Kadiri matamshi ya kivita yanavyozidi kutoka kwa Rais wa Marekani, Donald Trump, pamoja na baadhi ya maafisa wa utawala wake, wimbi jipya la upinzani dhidi ya uwezekano wa a vita vya kichochezi vya Marekani dhidi ya Iran limeanza kushika kasi.

Kwa mujibu wa ripoti ya Pars Today, kuongezeka kwa kauli za uchokozi na vitisho vya kijeshi vinavyotolewa na Trump na baadhi ya watu wa karibu na serikali yake dhidi ya Iran kumesababisha kuibuka kwa hali mpya ya wasiwasi na upinzani miongoni mwa wananchi wa Marekani.

Katika mwelekeo huu, kura mpya ya maoni iliyofanywa nchini Marekani imebaini kuwa Wamarekani wengi wana imani ndogo kwa busara ya Trump, kuhusu suala la kutumia nguvu za kijeshi nje ya mipaka ya Marekani.

Utafiti mpya wa AP‑NORC—uliofanywa na Shirika la Habari la Associated Press kwa ushirikiano na Kituo cha Tafiti za Maoni ya Umma cha NORC—ambao matokeo yake yalitangazwa siku ya Alhamisi tarehe 26 Februari, unaonyesha kuwa kiwango cha imani ya wananchi wa Marekani kwa maamuzi ya Trump kuhusu uhusiano na mataifa yanayoonekana kuwa hasimu, pamoja na matumizi ya nguvu za kijeshi nje ya nchi, kiko chini.

Hata ndani ya Chama cha Republican, baadhi ya wanachama—hasa Warepublican wa kizazi cha vijana—wanaonyesha wasiwasi na mashaka juu ya uwezo wa Trump wa kufanya maamuzi sahihi na yenye mizani katika masuala haya nyeti

Kwa mujibu wa matokeo ya kura hii ya maoni, Wamarekani pia wana mashaka makubwa kuhusu busara ya Donald Trump katika kushughulikia migogoro ya nje ya nchi. Ni takribani watu 3 tu kati ya kila 10 ya watu wazima nchini Marekani wanaosema wana imani kubwa au ya kiasi fulani kwa uamuzi wa Trump kuhusiana na matumizi ya nguvu za kijeshi, mahusiano na mataifa hasimu, au matumizi ya silaha za nyuklia.

Kwa upande mwingine, zaidi ya nusu ya washiriki wa utafiti walisema wana imani ndogo sana au hawana kabisa imani na uamuzi wake katika masuala hayo nyeti. Kura hii ya maoni ilifanywa kwa watu 1,133 wazima wa Marekani katika kipindi cha kati ya tarehe 19 hadi 23 Februari 2026.

Mashaka kuhusu uwezo wa Trump kuchukua maamuzi sahihi hayapo tu miongoni mwa wananchi wa Marekani, bali pia yanaonekana wazi katika ngazi ya wanasiasa wakuu wa nchi hiyo, hasa ndani ya chama cha upinzani cha Democratic.

Katika muktadha huu, Kamala Harris, mwanasiasa wa Democratic wa Marekani aliyechuana na Trump katika uchaguzi wa rais, akizungumza kuhusu kuongezeka kwa mvutano unaochochewa na Marekani katika eneo la Asia Magharibi, alisema: “Watu wa Marekani hawataki vita vingine. Hawataki vijana wetu kutumwa kuanzisha hatua ambazo zingeweza kuepukwa kupitia diplomasia.”

Harris pia alionyesha wasiwasi wake kuhusu kuongezeka kwa mvutano na Iran, akisisitiza kuwa washirika wa Marekani hawaungi mkono shambulio lolote litakalofanywa na rais. Aidha, alitoa onyo kwamba kudhoofisha miungano ya kimataifa si jambo jema kwa usalama wa taifa wa Marekani.

Mashaka kuhusu mwelekeo wa kichokozi wa Trump hayajaishia kwa wananchi wa Marekani pekee, bali pia yanaonekana wazi miongoni mwa wanasiasa wakuu wa nchi hiyo, hususan ndani ya Chama cha Democratic.

Katika muktadha huu, Chris Van Hollen, seneta wa Democratic kutoka jimbo la Maryland, katika kipindi hiki cha kuongezwa kwa zana za kivita za Marekani katika eneo la Asia Magharibi kwa amri ya Trump, ameandika kwenye mtandao wa kijamii wa X akirejelea uzoefu wa vita vya Marekani nchini Iraq na kuuliza: “Je, tumesahau kilichotokea Iraq?”

Van Hollen amekumbusha kiwango kikubwa cha vifo na gharama kubwa ambazo Marekani ilibeba wakati wa uwepo wake wa kijeshi nchini Iraq, akisema kuwa zaidi ya Wamarekani 8,000 na mamia ya maelfu ya raia wa Iraq waliuawa, huku trilioni za dola zikitumika. Amesisitiza kuwa hakuna mtu aliyefafanua ni kwa namna gani vita dhidi ya Iran vinaweza kuinufaisha Marekani, na akaongeza kwa msisitizo: “Kwa sababu havitasaidia.”

Kwa hivyo, wimbi jipya la upinzani dhidi ya vita nchini Marekani—ambalo katika tafiti za hivi karibuni linaonyesha kuwa chini ya asilimia 30 ya wananchi wanaunga mkono matumizi ya chaguo la kijeshi dhidi ya Iran, linapita zaidi ya tofauti ya kawaida ya kisiasa.

Hali hii ina mizizi katika kutokuaminiana baina ya umma na utawala wa Trump, na inaashiria mgawanyiko wa kimsingi katika mtazamo wa vita na amani ndani ya jamii ya Marekani.

Aidha baadhi ya wanasiasa wa chama cha Trump cha Republican wanapinga vita  kutokana na msimamo wa wananchi waliowengi.

Sababu muhimu zaidi ya hali hii ya kutokuaminiana ni kupuuzwa wazi kwa Bunge la Marekani (Congress) na hekima ya pamoja katika maamuzi makubwa ya kitaifa.

Tofauti na kipindi kilichotangulia vita vya Iraq, ambapo serikali ya George W. Bush ilianzisha kampeni pana ya propaganda ili kupata uungwaji mkono wa umma, utawala wa Trump umeendelea kuandaa mazingira ya uwezekano wa vita dhidi ya Iran bila kutoa maelezo ya wazi au kufanya vikao vya kusikilizwa katika Bunge.

Wabunge wakuu wa chama cha upinzani cha Democratic, akiwemo Gregory Meeks na Adam Smith, wamesisitiza kuwa Ikulu ya White House haikujaribu hata kupata idhini ya Bunge, wala haikuwasilisha au kueleza mpango wake kwa wawakilishi wa wananchi. Tabia hii imeelezwa kama mfano wa maamuzi ya kiimla katika suala la vita, ambapo ridhaa ya watu na taratibu za kidemokrasia zinawekwa pembeni.

 

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *