Tehran. Mwanazuoni wa Kishia na mjumbe wa Baraza la Walinzi, Alireza Arafi, amechaguliwa kuwa mwakilishi wa wanazuoni wa sheria katika Baraza la Uongozi la Muda la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, chombo kinachotarajiwa kushika majukumu ya kiongozi mkuu hadi atakapoteuliwa mrithi rasmi.
Uteuzi huo umefanywa na Baraza la Utambuzi kufuatia taarifa za kuthibitishwa kwa kifo cha kiongozi mkuu wa Iran, Ali Khamenei, kilichoripotiwa kutokea Machi 1, 2026.
Kwa mujibu wa Kifungu cha 111 cha Katiba ya Iran, baada ya kifo cha kiongozi mkuu, majukumu yake huchukuliwa kwa muda na baraza la watu watatu linaloundwa na rais wa nchi, mkuu wa mhimili wa mahakama na mwakilishi wa wanazuoni wa baraza la walinzi, nafasi ambayo sasa inashikiliwa na Aarafi hadi baraza la wataalamu litakapomteua kiongozi mpya.
Mwanazuoni wa Kishia na mjumbe wa Baraza la Walinzi, Alireza Arafi, amechaguliwa kuwa mwakilishi wa wanazuoni wa sheria katika Baraza la Uongozi la Muda la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Hata hivyo, baraza hilo la muda halina mamlaka kamili ya kiuongozi, maamuzi nyeti ya kijeshi na kiusalama, ikiwamo uteuzi au uondoaji wa makamanda wakuu wa jeshi na walinzi wa mapinduzi, lazima yaidhinishwe na robo tatu ya wajumbe wa baraza la utambuzi.
Hatua hiyo inakuja wakati Iran ikikabiliwa na changamoto za kiusalama kufuatia taarifa za kuuawa kwa makamanda kadhaa waandamizi wa kijeshi, akiwamo Kamanda Mkuu wa Walinzi wa Mapinduzi (IRGC) na Mkuu wa Majeshi ya Pamoja, hali inayolifanya baraza la muda kukabili maamuzi mazito ya uongozi wa vikosi vya ulinzi.
Vyombo vya habari vya ndani na nje, vikiwamo The New York Times, vimeripoti kuwepo kwa ngazi kadhaa za urithi wa madaraka ndani ya mfumo wa Iran, madai ambayo vyombo vilivyo karibu na serikali vimeyaita propaganda na vita ya kisaikolojia.
Aliyekuwa Kiongozi Mkuu wa taifa la Iran, Ayatollah Ali Khamenei ambaye ameuawa kufuatia mashambulizi ya Israel na Marekani.
Mshauri wa IRGC, Ebrahim Jabbari, amesema mipango ya vikosi vya jeshi tayari ilishapangwa na Khamenei kwa muda mrefu, akisisitiza kuwa mabadiliko ya uongozi hayatayumbisha mwelekeo wa kijeshi wa nchi hiyo.
Wasifu wa Arafi
Aarafi, mwenye umri wa miaka 70, alizaliwa mwaka 1955 katika mji wa Meybod, mkoa wa Yazd. Alipata mafunzo ya awali ya dini kutoka kwa baba yake kabla ya kuhamia Qom ambako alisomea katika seminari za Kishia chini ya wanazuoni wakuu.
Amefundisha katika taasisi kadhaa za elimu ya juu, zikiwamo Chuo Kikuu cha Allameh Tabataba’i na Chuo Kikuu cha Tarbiat Modarres, na kuongoza taasisi ya kimataifa ya elimu ya dini ya Al-Mustafa tangu ilipoanzishwa 2008 kwa amri ya Khamenei.
Alireza Arafi alipokutana na Pope Francis enzi za uhai wake katika makao ya Vatican, Mei 2022, alipokuwa Rais wa Seminari za Kiislamu za Iran. Picha na Reuters
Pia amewahi kuwa Imamu wa Ijumaa wa Meybod tangu 1992 na Qom tangu 1994, huku mwaka 2016 akiteuliwa kuwa mkuu wa seminari za Qom na mtandao wa seminari nchini Iran.
Kisiasa, Aarafi aliteuliwa mwaka 2019 kuwa mjumbe wa Baraza la Walinzi kwa amri ya Khamenei, kabla ya kushinda uchaguzi wa Baraza la Wataalamu mwaka 2023 katika jimbo la Tehran kwa zaidi ya kura 888,000.
Wachambuzi wa Iran wanamtaja Aarafi kuwa miongoni mwa wanazuoni waliokuwa karibu na Khamenei na waliokuwa wakitazamwa miongoni mwa majina yanayoweza kuzingatiwa katika urithi wa uongozi wa juu wa kidini.
Katika hotuba zake, amekuwa akisisitiza mwendelezo wa sera za Iran kuhusu ulinzi, upinzani dhidi ya Marekani na sera za kijamii za Jamhuri ya Kiislamu, akijitambulisha kama mtetezi wa busara ya Kiislamu dhidi ya mifumo ya Magharibi.
Kwa kuteuliwa kwake katika Baraza la Uongozi la Muda, Aarafi sasa anaingia moja kwa moja katika kiini cha mpito wa madaraka Iran, huku Baraza la Wataalamu likitarajiwa kuanza mchakato wa kumteua Kiongozi Mkuu mpya katika kipindi kijacho.
Imeandikwa kwa msaada wa Mashirika