Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, amezitaka halmashauri, majiji, manispaa na vyombo vyote vinavyohusika na udhibiti kuacha kuwanyanyasa wajasiriamali wadogo, wakiwemo waendesha bodaboda, bajaji na mama lishe, na badala yake waachwe wafanye shughuli zao kwa uhuru.

Akijenga hoja hiyo huku akishangiliwa na wananchi, amesema iwapo mwendesha bodaboda au mama lishe atafanya kosa, anatakiwa kuandikiwa na kupewa muda wa kulipa faini badala ya kushikilia kitendea kazi chake akisema utaratibu wa kushikilia vifaa vyao ni wa kizamani.

Hayo amezungumza  leo, Machi 1, 2026, alipokuwa katika ziara ya kusikiliza kero za wananchi na kutoa ufumbuzi mkoani Manyara, amesema ni muhimu kwa vyombo vya udhibiti kuhakikisha kundi hilo linapata fursa ya kufanya kazi zao bila vikwazo visivyo vya lazima.

“Natoa rai kwa wenzetu wa halmashauri, majiji, manispaa na vyombo vyote vinavyohusika na masuala ya udhibiti tuwape Watanzania wafanye kazi kwa uhuru,” amesema.

Akiendelea, amesema kuwa faini zinazotolewa kwa wajasiriamali hao, kama vile waendesha bodaboda na bajaji, ziwe za manufaa na zisigeuke kuwa kikwazo katika shughuli zao.

Amesema endapo mwendesha bodaboda hatakuwa ametenda kosa kubwa, kama wizi wa kutumia silaha au ubakaji, vyombo vya usalama havina sababu ya kushikilia pikipiki au kuchukua sahani na sufuria za mama ntilie.

“Faini zisiwe kikwazo kwa mtu yeyote kufanya shughuli zake. Rais Samia Suluhu Hassan aliona umuhimu wa kupunguza faini ili watu waweze kuendelea na shughuli zao,” amesema

Waziri Mkuu amehoji namna mtu atakavyopata fedha za kulipa faini ikiwa atanyimwa fursa ya kufanya kazi yake, amewataka wadhibiti kutoa muda wa kutosha kwa wajasiriamali hao ili waweze kuendelea na kazi zao na hatimaye kutimiza wajibu wao kwa Serikali.

Kuhusu utaratibu wa kushikilia vitendea kazi, amesema kushikilia bajaji, vifaa vya mama lishe au bodaboda ni jambo la kizamani, akisema vitendea kazi hivyo ni kama ofisi kwa wajasiriamali hao, hivyo havipaswi kushikiliwa.

“Mwacheni afanye kazi ili aweze kulipa faini. Huu ni utaratibu wa kizamani, acheni tabia ya kuchukua vitendea kazi vya watu,” amesema

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya, amesema Serikali ina mpango wa kujenga barabara ya njia nne katika mji wa Babati, mkoani Manyara, ili kupunguza msongamano wa magari.

Amesema hatua hiyo inachukuliwa baada ya kubaini kuwa mji huo una idadi kubwa ya magari, hasa yanayotoka Mombasa, Kenya, na Tanga, ambayo hupita eneo hilo na kusababisha foleni inayokwaza shughuli za kiuchumi.

Kasekenya ameongeza kuwa Manyara ni miongoni mwa mikoa yenye mtandao mdogo wa barabara za lami, ukiwa na barabara kuu moja tu kutoka Arusha hadi Babati kuelekea Singida, na kutoka Babati kwenda Dodoma.

“Mkakati wa Serikali ni kuunganisha makao makuu ya wilaya na makao makuu ya mikoa. Manyara, wilaya pekee iliyounganishwa ni Hanang’, kwa kuwa kuna barabara inayounganisha na Singida,” amesema.

Ametaja pia barabara ya Mbuyu wa Mjerumani hadi Babati, akisema usanifu wake umekamilika na tathmini ya fidia imefanyika, hivyo ujenzi utaanza muda wowote. Amesema kuwa daraja kubwa katika barabara hiyo tayari limejengwa na kuzinduliwa na Makamu wa Rais mstaafu, Dk Philip Mpango.

Amesema barabara ya Babati hadi Kiteto tayari imefanyiwa usanifu na kinachosubiriwa ni upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wake ili kuunganisha wilaya hizo.

Kuhusu barabara ya Dareda hadi Dongobeshi inayounganisha na barabara ya Mbulu–Karatu, amesema ipo kwenye mpango wa kujengwa kwa kiwango cha lami baada ya kukamilika kwa usanifu wa kipande cha kilomita saba.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *