MWANZA: Jengo la kisasa lenye viwango vya kimataifa kwa ajili ya kuhudumia watoto njiti limezinduliwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza na Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, Dk Mohamed Janabi.

Dk Janabi alimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus.

Jengo hilo limejengwa na Doris Mollel Foundation chini ya Mkurugenzi Mkuu wake, Doris Mollel, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo.
Miongoni mwa wadau hao ni Keep a Child Alive ya msanii maarufu wa Marekani Alicia Keys, pamoja na Jhpiego, DAMAC Foundation na marafiki wa Doris Mollel Foundation.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi huo, Dk.Janabi amesema Tanzania imeendelea kupiga hatua katika kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka mitano.
Amesema takwimu zinaonesha vifo hivyo vimepungua kutoka 81 hadi 68 kwa kila watoto 1,000 wanaozaliwa hai kati ya mwaka 2015 na 2022.

Ameeleza kuwa mafanikio hayo yametokana na juhudi za Serikali kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya afya, akiwemo Doris Mollel, ambao wamewekeza katika kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto, hususan kwa watoto njiti wanaohitaji uangalizi maalum mara baada ya kuzaliwa.
Uzinduzi wa jengo hilo unatarajiwa kuongeza uwezo wa hospitali hiyo kutoa huduma bora, kupunguza vifo vya watoto wachanga na kuimarisha ustawi wa jamii katika Mkoa wa Mwanza na maeneo ya jirani.