Moshi naonekana ukifuka juu ya mji mkuu wa Iran Tehran, kufuatia shambulio la anga siku ya Jumamosi

Chanzo cha picha, Reuters

    • Author, Na Rashid Abdallah
    • Nafasi, BBC Swahili
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

“Kuongezeka kwa mapigano kunahatarisha kuharibu zaidi utulivu wa dunia, na athari kubwa kwa biashara ya nishati, usalama wa chakula, na uchumi – hasa barani Afrika, ambako migogoro na misukosuko ya kiuchumi bado ni mikali.”

Hiyo ni sehemu ya taarifa ya Umoja wa Afrika Jumamosoa, baada ya Israel na Marekani kuanzisha mashambulio dhidi ya Iran. Umoja wa Afrika pia umetaka pande zinazopigana kujizuia, kupunguza mvutano na kuendelea na mazungumzo.

Turudi nyumba kidogo: Wakati Urusi inaivamia Ukraine miezi ya mwanzoni mwaka 2022, Afrika ilianza kuona makali ya vita hivyo baada kutokea mgogoro wa chakula, ikiwemo kupanda kwa gharama ya chakula hasa ngano na mafuta.

Katika ripoti ya Shirika la Fedha Duniani (IMF) iliyochapishwa Aprili mwaka huo, ilisema, “baadhi ya mataifa ambayo yanaathirika moja kwa moja na vita vya Ukraine kwa kutegemea uagizwaji wa ngano kutoka nchi hiyo na Urusi kwa asililia 85 ni pamoja na Tanzania, Ivory Coast, Senegal na Msumbiji.”

Haikuwa Afrika pekee, dunia nzima iliona makali ya vita hivyo ambavyo bado vinaendelea. Ni kutokana na ukweli kwamba hadi vita vinaanza, Urusi ndiyo nchi inayoongoza katika mauzo ya ngano duniani ikifuatiwa na Ukraine.

Turudi katika vita vya Mashariki ya Kati vya sasa. Bila shaka muathirika mkubwa katika vita hivi atakuwa ni Iran, ambaye amezungukwa na mashambulizi ya Marekani na Israel. Lakini Afrika nayo itaathirika kwa namna ipi?

Moshi

Chanzo cha picha, Reuters

Mafuta

Kwa mujibu wa shirika la habari la Uingereza Reuters, likimnukuu afisa mmoja wa Umoja wa Ulaya ambaye amesema meli zimekuwa zikipokea ujumbe kutoka Jeshi la Iran likisema hakuna meli inayoruhusiwa kupita katika Mlango wa Bahari wa Hormuz.

Mlango huu ni njia muhimu ya kusafirisha mafuta duniani, takribani mapipa milioni 20 ya mafuta kwa siku hupitia, yakiwakilisha 20-25% ya biashara ya mafuta ya baharini duniani na moja ya tano ya matumizi ya mafuta duniani.

Kulingana na Shirika la Taarifa kuhusu Nishati la Marekani (EIA), mapipa milioni 20 ya mafuta yalisafirishwa kupitia Mlango wa Bahari wa Hormuz kila siku mwaka 2024.

Hiyo ni sawa na karibu dola bilioni 500 katika biashara ya nishati ya kila mwaka. Mafuta yanayopita kwenye mlango huu yanatoka Iran, Iraq, Kuwait, Qatar, Saudi Arabia na UAE.

Njia hii ya maji iko kati ya Iran upande wa kaskazini na Oman na Falme za Kiarabu upande wa kusini. Licha ya sehemu kubwa ya mafuta haya kwenda Asia, lakini Afrika inaweza kuathirika pia.

Kwa mujibu wa Taasisi ya Utafiti kuhusu Usalama (ISS), yenye makao makuu Afrika Kusini, usumbufu katika Mlango wa Bahari wa Hormuz – utaongeza bei ya nishati hiyo duniani.

Biashara

Mashambulizi ya Marekani na Israel yamesababisha Iran kulipiza kisasi kwa kufanya mashambulizi katika kambi za kijeshi za Marekani ambazo zipo katika mataifa ya Kiarabu kama Qatar, Bahrain, Saudi Arabia, Jordan na UAE.

Kupanda kwa bei ya mafuta duniani kunaweza kuongeza gharama za juu za usafiri na nishati kwa ndani. Hilo litaongeza gharama ya bidhaa zinazoagizwa kutoka nje na usafirishaji wa bidhaa ndani kwa mataifa ya Afrika.

Nchi nyingi za Kiafrika zinategemea sana bidhaa kutoka nje, na kukatizwa kwa njia hii ya biashara na gharama kubwa za usafirishaji kunaweza kuchangia mfumuko wa bei.

Kenya imesema mashambulizi hayo yanaweza kuathiri moja kwa moja mauzo ya nje ya nchi, ikiwa ni pamoja na chai, kahawa, maua, nyama, na mboga, ambazo hutegemea sana masoko ya Mashariki ya Kati.

Tanzania inasafirisha kahawa, korosho, karafuu, na bidhaa zingine kwa mataifa ya Ghuba. Mashambulizi katika Mashariki ya Kati yanaweza kuathiri safari za meli na biashara, na kuathiri uchumi wa nchi hizi.

Ripoti zinaeleza kuwa mashirika kadhaa ya ndege ya kimataifa yamefuta, kusimamisha au kubadilisha njia za ndege kwenda na kuvuka Mashariki ya Kati kutokana na wasiwasi wa usalama.

Athari za hatua hii zinaweza kujumuisha nauli kupanda bei na ucheleweshaji wa safari – na kuathiri safari za biashara, masomo na kidini.

Usalama

Iran imeamua kutumia mbinu ya kushambulia kambi za kijeshi katika mataifa ya Kiarabu. Nchi kadhaa za Afrika zina kambi za kijeshi za Marekani. Djbout ni moja ya nchi ambayo makombora ya Iran yana uwezo wa kufika.

Kutokana na ukaribu wa Iran na Djbout, makombora ya Iran ya masafa ya kati kilomita 1,000 hadi 3,000 yanaweza kufika Pembe ya Afrika. Djibouti ni wenyeji wa kambi ya jeshi la Marekani ya Lemonnier.

Ikiwa Iran itaendelea na mbinu ya kushambulia kambi za kijeshi za Marekani, nchi hii ya Afrika iko ndani ya masafa ya makombora ya Iran. Ikiwa mashambulizi yatatokea, yatavuruga usalama wa Djbout.

Usalama wa raia kutoka mataifa ya Afrika wanaoishi Mashariki ya Kati ni suala jingine muhimu. Jumamosi, kombora la Iran lililopiga katika mji wa Abu Dhabi limeua mfanyakazi mmoja mwenye asili Asia.

Inaeleweka kuwa Waafrika wengi wako katika nchi za Kiarabu kwa shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na masomo na kazi. Kuendelea kwa mashambulizi haya pia kunahatarisha usalama wao.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania imesema inafuatilia kwa karibu hali ya mambo huku ikiwashauri raia wa Tanzania katika maeneo yaliyoathiriwa kuendelea kuwa macho.

Bila shaka athari ya mashambulizi haya, yatategemea urefu wa muda ambao mashambulizi yatafanyika. Kadiri mashambulizi yanavyochukua siku nyingi, ndivyo athari za kiuchumi, kibiashara na maisha ya watu zitakavyozidi kuongezekas Mashariki ya Kati na Afrika pia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *