Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Solomon Itunda amewahimiza wanawake kuendelea kuwa chachu ya mabadiliko chanya katika jamii kwa kusimamia maadili, kupinga vitendo vya mmomonyoko wa maadili na kuhamasisha mshikamano wa kifamilia na kijamii.

Itunda ameyasema hayo Jumamosi Februari 28, 2026 katika ukumbi wa VETA jijini Mbeya alipokuwa amemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa, katika Kongamano la Kitaifa la Wanawake wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT).

Akizungumza wakati wa kongamano hilo kwa niaba ya mkuu wa mkoa, Itunda aliwapongeza wanawake wa CCT kwa kuandaa kongamano hilo muhimu lililowakutanisha washiriki kutoka mikoa zaidi ya 13 nchini, akisisitiza kuwa mchango wa wanawake katika maombi, maadili na malezi ya kizazi una nafasi kubwa katika kuijenga Tanzania yenye amani, mshikamano na hofu ya Mungu.

Itunda ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuthamini na kushirikiana na taasisi za kidini katika kukuza maadili, kuimarisha amani na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Amesisitiza kuwa maombi ya pamoja kwa Taifa ni nguzo muhimu ya kuimarisha umoja wa kitaifa na ustawi wa wananchi.

Katika hotuba yake, Itunda amebainisha kuwa wanawake ni nguzo ya Taifa na wanayo nafasi ya kipekee katika kulea kizazi chenye uzalendo na nidhamu.

Aidha, amewashukuru viongozi wa dini kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuhubiri amani na utulivu, akisema kuwa Mkoa wa Mbeya utaendelea kuwa kitovu cha mikutano na makongamano yenye tija kwa Taifa kutokana na mazingira yake ya amani na ushirikiano mzuri kati ya Serikali na taasisi za kidini.

Kongamano hilo limehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini akiwemo Askofu wa Dayosisi ya Konde wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Baba Askofu Gefrey Mwaihaba, Askofu wa Kanisa la Moravian Jimbo la Mbeya pamoja na Askofu wa Kanisa la Anglikana, sambamba na

Katibu Mkuu Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) ni Mchungaji Canon Dk Moses Matonya.

Kongamano hilo la kitaifa limehitimishwa kwa maombi maalum ya kuliombea Taifa, viongozi wa Serikali na Kanisa, pamoja na kuhimiza umoja, upendo na mshikamano miongoni mwa Watanzania, huku Serikali ikiendelea kuwatambua na kuthamini mchango wa wanawake wa CCT katika kujenga Taifa lenye maadili na hofu ya Mungu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *