
BAADA ya mwenendo mbaya wa matokeo ya Ligi Kuu Bara hadi sasa, Kocha wa Fountain Gate, Mohamed Ismail ‘Laizer’ amesema kazi kubwa aliyonayo katika kikosi hicho ni kutengeneza saikolojia ya wachezaji ili wafanye vizuri kwa mechi zijazo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Laizer amesema wachezaji wa timu hiyo wanatengeneza nafasi nyingi za kufunga, ingawa suala nzima la utumiaji ndio imekuwa ni changamoto kubwa iliyopo kikosini, japo anaendelea kupambana nalo siku baada ya siku.
“Ni suala la saikolojia tu kwa sababu sio kwamba nafasi hatuzitengenezi za kutosha, mechi yetu ya mwisho tuliyofungwa na TRA United mabao 4-1, tulicheza vizuri hasa kipindi cha pili, hivyo tunahitaji kuendelea kuanzia pale,” amesema Laizer.
Fountain ndio timu pekee tangu mwaka 2026, umeanza haijaonja ladha ya ushindi katika mechi za Ligi Kuu kwani mara ya mwisho kikosi hicho kushinda ilikuwa ni Novemba 26 mwaka jana ilipoinyoa Tanzania Prisons kwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Babati Manyara.
Timu hii iliyohamishia makazi yake kwa sasa jijini Arusha ikiutumia Uwanja wa Black Rhino uliopo Karatu, tangu ushindi huo dhidi ya Prisons imecheza mechi sita na kati ya hizo imechapwa minne na kutoka sare miwili.
Msimu uliopita wa 2024-2025, Fountain ilimaliza nafasi ya 14 na pointi 29, katika Ligi Kuu Bara na kukutana na Tanzania Prisons iliyomaliza nafasi ya 13 na pointi 31, ambapo kwenye mechi ya mtoano kikosi hicho kilichapwa jumla ya mabao 4-2.
Baada ya hapo, Fountain ikacheza tena ‘Play-Off’, ya kubakia Ligi Kuu, ambapo iliitoa Stand United kwa jumla ya mabao 5-1, kufuatia kikosi hicho cha ‘Chama la Wana’, kinachoshiriki Championship, kuifunga Geita Gold kwa jumla ya mabao 4-2.
Hadi sasa msimu huu wa 2025-2026, Fountain Gate inashika nafasi ya 15 na pointi 12, baada ya kucheza mechi 14, ambapo kati ya hizo imeshinda mitatu, ikitoka sare mitatu na kupoteza minane, huku ikifunga mabao sita na kuruhusu mengine 18.