Dar es Salaam. Kanisa Anglikana la Mtakatifu Msalaba Mbagala jijini Dar es Salaam, limetangaza mpango wa kufungisha ndoa za pamoja Aprili 1, 2026 kwa waumini wanaoishi na wenza wao bila kufunga ndoa takatifu.
Mpango huo umetangazwa leo Machi 1, 2026 na Mchungaji wa Kanisa Anglikana Mtakatifu Msalaba Mbagala, Rogers Mshuza wakati wa mahubiri yake ya Jumapili kanisani hapo.
Mahubiri hayo ni ya kwanza kuongoza kanisani hapo tangu alipohamishiwa akitokea Kanisa la Anglikana Sofu Kibaha, Mkoa wa Pwani.
Amesema hatua hiyo inalenga kuimarisha maadili ya kanisa na kusaidia waumini kuishi maisha yanayompendeza Mungu, akisisitiza ndoa hizo zitafungwa kwa utaratibu wa pamoja na hazitahitaji gharama kubwa kama ambavyo baadhi ya waumini wamekuwa wakitumia katika maandalizi ya sherehe.
Amesema kanisa lipo tayari kusaidia pale ambapo kutakuwa na changamoto.
Akinukuu tangazo la katibu wa kanisa lililosomwa ibadani hapo, Msuza amesema idadi ya waumini waliohudhuria ibada ya Jumapili iliyopita ilikuwa zaidi ya 100 huku washiriki wapatao 30 tu ndio walioshiriki ushirika mtakatifu, hivyo ni kiashiria tosha kuwa wengi wanaishi bila kufunga ndoa takatifu.
Mpango huo umetangazwa leo Machi 1, 2026 na Mchungaji wa Kanisa Anglikana Mtakatifu Msalaba Mbagala, Rogers Mshuza wakati wa mahubiri yake ya Jumapili kanisani hapo.
“Waumini waliosali Jumapili iliyopita ni zaidi ya 100 lakini washiriki 30 mmoja mmoja inaonekana wengi ni watu wazima hawana ndoa, ndiyo moja ya kizuizi, sasa nawatangazia tarehe 1 Aprili 2026, Jumatatu ya Pasaka, nitafungisha ndoa za pamoja hapa kanisani,” alinukuliwa mchungaji huyo.
Mbali na suala la ndoa, Mshuza amewataka waumini kujiepusha na vitendo viovu vinavyokwamisha maendeleo ya kiimani, kijamii na kiuchumi akisisitiza kuwa dhambi humuweka mtu mbali na baraka hata kama ataishi nje ya nchi.
Amewahimiza pia kuwa wavumilivu, kutenda mema katika jamii na kushirikiana katika kazi za kanisa ili kuwaletea maendeleo ya kiroho na kiuchumi waumini wote.
Aidha, amewataka waumini kuiombea nchi na viongozi wake akisisitiza mamlaka zote hutoka kwa Mungu na kwamba ni muhimu kudumisha amani na mshikamano katika jamii.
Baadhi ya waumini walishukuru hatua hiyo wakisema itawarahisishia kufunga ndoa na kuishi maisha yanayompendeza Mungu.
Miongoni mwao ni Veronica Yohana na Daniel Jackson waliodai gharama ndogo zitawasaidia wengi waliokuwa wakishindwa kufunga ndoa kutokana na kutokuwa na uwezo.