WATUMISHI wa idara ya afya Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza wamepatiwa mafunzo ya matumizi sahihi na salama ya gesi ya kupikia sambamba na kuelezwa kwa kina madhara yanayotokana na matumizi ya kuni na mkaa kiafya.
Mafunzo hayo yametolewa na Kampuni ya Oryx Gas Tanzania, lengo ikiwa ni kuiwezesha kada hiyo ya sekta ya afya kuwa na uelewa mpana kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia ya gesi na kisha watumishi hao wawe mabalozi kwa wananchi wengine wakiwemo wagonjwa.
Akizungumza jana wakati wa utolewaji wa mafunzo hayo kwa watumishi wa sekta ya afya Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza, Mkuu wa Mafunzo wa Kampuni ya Oryx Gas Tanzania, Peter Ndomba amesema hatua hiyo ni katika muendelezo ule ule wa jitihada za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia
“Oryx Gas tumeamua kutoa mafunzo haya kwa watumishi wa afya wa Wilaya ya Kwimba kwa sababu tunajua wananchi wanapopata matatizo ya kiafya wanakuja hospitali kwa hiyo wale ndio wanakuwa watu wa kwanza kukutana na wananchi wenye matatizo.

“Kwa hiyo tumeamua kuwapa mafunzo ya ndani kabisa kuhusu matumizi sahihi ya gesi,usalama na kila kitu kuanzia athari ya kimazingira pamoja na athari za kiafya.
“Tumekuwa na kundi kubwa la watumishi wote wa sekta ya afya zaidi ya 267 wakiwemo wa Hospitali ya Wilaya ya Kwimba na wamepata mafunzo haya kwa siku mbili kuhusu nishati safi ya kupikia
“Tunafurahi mwitikio ni mkubwa na mafunzo haya ni mwanzo tu kwani tutakwenda katika taasisi zote,shule mbalimbali na kila jukwaa tutaweza kufika ili sasa muendelezo mzima wa matumizi ya nishati safi uweze kufikia watu wote,” amesema.
Aidha Ndomba ametoa shukrani uongozi mzima wa Hospitali ya Wilaya ya Kwimba, DMO pamoja na mganga mfawidhi kwa kuwapatia nafasi ya kukutana na madaktari na wauguzi kuwapa elimu ya gesi ambayo watu wengi hawaijui.
“Tumegundua kuna haja ya kupeleka elimu hii kwao ili wawe mabalozi wanapokutana na wananchi,wagonjwa hasa wamama wanaokuja hospitali kwa matatizo mbalimbali na kuwafafanulia kwamba matumizi ya nishati ndio jambo muhimu na itasaidia kupunguza matatizo mengi yanayotokea kutokana na matumizi ya kuni na mkaa,”amesema Ndomba.

Kwa upande wao watumishi wa sekta ya afya katika Wilaya hiyo wameishukuru kwa kupatiwa mafunzo hayo ambapo wengine wamekiri wamekuwa wakitumia gesi ya kupikia kwa muda mrefu lakini hawakuwa wanajua faida na hasara zake lakini kupitia mafunzo hayo sasa watakuwa mabalozi kwa wengine.
Kwa upande wake Christian Mvula, amesema ambaye Muuguzi Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Kwimba amesema wanashukuru Oryx kwa kuwapatia mafunzo ya matumizi sahihi ya gesi sambamba na kuachana na mkaa na kuni na kuingia katika matumizi ya gesi.

“Ukweli tumepata elimu sahihi ya kutumia gesi ya kupikia kama nishati ya kupikia majumbani na sisi watumishi tunafurahi kupata huduma hiyo na kimsingi tulikuwa tunateseka kutumia kuni na mkaa ambayo wakati mwingine ni ngumu kupatikana hasa kipindi hiki cha mvua,” amesema.
Wakati huo huo Ofisa Muuguzi, Salome Malale amesema ametumia gesi kwa miaka 15 lakini hakujua faida na hasara za gesi na yeye kama muuguzi kuna changamoto nyingi zimetokea kwa mfano jamii nyingi zinatumia kuni na mkaa.