asisti mbili, ninachotakiwa kukifanya ni kuendelea kupambana bila kukata tamaa, ikifika zamu yangu nitacheza na kuwa tegemeo kikosi cha kwanza,” amesema Chikola na kuongeza:
“Lengo la Yanga kunitoa kwa mkopo ni kuhakikisha napambana na napata nafasi ya kucheza, siyo kwamba Singida Black Stars ni timu rahisi, ina wachezaji wenye uzoefu mkubwa ambao wananipa chalenji ya kuongeza bidii.”
Amesema kazi ya mpira wa miguu siyo wa kuonewa huruma, inahitaji mapambano na kukaza buti, hivyo kitu kikubwa kwake kwa sasa ni kuangalia wanaopata nafasi ubora wao na kuongeza bidii.
Yanga imemtoa kwa mkopo Chikola ili kwenda kupata muda zaidi wa kucheza baada ya kuonekana kuwa ngumu mbele ya Pacome Zouzoua ambaye msimu uliopita alifunga mabao 12 na asisti 10, Maxi Nzengeli (mabao 6, asisti 10), Clement Mzize (mabao 13, asisti tano), Edmund John na ameongezeka Allan Okello.
Kwa upande wa Singida Black Stars, amekwenda kukutana na ushindani wa Ayoub Lyanga, Lamine Jarjou, Mishamo Daudi na Deus Kaseke.