Ni sahihi kusema hakuna unyonge! Simba imemaliza uteja wa kupoteza michezo mitano dhidi ya Yanga baada ya kulazimisha suluhu kwenye mchezo mkali wa Dabi ya Kariakoo uliopigwa kwenye Uwanja wa Amaan Zanzibar.

Huu ulikuwa mchezo wa kwanza Simba wanaitawala Yanga kwa dakika nyingi katika michezo ya hivi karibuni, huku ikiwatumia wachezaji wake wapya, Libase Gueye, Anicet Oura, Inno Liemba ambao waliipa shida kubwa safu ya ulinzi ya Yanga kwa muda wote wa mchezo na Simba kumaliza ikiwa inaongoza kwa mambo mengi, mashuti yaliyolenga lango 4-3, mashuti yaliyotoka nje 5-4, lakini umiliki wa mchezo vipindi vyote walikuwa mbele kwa jumla ya asilimia 54-46 za Yanga.

Kabla ya mchezo huu, Simba ilikuwa imepoteza michezo sita mfululizo ya ligi dhidi ya Yanga lakini mabadiliko makubwa kwenye kikosi yaliyofanywa na kocha wa timu hiyo Steven Barker yamebadilisha mambo mengi kwenye kikosi hicho.

Hata hivyo, kipindi cha pili Simba ilifanikiwa kuuweka mpira kimiani kupitia kwa mshambuliaji wake Seleman Mwalimu lakini mwamuzi wa akiba aliyoosha kibendera, ingawa marudio ya tukio hayakuonyesha tatizo lolote jambo ambalo limezua gumzo mitandaoni.

Pamoja na Simba kutawala kwenye eneo la kushambulia, lakini ni dhahiri kuwa pongezi kubwa zinakwenda kwa kipa wa kimataifa wa timu ya Yanga, Djigui Diarra kutokana na ubora wa juu ambao alifanikiwa kuuonyesha kwa kuokoa michomo kadhaa mikali na mwisho alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo ambao ulikuwa bora na kuvutia.

Katikati mwa kipindi cha kwanza Dickson Job ambaye ni nahodha wa Yanga aliumia na kumpisha Bakari Nondo Mwamnyeto ambaye alifanikiwa kuituliza timu hiyo kwenye eneo la ulinzi huku akiiwahi mipira mingi ya juu na kuwazuia Simba kupata bao.

Matokeo hayo yanaifanya Yanga iendelee kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi ikiwa na pointi 29 zikiwa ni tano mbele ya Simba iliyopo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 24.

Makocha wamesemaje

”Nafikiri tumecheza vizuri lakini nia yetu tulitaka kupata ushindi kwenye mchezo, tulihitaji kupata pointi tatu ili kupunguza gepu dhidi ya wapinzani wetu, lakini hakuna jinsi tunakwenda kujipanga vizuri,” Steven Barker Simba.

“Hatukucheza vizuri kipindi cha kwanza, nafikiri kipindi cha pili tulikuwa bora na tulitengeneza nafasi na kushindwa kuzitumia, Job alichezewa faulo na ilistahili kadi ya njano kwenye tukio lile, tunakwenda kwenye ligi tena na sasa itakuwa na spidi kubwa sana kwa kuwa kuna mechi karibu karibu, tunatakiwa kujipanga zaidi,” Pedro Concalves Yanga.

MZIZE AKUMBUKWA

Katika mechi ya jana kabla ya kuanza wachezaji wa Yanga walionekana kupiga picha ya jezi ya timu hiyo yenye nmba 24 inayovaliwa na Clement Mzize kama ishara wa kumtakia kila la kheri baada ya kufanyiwa upasuaji mwingine wa goti huko Afrika Kusini.

Mzize aliumia kaatika mechi ya kwanza ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu dhidi ya Wiliete Banguela ya Angola na kuwa nje hadi alipoonekana mwezi uliopi katika mechi ya marudiano ya makundi dhidi ya As FAR Rabat ya Morocco kabla kuelezwa amejitonesha walipokuwa wakijiandaa kuikabili JS Kabylie ya Algeria.

Nyota huyo aliyemaliza kinara wa mabao wa Yanga msimu uliopita akifunga 14, akishika nafasi ya pili nyuma ya kinara wa Ligi Kuu, Jean Charles Ahoua aliyekuwa Simba ni mmoja ya waliofunga mabao mawili yaliyoizamisha Simba na kuipa Yanga ubingwa wa msimu uliopita.

Bao jingine la Yanga katika mechi hiyo iliyopigwa Juni 25 mwaka jana lilifungwa na Pacome Zouzoua ambaye alikuwa jukwaani na baadhi ya nyota wengine katika mechi hiyo ya jana.

KITU KINACHOFUATA

Mara baada ya pambano hilo la saba kwa Simba na Yanga kukutana Zanzibar na la kwanza kwa Ligi Kuu Bara msimu huu, timu hizo zitarudi jijini Dar es Salaam kabla ya kujiandaa na mechi zijazo za Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho.

Yanga itakuwa ya kwanza kucheza keshokutwa Alhamisi ugenini kukabiliana na Singida Black Stars kisha Machi 8 itaumana na Polisi Tanzania katika pambano la 32 Bora la Kombe la Shirikisho (FA) na Machi 12 itaumana na Tanzania Prisons pia ugenini jijini Mbeya na Machi 15 itavaana na Azam.

Kwa upande wa Simba yenyewe itaanza Kombe la Shirikisho Machi 7 dhidi ya B19 FC na Machi 11 itaifuata Singida BS kwa mechi ya Ligi Kuu itakayopigwa ugenini kabla ya kujisogeza mjini Tabora Machi 14 kumalizana na Watoza Ushuru wa TRA United kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi.

VIKOSI VILIVYOANZA JANA;

YANGA: Diarra, Mwenda, Tshabalala, Bacca, Job, Damaro, Maxi, Duke, Depu, Mudathir na Dube

SIMBA: Kassali, Kapombe, Kibabage, Toure, Rushine, Kagoma, Guaye, Kante, Oura, Chama na Inno

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *