London, England. Ndio hivyo. Arsenal imewekwa kwenye nafasi kubwa ya kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu baada ya droo iliyopangwa Ijumaa kuonekana imekaa vizuri upande wao.

Chama hilo linalonolewa na kocha Mikel Arteta limepangwa katika upande wa droo utakaowafanya waepuke kukutana na timu kama Manchester City, Liverpool, Chelsea, Real Madrid, Bayern Munich na Paris Saint-Germain labda kwenye fainali tu itakayofanyika Budapest, Mei 30.

Katika hatua ya mtoano ya 16 bora, Arsenal imepangwa kukutana na Bayer 04 Leverkusen. Arteta na jeshi lake akifanikiwa kupenya hapo, atakwenda kucheza dhidi ya mshindi kati ya FK Bodoe/Glimt na Sporting CP katika hatua ya robo fainali.

Katika nusu fainali, Arsenal inaweza kukutana na Tottenham Hotspur, Newcastle United, Barcelona au Atletico Madrid, mechi ambazo kwenye karatasi zinaonekana si ngumu sana ukilinganisha na kama ingepangwa kupita kwenye ile njia nyingine. Kwenye upande huo wa mechi za nusu fainali, tishio la Arsenal linaweza kuwa kwenye mechi dhidi ya Barcelona au Atletico Madrid. Hata hivyo, nazo si tishio.

Kutokana na kumaliza nafasi ya kwanza katika msimamo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya katika raundi ya makundi iliyochezwa kwa mtindo wa ligi, Arsenal itakuwa na faida ya kucheza mechi ya marudiano nyumbani katika kila hatua.

Hiyo ndiyo sababu kampuni ya takwimu ya Opta imewapa kikosi cha Arteta nafasi kubwa zaidi ya kunyanyua kombe hilo Mei mwaka huu. Arsenal imepewa asilimia 27 ya kushinda ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya kwanza katika historia yao.

Hiyo ni karibu mara mbili ya nafasi iliyopewa wababe wa pili, Bayern Munich, ambayo iko mbele kidogo ya Liverpool. Wapinzani wa Arsenal katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England, Manchester City, yenyewe imepewa nafasi ya nne ikiwa na asilimia 10 baada ya kupangwa dhidi ya Real Madrid katika hatua ya 16 bora.

Katika nafasi ya tano, Barcelona imepewa nafasi ya asilimia saba. Mabingwa hao wa La Liga wako juu ya Chelsea, Newcastle na PSG katika viwango hivyo vya nafasi za timu kunyakuwa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya katika asilimia.

Labda mshangao mkubwa ni Real Madrid. Mabingwa hao wa kihistoria, waliobeba taji la Ulaya mara 15 wamepewa nafasi ya asilimia mbili tu ya kushinda taji lao la 16, licha ya kikosi chao kusheheni nyota wa viwango bora. Na wasiwasi huo umekuja baada ya Los Blancos kuhitaji mechi ya mchujo dhidi ya Benfica ili kutinga kwenye hatua ya 16 bora.

Timu ya England iliyopewa nafasi ndogo zaidi ni Spurs, itakayokutana na Atletico Madrid katika hatua ya 16 bora. Opta wameipa Spurs nafasi ya asilimia moja tu, huku kiwango chao cha uwanjani kwenye mechi za Ligi Kuu England msimu huu kikionyesha mashaka makubwa.

Akizungumza baada ya droo ya Ijumaa, kocha Arteta alisema: “Tuna hamasa kubwa sana. Tunapambana katika mashindano manne na jinsi timu inavyocheza kwa uthabiti kunatupa matumaini na mawazo chanya kuhusu yajayo. Lakini, tunaweza kuangazia wakati wa sasa tu.

“Hapo ndipo tutaweka nguvu zetu na ni Jumapili (dhidi ya Chelsea). Nazingatia sana kile tunachopaswa kufanya ili kuendelea katika mwenendo na mwelekeo tulionao kama timu na kutoka hapo kujaribu kuboresha zaidi.”

Fainali ya mwaka huu itafanyika Jumamosi, Mei 30 katika uwanja wa Puskás Aréna. PSG ndio mabingwa watetezi baada ya kuifunga Inter Milan mabao 5-0 katika fainali ya mwaka jana. Mambo yatakuwa msimu huu? Utabiri unaotabiriwa kwa Arsenal utatimia? Ngoja tuone!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *