SHINYANGA: CHAMA Kikuu cha Ushirika mkoani Shinyanga (SHIRECU) kimenunua tani 387 za dengu kwa thamani ya Sh milioni 386 kutoka Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) sita katika msimu wa kuanzia Julai hadi Septemba mwaka 2025.
Hayo yamesemwa na Meneja wa Chama hicho, Alphonce Makasi alipokuwa akitoa taarifa kwenye Mkutano Mkuu wa 31 uliohudhuliwa na wajumbe 202 kati ya wajumbe halali 214 kutoka kwenye vyama vya msingi (Amco’s) 107.

Makasi amesema kupitia Amco’s sita za Sayu, Bunambila, Iselamagazi, Mwamadilana, Mwamadulu nakuweza kununua zaidi ya tani 387 sawa na kilo 387,750 na kuuza kilo 382,300 na kilo 5450 zimebaki kwaajili ya mbegu na faida yake watapata Sh milioni 8 ambazo zitaendesha ushirika.
“Ingawa tumetenga Sh bilioni moja kwa ajili ya ununuzi wa mazao mchanganyiko changamoto iliyokuwepo ni kukosekana kwa mfumo wa stakabadhi ghalani unaowezesha kuleta ushindani wa haki katika soko la mazao,”amesema Makasi.
Makasi amesema pia wamekamilisha duka la kuuza pembejeo lenye thamani ya Sh milioni 50 litakalohudumia zaidi ya wakulima 7,000 kutoka maeneo tofauti tofauti ndani ya mkoa huu.

Makasi amesema upo mpango ulioanzishwa na bodi juu ya ujenzi wa Maghala sita ikiwemo kuomba tena ridhaa kwa wanachama kutoa kibali cha kukarabati ghala lililopo eneo la kurasini Dar es Salaam kutokana na mwaka wa fedha uliopita kukosa fedha kwaajili ya utekelezaji huo.
Mwenyekiti wa Bodi ya SHIRECU, Naomi Chaba amesema vipaumbele kwa mwaka 2026/2027 ni kuhakikisha wanajiendesha kibiashara na kuwajali wakulima wao huku akieleza kuwepo zoezi la kununua zao la pamba na mazao mchanganyiko ikiwemo kufufua kiwanda kipya cha kusindika alizeti.
Mrajis Msaidizi Mkoa wa Shinyanga Ibrahimu Kakozi alishauri vyama vya msingi vyote (amco’s) vitoe ushirikiano na namna ya kujitathimini wao kwani wanapofanya vibaya ndipo wanakuwa wanakwamisha maendeleo ya shiirecu kufanya vizuri.