Marekani. Mwigizaji na mwanamuziki kutoka Marekani, Selena Gomez (33,) ameshauriwa kuachana na mume wake, Benny Blanco, (37), kwa kile kinachodaiwa kuwa ameshindwa kujijali linapokuja suala la usafi.
Ushauri huo umetoka kwa baadhi ya mashabiki wake mara baada ya miguu ya Blanco kuonekana ikiwa michafu katika uzinduzi wa Podcast yake mpya iitwayo Friends Keep Secrets.
Blanco ambaye ni mtayarishaji muziki, alizindua podcast hiyo mapema wiki hii akiwa pamoja na rafiki yake wa karibu Lil Dicky na mke wa Lil Dicky, Kristin Batalucco.
Wakati wa kipindi hicho, Blanco alionekana amekaa kwenye kochi bila kuvaa viatu na ndipo miguu yake ikionekana kuwa na uchafu, kitu ambacho kimezua maswali mengi kwa mashabiki waliokuwa wakifuatilia.
Mashabiki wa Selena ndio hasa waliochukia, baadhi wameonyesha wazi kabisa kuwa hawakufurahishwa na tukio hilo na wameeleza hisia zao kwenye mitandao ya kijamii.
Mtu mmoja aliandika (comment) chini ya video hiyo ya podcast; “Siwezi kuamini kwamba Selena anamruhusu amguse.”. Mwingine aliandika: “Kwanini hasa ameamua kuolewa naye kati ya wanaume wote duniani?”.
“Hiyo inatia kinyaa, sielewi Selena anavumiliaje,” alieleza mtumiaji mmoja wa mtandao wa X, zamani Twitter.
Baadhi ya mashabiki hata walimshauri Selena aachane na Blanco. Mtu mmoja aliandika;
“Selena anatakiwa kuachana naye na kutafuta mtu bora zaidi,”. Na mwingine aliongeza; “Sijawahi kukatishwa tamaa na Selena kama sasa.”
Hata hivyo, hii si mara ya kwanza kwa Blanco kuzua mjadala kuhusu usafi wake. Katika mahojiano na Jarida la People mnamo Novemba 2024, alikiri kwamba huwa haogi kila siku!.
“Baadhi ya watu ninaowajua huoga mara mbili au tatu kwa siku, lakini mimi nahisi hilo linaweza kufanya mafuta yaliyopo kwenye ngozi yako kutopata muda wa kujirudisha ili kuwa na unyevu au mvuto,” alisema.
Licha ya hilo, Selena aliwahi kueleza sababu iliyomfanya ampende Blanco, ni baada ya kutajwa kwenye orodha ya Jarida la People ya wanaume wanaovutia zaidi kwa mwaka 2024.
“Si tu kwamba unanipenda bila masharti… lakini kila mara unaniletea pizza ya Taco Bell Mexican ambayo ninayoipenda,” alieleza Selena kupitia ukurasa wake wa Instagram.
Mnamo Novemba 2025, ndipo Selena alifunga ndoa na Blanco ambaye wamefanya kazi pamoja katika albamu, I Said I Love You First… And You Said It Back (2025).
Kabla ya kuwa na Blanco, huku nyuma Selena aliwahi kuwa na wanaume kadhaa, baadhi yao ni wanamuziki kutokea Canada, Justin Bieber na the Weeknd ambaye walidumu kwa takribani miezi tisa.
Ikumbukwe kwa sasa Selena anashikilia rekodi kama mwanamke mwenye wafuasi (followers) wengi zaidi katika mtandao wa Instagram akiwa nao milioni 415, huku akifuatiwa na Kylie Jenner.