Wizara ya Mambo ya Nje ya China imeeleza wasiwasi wake kuhusu mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran na kutoa wito wa kusitishwa mara moja kwa mapigano, ikizitaka pande zote kuepuka kuongezeka kwa mvutano na kurejea kwenye mazungumzo na majadiliano.
Kwa mujibu wa Reuters, katika taarifa iliyotolewa Jumamosi, Februari 28, 2026, wizara hiyo ilieleza mamlaka ya Iran, usalama wake na ukamilifu wa mipaka yake vinapaswa kuheshimiwa.
Leo, Machi Mosi, 2026, Ubalozi wa China nchini Israel umetoa notisi ukiwashauri raia wa China waliopo Israel kuhamia maeneo salama ndani ya nchi hiyo haraka iwezekanavyo au kuondoka kuelekea Misri kupitia mpaka wa Taba.
Wizara ya Mambo ya Nje ya China, pia, imewasihi raia wake waliopo Iran kuondoka haraka iwezekanavyo, ikiorodhesha njia nne za ardhini kupitia Azerbaijan, Armenia, Uturuki na Iraq.
Marekani na Israel zilianzisha mashambulizi dhidi ya Iran Jumamosi, zikilenga uwezo wake wa kijeshi. Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, aliuawa katika operesheni hiyo, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali.
Katika makala ya maoni, leo Jumapili, shirika la habari la serikali ya China, Xinhua, lilikosoa mashambulizi hayo, likiyataja kuwa ni uchokozi wa wazi dhidi ya taifa huru na mfano wa siasa za nguvu na ubeberu.
Xinhua limesema matumizi ya nguvu za kijeshi kwa Marekani ni ukiukwaji wa wazi wa madhumuni na misingi ya Hati ya Umoja wa Mataifa na ni kuacha kanuni za msingi za uhusiano wa kimataifa.
Wakati huohuo, kampuni ya ndege yenye makao yake Hong Kong, Cathay Group, Jumamosi ilisimamisha safari zake katika eneo la Mashariki ya Kati, ikitaja mvutano wa kikanda kufuatia mashambulizi hayo.
Hatua hiyo inaathiri safari za abiria kwenda na kutoka Dubai na Riyadh, pamoja na safari za mizigo zinazopita katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Al Maktoum jijini Dubai, kwa mujibu wa taarifa ya Cathay, kampuni mama ya Cathay Pacific Airways.
Ilisema pia kuwa inabadilisha njia za ndege ambazo kwa kawaida hupita juu ya eneo lililoathirika.