
Mbinga. Wakulima wa zao la kahawa katika Wilaya ya Mbinga, mkoani Ruvuma, wameanza kushuhudia ongezeko la tija, ubora na bei ya zao hilo, hali inayochochea matumaini mapya ya kuinua uchumi wa kaya na vijiji kwa ujumla.
Mathalani, msimu wa mwaka jana, bei ya kahawa ilipanda kutoka wastani wa Sh7,000 hadi zaidi ya Sh11,000 kwa kilo moja. Ongezeko hilo lilichangiwa na ubora wa kahawa inayozalishwa pamoja na kuongezeka kwa uelewa wa wakulima kuhusu thamani halisi ya zao hilo.
Mageuzi hayo, yanayotarajiwa kuchochea uzalishaji zaidi katika msimu ujao, yanahusishwa na juhudi za Serikali kwa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali la Hanns R. Neumann Stiftung (HRNS). Kwa kipindi cha miaka mitatu, shirika hilo limekuwa likitekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wakulima wa kahawa kupitia mafunzo ya mbinu bora za kilimo.
Takribani wakulima wadogo 2,000, kupitia vikundi 65 na Vyama vya Ushirika wa Msingi (AMCOS) 10, wamenufaika na mafunzo hayo yaliyolenga kuongeza tija mashambani, kuboresha ubora wa mazao na kuimarisha uelewa wa masoko.
“Mabadiliko haya si ya bei pekee, bali pia ni ya fikra na mtazamo. Wakulima sasa wanaona kilimo kama biashara yenye faida na mustakabali mzuri,” amesema Steven Milinga, Mwenyekiti wa Kikundi cha Ngwindi Group chenye wanachama 29 wenye uwiano wa kijinsia unaokaribiana.
Kwa mujibu wa Milinga, kikundi hicho kimefanikiwa kuzalisha miche 30,000 ya kahawa kati ya lengo la miche 150,000 kupitia mafunzo ya kilimo cha kisasa na ujasiriamali.
Pia, wamepata mkopo wa Sh70 milioni kutoka Halmashauri ya Wilaya kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya kulala wageni katika Kata ya Mpapa, Mbinga Vijijini, hatua inayoashiria kupanuka kwa uwekezaji na vyanzo vya mapato.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa AMCOS ya Kigoti, Grace Ndunguru, amesema mradi huo umeleta mageuzi makubwa katika usimamizi wa ushirika na uzalishaji.
Amesema walipokea mbegu bora kutoka Tanzania Coffee Research Institute (TaCRI), hatua iliyowezesha kuanzishwa kwa vitalu vya miche bora vinavyouzwa kwa wanachama na wakulima wengine. Mapato yatokanayo na uuzaji huo yamewezesha ujenzi wa ofisi ya kisasa ya AMCOS hiyo.
January Komba wa Kikundi cha Namwang’ina, Kata ya Kitanda, amesema msaada wa pembejeo, zikiwemo pampu za maji, viliba na neti za vivuli, umepunguza upotevu wa miche na kuongeza kiwango cha uhai pamoja na tija mashambani.
Akizungumzia mafanikio hayo leo, Machi Mosi, 2026, Mtaalamu wa Kilimo wa HRNS, Isack Lungu, amesema kabla ya mradi huo wakulima wengi walikabiliwa na changamoto za ukosefu wa miche bora, matumizi duni ya pembejeo na usimamizi hafifu wa mashamba.
“Leo tunaona mashamba yenye afya, wakulima wenye maarifa na AMCOS zenye mifumo bora ya uongozi na uwazi,” amesema.
Mbali na kahawa, vikundi vilivyonufaika vimeanzisha miradi mingine ya kiuchumi kama ufugaji wa nyuki na samaki pamoja na kilimo cha maparachichi, hatua inayosaidia kupunguza utegemezi wa zao moja na kuongeza ustahimilivu wa kaya dhidi ya misukosuko ya soko.
Katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, zaidi ya miti 200,000 ya kivuli na matunda imesambazwa kwa wakulima, hatua inayosaidia kuimarisha afya ya udongo na kuongeza uimara wa mashamba dhidi ya hali mbaya ya hewa.
Wadau wameitaka Serikali na washirika wengine kuendeleza uwekezaji katika elimu ya kilimo, miundombinu na uimarishaji wa ushirika, wakisisitiza kuwa uzoefu wa Mbinga unaonyesha wazi kuwa uwekezaji katika maarifa na umoja wa wakulima unaweza kugeuza changamoto kuwa fursa.
Kwa sasa, kahawa ya Mbinga imekuwa zaidi ya zao la biashara; ni chachu ya mageuzi ya kiuchumi, ishara ya umoja wa wakulima na tumaini jipya kwa maelfu ya familia za vijijini.