Tehran, Iran. Shirikisho la Soka la Iran limetishia kuiondoa timu ya taifa katika Kombe la Dunia lijalo kufuatia mashambulizi ya anga yaliyoripotiwa kufanywa na Marekani na Israel, yaliyosababisha kifo cha Kiongozi Mkuu wa nchi hiyo, Ayatollah Ali Khamenei.
Taarifa hizo zinakuja baada ya operesheni ya kijeshi iliyolenga maeneo kadhaa ya miji mikuu ya Iran, ikiwamo Tehran, kufuatia wiki kadhaa za mvutano wa kisiasa na kijeshi kati ya Iran na Marekani.
Mashambulizi hayo yamefanyika wakati kukiwa na mazungumzo kati ya Iran na Marekani kuhusu mpango wa nyuklia wa Tehran, ambapo Washington ilikuwa ikishinikiza kusitishwa kwa juhudi za Iran kumiliki silaha za nyuklia kwa kubadilishana na kuondolewa kwa vikwazo vya kiuchumi.
Timu ya taifa ya Iran, ambayo imefuzu kushiriki mashindano ya Kombe la Dunia ya 2026 yatakayofanyika Marekani, Canada na Mexico. Picha na Mtandao
Rais wa Shirikisho la Soka la Iran, Mehdi Taj, amesema hali ya sasa inatia shaka ushiriki wa timu hiyo katika mashindano hayo makubwa ya dunia.
“Kwa yaliyotokea leo na mashambulizi ya Marekani, ni vigumu kuzungumzia ushiriki wetu katika Kombe la Dunia,” amenukuliwa akisema kupitia televisheni ya Tehran.
Hata hivyo, amebainisha kuwa uamuzi wa mwisho utachukuliwa na viongozi wa michezo wa nchi hiyo.
Iran ilijihakikishia tiketi ya Kombe la Dunia kwa mara ya nne mfululizo baada ya kumaliza kinara wa Kundi A katika hatua za kufuzu barani Asia, ikiwekwa katika Kundi G pamoja na Ubelgiji, New Zealand na Misri.
Rais wa Marekani, Donald Trump (kushoto), akisalimiana na rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Gianni Infantino. Picha na Mtandao
FIFA kuanza uchunguzi
Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) limesema linafuatilia kwa karibu hali hiyo, miezi michache kabla ya mashindano kuanza katika nchi za Marekani, Canada na Mexico.
Katibu Mkuu wa FIFA, Mattias Grafstrom, amesema kuwa ni mapema kutoa maoni ya kina, lakini amesisitiza kuwa lengo lao ni kuhakikisha Kombe la Dunia linafanyika katika mazingira salama kwa timu zote zitakazoshiriki.
“Tunaendelea kufuatilia maendeleo ya matukio duniani. Lengo letu ni kuona Kombe la Dunia salama likiwahusisha washiriki wote,” amesema.
Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, ambaye anaripotiwa kuuawa kufuatia mashambulizi ya kijeshi ya Israel na Marekani dhidi ya Iran. Picha na Mtandao
Hali ya kisiasa yazidi kuchafuka
Wakati huo huo, Rais wa Marekani, Donald Trump, ameandika kwenye mtandao wa kijamii akithibitisha kifo cha Khamenei na kueleza kuwa tukio hilo ni haki kwa watu wa Iran na Wamarekani.”
Hata hivyo, wachambuzi wa siasa za kimataifa wanasema kifo cha Khamenei, hakimaanishi moja kwa moja mabadiliko ya haraka ya utawala nchini Iran, huku Tehran ikiripotiwa kujibu mashambulizi kwa operesheni zake katika maeneo mbalimbali ya Mashariki ya Kati.
Hali hiyo imezua taharuki si tu kisiasa bali pia katika sekta ya michezo, huku dunia ikisubiri uamuzi rasmi wa Iran kuhusu ushiriki wake katika mashindano hayo makubwa zaidi ya soka duniani.