DAR ES SALAAM: Mkuu wa Magereza Mkoa wa Dar es Salaam, Rashid Mangara, amezitaka taasisi za kifedha kuongeza ubunifu katika utoaji wa huduma zao, hususan mikopo yenye masharti nafuu ili kuwasaidia wajasiriamali wadogo kukuza shughuli zao za kiuchumi.

Mangara ametoa kauli hiyo leo Februari 28, jijini Dar es Salaam, wakati wa semina ya elimu kuhusu matumizi ya nishati safi na umuhimu wa kuweka akiba. Amesema upatikanaji wa mikopo yenye masharti rafiki utasaidia kuongeza kipato na kuimarisha ustawi wa wananchi, hususan makundi yenye uhitaji maalumu.

Katika semina hiyo, amewahimiza askari wa magereza kujipanga na kutumia ipasavyo fursa za kifedha pamoja na mafunzo mbalimbali yanayotolewa na taasisi tofauti, ili kujiimarisha kiuchumi. Amesisitiza kuwa nidhamu ya kifedha na uwekezaji sahihi ni msingi wa maendeleo binafsi na ya taifa kwa ujumla.

Aidha, Mangara ameeleza kuwa jamii inapaswa kuchukua hatua za makusudi katika matumizi ya nishati safi kwa manufaa ya afya, uhifadhi wa mazingira na ustawi wa jamii kwa ujumla.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya TAWEN, Florence Masunga, amesema lengo la kutoa elimu ya nishati safi katika magereza ni kuhakikisha kuwa elimu hiyo inawafikia watu wa kada zote, ikiwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *